Na Mwandishi wetu– WAF, Dar es Salaam.
Wizara ya Afya imewataka wananchi kuendela kuchukua tahadhari na kufuatilia ushauri wa kitaalam ili kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali kama ilivyoelezwa katika taarifa kwa umma ya Mganga Mkuu wa Serikali hivi karibuni.
Hayo yamebainishwa leo Februari 27, 2026 Jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa alipofanya ziara ya kimakakati katika hospitali ya Rufaa Mkoa Amana kwa lengo la kukagua utolewaji wa huduma za afya pamoja na maendeleo ya uboreshaji wa miundombinu ya hospitali hiyo.
“Napenda kuwahakikishia wananchi na Watanzania wote Serikali yenu ipo makini na inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa maambukizi ya UVIKO-19 nchini na kimataifa, lakini pia tunasisitiza umuhimu wa kila mmoja kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia ushauri wa kitaalamu unaotolewa na wataalamu wa afya ili kulinda afya binafsi na ya jamii kwa ujumla,” amesema Mhe. Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa amesema kuwepo kwa bima ya afya kwa wote kuendana sanjari na upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na hospitali ili kukamilisha dhamira ya serikali katika kurahisisha huduma za afya kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mchengerwa ameambatana na Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe pamoja na menejimenti ya Wizara ya Afya, ambapo alikagua hali ya upatikanaji wa huduma, kusikiliza changamoto zinazowakabili watumishi na wagonjwa, na kueleza mikakati madhubuti ya serikali katika kuimarisha ubora na ufanisi wa huduma za afya kwa wananchi.