Video: Serikali Ya Tanzania Yajibu Meli Iliyokamatwa Na Dawa Za Kulevya El Salvador

Bakari Mahundu
February 26, 2026
0 Comments

Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, amezungumzia tukio la kukamatwa kwa meli ya FMS Eagle katika nchi ya El Salvador, baada ya kubainika kuwa ilikuwa imebeba shehena kubwa ya dawa za kulevya.

Katika ufafanuzi wake, Msigwa amekiri kuwa meli hiyo ilikuwa imesajiliwa nchini Tanzania kupitia upande wa Zanzibar, akisisitiza kuwa mamlaka za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zilichukua hatua za haraka mara tu taarifa za tukio hilo zilipopatikana, ikiwemo hatua za kisheria na kiutawala dhidi ya meli hiyo ikiwemo kutozwa faini kwa kampuni inayomiliki meli hiyo na kufutwa usajili wa meli hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mamlaka za El Salvador, meli ya FMS Eagle ilikamatwa ikiwa na tani 6.6 za dawa za kulevya. Katika operesheni hiyo, watu 10 kutoka nchi za Colombia, Nicaragua, Panama na Ecuador walikamatwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Hadi sasa, mamlaka husika hazijaweka wazi dawa hizo zilikuwa zikitoka nchi gani wala zilikuwa zikielekea wapi, huku uchunguzi wa kina ukiendelea kufanyika kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa za usalama.