Bakari Mahundu
February 26, 2026
0 Comments
Leo Februari 26, 2026, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba ameendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Manyara, wilayani Kiteto, ambako amewahutubia wananchi, kusikiliza kero zao na kuzitolea ufumbuzi.
Katika mkutano huo, mwananchi Ngobi Zuberi aliibua kero akidai wafugaji kulisha mifugo kwenye shamba lake lote hali iliyosababisha kushindwa kuvuna chochote. Aidha, alilalamikia eneo la shamba la marehemu baba yake kuchukuliwa na ofisi ya kijiji bila kufuata utaratibu.
Waziri Mkuu alimpa nafasi ya kujitetea Diwani pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji, ambao walieleza kuwa eneo hilo lilichukuliwa kwa kuzingatia utaratibu wa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Akizungumza kufuatia maelezo hayo, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa maeneo yanayochukuliwa kwa ajili ya mpango wa matumizi bora ya ardhi yafidiwe na masuala hayo yashughulikiwe kwa misingi ya kindugu ili kuepusha migogoro inayoweza kuvuruga umoja.
Pia alikataza migogoro ya wakulima na wafugaji, akibainisha kuwa migogoro hiyo ni tishio kwa usalama na umoja wa taifa. Alitoa mfano wa mgogoro uliowahi kutokea mkoani Morogoro uliosababisha mkulima kuuawa baada ya kupigwa mshale.
“Tuepuke kabisa kuleta uhasama kwenye jamii hizi. Tusifikishe mahali mkulima amuone mfugaji kama adui, wala mfugaji amuone mkulima kama adui. Hata mkipigana ardhi haiongezeki, hata mkichukiana ardhi haiongezeki; mtauana bure. Timalize mambo haya kwa amani ili yasitokee,” alisisitiza Waziri Mkuu.