Dar es Salaam. Baadhi ya watu kurasa zao za mafanikio huanza kufunuliwa baada ya kupitia magumu, misukosuko na kukatishwa tamaa.
Kama dhahabu ili ing’ae ni lazima ipitishwe kwenye moto; ndivyo ilivyokuwa kwa Nisa Kitenge, binti wa miaka 24 anayejishughulisha na utengenezaji maudhui mtandaoni.
Nisa amejizolea umaarufu kwenye mitandao ya kijamii hasa Instagram na TikTok kutokana na maudhui yake yanayotoa elimu ya namna mtu anavyoweza kula lishe bora kwa gharama nafuu.
Ni kutokana na kazi hiyo, amejizolea wafuasi wengi na kumwezesha kuwa balozi wa taasisi kadhaa nchini.
Hata hivyo, safari yake ya kufika alipo sasa haikuwa rahisi; ni yenye milima na mabonde ambayo hakuruhusu imkatishe tamaa kufikia ndoto zake.
Anaeleza aligeuza changamoto hizo kuwa fursa na chachu ya ubunifu katika utengenezaji maudhui mitandaoni.
Kupitia juhudi binafsi, nidhamu na matumizi ya majukwaa ya kidijitali alijiajiri, kujenga chapa yake na hatimaye kufungua milango ya mafanikio ambayo awali ilionekana imefungwa.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Nisa anasema ana miezi sita tangu apate umaarufu kupitia utengenezaji maudhui mitandaoni lakini safari ya kufikia hapo ilimchukua zaidi ya miaka mitano.
“Kitaaluma nimesoma masuala ya masoko nikijiegemeza zaidi katika mitandao ya kijamii, hivyo ninachokifanya ni kama kinaendana na fani niliyosoma,” anasema.
Anaeleza miaka mitano iliyopita baada ya kumaliza masomo alitafuta kazi mara kadhaa bila mafanikio, ikiwamo kuomba kusimamia akaunti za mitandao ya kijamii ya baadhi ya wafanyabiashara.
“Nilichoambulia ni kukatishwa tamaa, walidai kama akaunti zangu za mitandao ya kijamii zina wafuasi wachache nitaweza vipi kuwafanya wao wapate wafuasi wengi? Hawakuwa tayari kuniruhusu kuonesha uwezo wangu,” anasimulia.
Nisa anasema kukataliwa kulimuumiza lakini baadaye aliwaza ni kwa namna gani anaweza kupata wafuasi wengi kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.
Ni katika dimbwi la mawazo ya namna ya kuja na ubunifu tofauti katika kutengeneza maudhui mtandaoni, alitumia siku kadhaa kupita kwenye mitandao ya kijamii.
Anaeleza alibaini baadhi ya watu, hususani wanawake kwenye mitandao ya kijamii wanapenda kuonesha maisha yasiyo na uhalisia wa hali zao za kiuchumi.
“Baadhi yao wanaonesha maisha ya kifahari ambayo kiuhalisia hayaendani na kipato chao, niliona watu wachache wanaonesha maisha yao halisi na hapa ndipo nilipoiona fursa,” anasema.
Ni kutokana na hayo, anaeleza ndipo wazo la kutengeneza maudhui ya ‘kula kwa bajeti’ lilipomjia kichwani, likirahisishwa na mazingira anayoishi huko Manzese, jijini Dar es Salaam, ambako gharama za maisha ni nafuu kulinganisha na maeneo mengine.
Dhamira yake anasema ni kuonesha maisha halisi ya mtu wa kipato cha kawaida anavyoweza kupanga matumizi na kuishi ndani ya uwezo wake bila presha ya kuiga maisha ya kifahari.
“Natengeneza maudhui yanayohusu kubana matumizi hasa katika chakula ili kipato chako kiendane na matumizi yako. Unachopata, kata kidogo, pangilia matumizi ya kila siku,” anasema.
Anasema alitaka kuionesha jamii fursa zilizopo katika maeneo ya ‘uswahilini’ isiwe panaongelewa kwa mambo mabaya tu, bali pia upande wa mema katika maeneo hayo.
“Naishi Manzese kwa zaidi ya miaka mitano. Nayajua masoko, bei za bidhaa na maisha ya huku ambako kidogo kuna unafuu. Lakini hayo hayaelezwi, mara nyingi maeneo kama haya hutajwa kwa mambo mabaya. Nikaamua kuja tofauti kwa kuonesha uhalisia wa maisha yangu,” anasema.
Video ya ‘tupike kwa bukujero’ ni kati ya zilizofanya vizuri katika mitandao ya kijamii na kumtambulisha Nisa.
Akizungumzia video hiyo, anasema aliirekodi siku kadhaa kabla ya kuipakia kwenye mtandao, akieleza alikuwa na hofu ya jinsi gani itapokewa na jamii.
Anaeleza aliuvaa ujasiri, akaipakia kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, wakati huo akiwa na wasiwasi wa namna itakavyopokewa.
Katikati ya hofu yake, video hiyo ilipokewa vyema na kuwa chanzo cha yeye kuanza kufahamika.
“Kwa mara ya kwanza wakati narekodi video ile sikujua kama itapokewa kwa ukubwa maana nilikuwa naonesha tu maisha yangu ya kawaida. Sikujua kama kuna watu pesa hiyo ambayo mimi nilinunua mahitaji yangu yote ya kupikia wao wananunua nyanya tu,” anasema.
“Nilipokea simu na ujumbe kutoka kwa watu wakieleza hawaamini, wengine wakiniuliza soko ambalo nimenunua bidhaa zangu.”
Tukio hilo anasema lilifungua macho ya wengi kutambua kuwa maisha yanatofautiana kulingana na maeneo na hali za watu.
Anatoa mfano wa maeneo ya Manzese, Tandale, Mabibo na Temeke kuwa ni sehemu ambako watu wanaishi kwa gharama nafuu zaidi kulinganisha na mengine.
“Maisha ni magumu kila sehemu, lakini kuna maeneo yana nafuu. Tusitishane maisha. Tusiishi kwa kukariri,” anasisitiza.
Anashukuru kupitia utengenezaji wa maudhui mtandaoni anapata kipato kinachomsaidia yeye na familia yake, akiwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanne.
Anasema licha ya manufaa anayopata pia anakumbana na changamoto, zikiwamo kukosekana huduma ya intaneti na kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo.
Anasema changamoto hizo kuna wakati humkwamisha kufanya kazi.
Vilevile, kutokana na kuchagua kuonyesha uhalisia wa maisha, kuna wakati hukumbana na watu wanaomdhihaki wakidhani anafanya hayo ili kuomba msaada.
Nisa anatamani kuvuka mipaka ili kuyafikia maeneo mengine ya mikoa yote ya Tanzania.
Pia, kutembelea nchi za Afrika Mashariki kuonesha uhalisia wa namna mtu anayeishi katika maeneo hayo anaweza kuishi ndani ya bajeti kulingana na kipato chake.
Mbali ya hayo, anawaasa vijana akiwataka kuamini katika ndoto zao bila ya kukatishwa tamaa.
Anawahimiza kuishi maisha yao ya uhalisia, wakiacha kuiga wanayoyaona mitandaoni, ambayo wakati mwingine hayaendani na kipato chao.
Kupitia maudhui yake, ameendelea kuwahamasisha vijana kuishi ndani ya uwezo wao, kupanga bajeti na kuthamini kile kidogo walichonacho akithibitisha kuwa uhalisia nao ni maudhui yenye mvuto mkubwa katika ulimwengu wa kidijitali.