Familia inavyoweza kujenga mtindo wa maisha wenye afya

Dar es Salaa. Katika mijadala mingi ya afya ya umma, mara nyingi mada huwa kuhusu hospitali, bima za afya, madaktari na sera za serikali.

Hata hivyo, kuna ukweli muhimu ambao mara nyingi hausikiki vya kutosha: safari ya afya njema haianzi hospitalini, bali huanzia nyumbani.

Familia ndiyo shule ya kwanza ya maisha. Ndani yake ndipo misingi ya tabia, maamuzi na mtazamo wa maisha hujengwa.

Kwa mantiki hiyo, familia ndiyo mhimili mkuu wa kujenga au kubomoa mtindo wa maisha wenye afya kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Ni muhimu kufahamu kwamba mtindo wa maisha wenye afya haujengwi kwa miujiza wala hauhitaji utajiri mkubwa. Badala yake, hujengwa kupitia maamuzi madogo madogo ya kila siku yanayofanywa ndani ya familia. Maamuzi haya yanahusu chakula tunachokula, muda tunaotenga kwa mapumziko, namna tunavyokabiliana na changamoto za maisha, na mifano tunayowaonyesha watoto wetu.

Nguzo ya kwanza ya afya ya familia ni lishe bora. Familia nyingi leo zimejikuta zikitegemea vyakula vya haraka (fast foods) vyenye mafuta mengi, sukari na chumvi kupita kiasi.

Sababu kubwa imekuwa kukosa muda au maarifa sahihi kuhusu lishe bora. Hata hivyo, lishe bora haimaanishi chakula cha gharama kubwa.

 Mboga za majani, matunda ya msimu, nafaka zisizokobolewa, kunde kama maharage na dengu, pamoja na samaki au nyama kwa kiasi, vinatosha kuijenga familia yenye afya. Zaidi ya hayo, wazazi wanapojali lishe yao, watoto huiga tabia hizo bila kulazimishwa.

Pili, familia ina nafasi ya kipekee katika kukuza utamaduni wa mazoezi ya mwili. Mazoezi si lazima yawe ya kwenda gym au kununua vifaa vya gharama kubwa. Kutembea pamoja jioni, kufanya usafi wa mazingira kwa pamoja, kucheza michezo ya watoto au kushughulikia bustani ya nyumbani ni aina nzuri za mazoezi. Watoto wanaokua wakiona wazazi wao wakithamini miili yao hujifunza mapema kwamba mazoezi ni sehemu ya maisha ya kawaida, si adhabu.

Afya ya akili nayo ni eneo muhimu ambalo kwa muda mrefu limepuuzwa katika familia nyingi.

 Shinikizo la maisha, gharama za maisha, matarajio ya jamii na changamoto za kifamilia huathiri sana ustawi wa kiakili. Familia yenye afya hujenga mazingira ya mawasiliano ya wazi, kusikilizana na kuheshimiana.

Mtoto anapokuwa na uhuru wa kueleza hisia zake bila hofu ya kukemewa au kubezwa, hujengeka kisaikolojia na kuwa na ujasiri.

 Vivyo hivyo, wazazi wanapaswa kujifunza kutafuta msaada wanapohisi kulemewa, badala ya kuficha maumivu ndani yao.

Aidha, usingizi na mapumziko ni sehemu muhimu ya afya lakini mara nyingi husahaulika. Utamaduni wa kulala usiku wa manane, unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya simu na televisheni, umeathiri afya ya familia nyingi.

Familia inayoweka ratiba ya pamoja ya kulala, kupunguza matumizi ya skrini nyakati za usiku na kuheshimu muda wa mapumziko hujenga kinga dhidi ya magonjwa mengi yatokanayo na uchovu wa mwili na akili.

Zaidi ya hayo, familia ina jukumu kubwa katika kuzuia magonjwa badala ya kuyasubiri. Hii ni pamoja na kufuata ratiba za chanjo, kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya.

Wazazi wanapochukua hatua za mapema, watoto hujifunza kuwa afya ni jukumu lao binafsi, si suala la kushughulikiwa tu wakati wa dharura.

Zaidi ya yote, mtindo wa maisha wenye afya hujengwa kwa mfano.

Watoto hawafundishwi kwa maneno pekee, bali kwa matendo wanayoyaona kila siku.

Mzazi anayesisitiza ulaji wa mboga huku yeye mwenyewe hafanyi hivyo, au anayekataza matumizi ya pombe na tumbaku huku akivitumia nyumbani, hutuma ujumbe wenye mkanganyiko. Familia yenye afya huishi kile inachokiamini.

Kwa jumla, kujenga mtindo wa maisha wenye afya ndani ya familia ni uwekezaji wa muda mrefu.

Faida zake si kupunguza gharama za matibabu pekee, bali pia kujenga familia yenye furaha, mshikamano na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha. Taifa lenye afya huanzia katika familia zenye afya. Na jukumu hilo halihitaji kusubiri sera mpya au bajeti mpya—linaanzia mezani nyumbani.