Dar es Salaam. Wakati Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akitafuta suluhisho la foleni nchini, wadau mbalimbali wametoa mapendekezo ya namna ya kumaliza changamoto hiyo inayodidimiza uchumi wa Watanzania.
Februari 23, 2026, wakati akizungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Fani za Uhandisi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ulega alitangaza zawadi ya Sh10 milioni kwa mwanafunzi atakayebuni mradi utakaosaidia kutatua changamoto ya msongamano wa magari.
Wakati Serikali ikiangalia ubunifu kama sehemu ya suluhu, wadau wa sekta ya usafirishaji wanaona kuna haja ya kufanya mageuzi ya kimkakati katika upangaji wa miji na usimamizi wa miundombinu.
Vilevile, wanaangazia suala la mipango miji kama chanzo cha tatizo hilo huku wakipendekeza uboreshaji wa mipango miji hasa katika maeneo yanayokua, huku wakipendekeza Dar es Salaam kujengewa miundombinu ya kisasa itakayoleta tija.
Jarida Mansoura Engineering 2024 la nchini Misri linaloelezea matokeo ya foleni katika sekta ya usafiri limefafanua kuwa, foleni husababisha upotevu mkubwa wa muda, ambao ungetumika katika uzalishaji kwa wafanyakazi na wafanyabiashara.
Pia, kutokana na magari hayo kukaa kwa muda mrefu kwenye foleni athari ambayo hujitokeza ni kutumia mafuta mengi zaidi jambo linaloongeza utoaji wa gesi ya ukaa (CO2) na gesi nyingine zenye sumu.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa sekta ya usafirishaji inachangia takriban asilimia 25 ya uzalishaji wa gesi chafu duniani na foleni huchochea hali hii kwa kutoa kiasi kikubwa cha hewa ukaa ikilinganishwa na magari yanayotembea.
Vilevile, jarida hilo linaeleza kuwa foleni zina uhusiano wa moja kwa moja na ongezeko la ajali za barabarani na vifo. Kadhalika, uchafuzi wa hewa unaosababishwa na msongamano wa magari huongeza hatari ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji, magonjwa ya moyo na saratani.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2010 ya Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), foleni za magari hutafuna hadi zaidi ya asilimia 20 ya faida kwenye biashara.
Kwa Dar es Salaam, jiji la kibiashara nchini, kulingana na ripoti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) 2010, ilionyesha kila siku Sh4 bilioni hupotea kwenye foleni kutokana na mafuta, kushuka kwa uzalishaji na ucheleweshaji wa bidhaa sokoni.
Ripoti ya mwaka 2017 iliyoandaliwa na Kampuni ya ushauri ya Disnney International Consultancy chini ya iliyokuwa Mamlaka Udhibiti Usafiri wa Ardhini na Majini (Sumatra), sasa Latra, ilibaini chanzo cha foleni Dar es Salaam kuwa ni ukosefu wa maegesho ya magari barabara ya Sokoine kwa abiria wanaosafiri kwenda na kurudi kutoka Zanzibar.
Sababu nyingine ambayo ilibainika kuwa ni chanzo cha foleni, ni namna askari wa usalama barabarani wanavyodhibiti magari.
Wakati sababu hizo zikibainika Dar es Salaam, jijini Mwanza, sababu ya foleni inatajwa kuwa viwanda vya uzalishaji, maghala na vituo vya uhifadhi mafuta kujengwa katikati ya jiji.
Pia, baadhi ya maeneo kukosa maegesho ya magari na usafiri wa umma ni moja ya sababu inayotajwa sababu ya foleni jijini Mwanza.
Ikumbukwe kwamba miji yote mikubwa, usafiri unaotumika ni mabasi yaendayo haraka (BRT), magari binafsi, magari ya umma, bajaji pamoja na pikipiki maarufu kama bodaboda.
Wakati foleni sasa ikionekana kuwa tishio, Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat) kupitia ripoti yake ya majiji duniani ya mwaka 2020, ilionya ongezeko la watu mijini kufikia asilimia 68 mwaka 2050 kutoka asilimia 55.
Hali hiyo inakadiriwa kuchangia ongezeko la idadi ya magari barabarani kutokana na mabadiliko ya mfumo wa maisha.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa) Chuki Shaban, amesema majiji makubwa yanahitaji mbinu mahsusi kulingana na mazingira yake.
Kwa Dar es Salaam, anaamini msongamano kwa kiasi kikubwa unachangiwa na mizigo inayotoka bandarini na kusafirishwa kwa malori yanayopita katikati ya jiji.
Amesema kukamilika kwa bandari ya Kwala kunaweza kuwa miongoni mwa majawabu ya tatizo hilo kwa kuwezesha malori kupokea na kushusha mizigo nje ya mji badala ya kuingia katikati ya jiji.
“Tunapaswa kuangalia pia, upangaji wa taasisi na miundombinu. Kuna vyuo na maghala katikati ya miji. Vingejengwa nje ya mji, tungepunguza msongamano wa magari hasa malori,” amesema.
Chuki amependekeza kuanzishwa kwa miji mipya yenye miundombinu ya kisasa nje ya miji ya zamani badala ya kuendelea kuboresha maeneo yaliyojaa tayari.
Ametolea mfano Soko la Kariakoo akisema licha ya maboresho yaliyofanyika, barabara zake haziwezi kuhimili wingi wa magari unaoongezeka kila mwaka.
Akichangia hilo, Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo, amesema ufinyu wa miundombinu na udhaifu wa usafiri wa umma ni chanzo kikuu cha foleni.
“Tunapaswa kuboresha usafiri wa umma. Ukiwa bora na wa uhakika, watu wengi wataacha kutumia magari binafsi wanapoingia mjini,” amesema, akiongeza kuwa ongezeko la ununuzi wa magari binafsi linachangiwa na kukosekana kwa usafiri wa uhakika.
Naye Profesa wa Uchumi, Dk Abel Kinyondo amesema chanzo kikuu cha foleni katika majiji makubwa ni makosa ya upangaji wa miji, lakini bado kuna nafasi ya kurekebisha hali hiyo.
Amesema suluhu ya muda mrefu ni kujenga barabara za pembezoni (ring roads) kuelekea maeneo yenye shughuli nyingi za biashara ili kupunguza magari kuingia katikati ya jiji. Pia ameshauri matumizi ya Reli ya Kisasa (SGR) kusafirisha mizigo nje ya miji badala ya kutegemea malori.
“Tunapoondoa mizigo katikati ya jiji tunapunguza foleni kwa kiasi kikubwa. Mabasi yaendayo haraka pia yaliletwa kupunguza magari mengine barabarani, si kuwafanya watu wafike haraka tu,” amesema.
Ameongeza kuwa kunahitajika utashi wa kisiasa katika kusimamia sera, ikiwemo kudhibiti daladala katika njia za mabasi yaendayo haraka na kupunguza malori yanayoingia mijini.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude ameona kuwa maboresho ya miundombinu katika maeneo korofi, ikiwemo ujenzi wa madaraja ya juu (flyover), ni hatua ya haraka inayoweza kupunguza msongamano.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa suluhu ya kudumu ni usafiri bora wa umma.
Ametoa mfano wa awamu za mwanzo za mabasi yaendayo haraka eneo la Kimara, ambapo wananchi walikuwa wakipaki magari yao na kutumia mabasi hayo kutokana na uwepo wa maeneo maalumu ya maegesho.
“Baada ya huduma hiyo kukumbwa na changamoto, watu wakarejea kutumia magari binafsi. Hii inaonyesha wazi kuwa usafiri wa umma ukiwa bora, watu wako tayari kuutumia,” amesema.