BAADA ya uongozi wa Singida Black Stars kutangaza kumsimamisha kwa miezi mitatu Khalid Aucho kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na kuchelewa kazini, kiungo huyo raia wa Uganda, ameonekana kujibu kupitia ujumbe aliouchapisha katika ukurasa wake wa Instagram.
Taarifa ya Singida Black Stars iliyotolewa leo Februari 27, 2026 na ofisi ya mtendaji mkuu wa klabu hiyo, imebainisha Aucho amesimamishwa sambamba na kipa Amas Obasogie, ambaye naye anatumikia adhabu ya miezi mitatu kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazohusiana na upangaji wa matokeo.
Kupitia ujumbe wake, Aucho ameweka bayana kuwa katika maisha yake yote ya soka amekuwa akijitambulisha kwa weledi, nidhamu na heshima kwa kila klabu aliyowahi kuitumikia.
Amesisitiza kuwa tangu aanze taaluma yake hajawahi kuhusishwa na tukio lolote la utovu wa nidhamu, kwani anatambua wajibu na maadili yanayopaswa kuzingatiwa na mchezaji wa kulipwa.
Aidha, amewashukuru mashabiki wake kwa kuendelea kusimama naye katika kipindi hiki kigumu, akieleza imani yake kuwa hali iliyopo itapita na mambo yatakuwa sawa.
“Nimekuwa nikijituma kwa taaluma na heshima kubwa kwa kila klabu niliyowahi kuitumikia. Katika miaka yangu yote ya soka, sijawahi kuhusishwa na suala lolote la utovu wa nidhamu kwa sababu ninafahamu wajibu wangu kama mchezaji wa kulipwa. Kwa mashabiki wangu wapendwa ambao mmekuwa na mimi wakati wote, nawashukuru kwa msaada wenu endelevu. Hali hii pia itapita,” ameandika Aucho.
Kauli hiyo imezua mjadala miongoni mwa wadau wa soka, huku wengi wakisubiri hatua zaidi kutoka kwa uongozi wa klabu hiyo kuhusu hatima ya mchezaji huyo ndani ya kikosi hicho.