Dube aanika ukweli wa mabao yake

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Prince Dube amesema hashindani na mtu bali anashindana na rekodi zake mwenyewe ndani ya ligi sambamba na kufikia mafanikio ya mataji akiwa ndani ya timu hiyo.

Dube amefunguka hayo baada ya kupachika bao lake la tano msimu huu likiwa ni la 18 kwake kwenye mechi 25 za ligi alizocheza tangu amejiunga na Yanga akitokea Azam FC na ni la 51 kwa misimu yake mitano katika Ligi Kuu Bara tangu alipotua nchini 2021.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dube amesema hajawahi kushindana na mtu yeyote bali mafanikio ya kila mchezaji ndani ya Yanga ni furaha kwake kwani yanasogeza mafanikio yake ya kutwaa makombe huku akiweka wazi kuwa anashindana na kivuli chake mwenyewe.

“Nawashukuru wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kwa kuniamini na kuendelea kunisapoti bila kusahau mashabiki ambao wamekuwa pamoja na mimi katika nyakati zote nzuri na mbaya, nitaendelea kuipambania Yanga na mafanikio yangu binafsi wasinichoke.

“Mchezo wetu juzi ulikuwa bora na wa ushindani kutokana na kukutana na timu bora. Kama wachezaji tulijiandaa vyema kuwapa furaha mashabiki wetu, lakini pia kuhakikisha tunajiweka kwenye kilele cha ubora kuelekea mchezo wetu dhidi ya Simba, tunawaahidi furaha zaidi.

Dube amesema mafanikio ya Yanga yanampa nguvu ya kupambana zaidi kwani anaamini anaweza kutimiza ndoto yake ya kubeba mataji kama alivyokuwa anatamani kabla ya kujiunga na timu hiyo na tayari amebeba mataji ila anatamani hilo liendelee kila msimu.

“Yanga ina timu bora na ya ushindani na tayari wachezaji tumepata muunganiko mzuri kwani wengi tumecheza pamoja kwa muda na kuipa mafanikio timu, lakini pia maingizo mapya yameingia moja kwa moja kwenye mfumo wa timu, tunashirikiana kuhakikisha tunaipa mafanikio timu.”

Msimu wake wa kwanza ndani ya Yanga Dube alifunga mabao 13 wakati alivyokuwa Azam FC msimu wake wa kwanza ndani ya kikosi hicho 2020/21 alifunga mabao 14 hivyo alishindwa kuvunja rekodi yake mwenyewe.

Akiwa na Azam FC amecheza misimu mitatu na nusu amefunga mabao 34 kwenye mechi 54. Msimu wa 2020-2021 alifunga mabao 14, 2021-21 alitupia kambani mara moja kutokana na kusumbuliwa na majeraha yaliyokuwa yamemuweka nje kwa muda mrefu, 2022-23 alifunga mabao 12 na msimu wake wa mwisho kuitumikia Azam FC 2023-24 alicheza miezi sita na kufunga mabao saba.

Katika mabao 13 aliyofunga nyota huyo akiwa na Yanga msimu wake wa kwanza alifunga, hat-trick moja ambayo ndio ilikuwa ya kwanza kwa msimu huo. Dube amefunga mabao hayo matatu kwenye ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mashujaa mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.