Hofu ya ‘kibamia’ inavyotesa wanaume wengi

Mwanza. Ukubwa wa uume ni mada ambayo wanaume wengi huijadili kwa sauti ya chini, kwa aibu au kwa mzaha, lakini ndani yake ikiwa imejaa hofu na mashaka.

Katika vijiwe vya kahawa, makundi ya marafiki na hata faraghani ndani ya ndoa, swali la wanaume wengi limekuwa lilelile; je, nina ukubwa wa kutosha? Nitamridhisha mke wangu?

Kadiri mitandao ya kijamii na maudhui ya ngono yanavyozidi kusambaa, taswira ya “ukubwa wa uume wa mwanaume” imekuwa ikiwekwa katika viwango visivyo vya kawaida.

Kibaya zaidi, wanaume wengi hujikuta wakijilinganisha na kile wanachokiona kwenye video ambazo haziwakilishi wastani wa uume wa wanaume duniani.

Matokeo yake, baadhi yao hupoteza kujiamini, hupata msongo wa mawazo na wakati mwingine huathirika hata katika ndoa zao.

Daktari wa Hospitali ya Wilaya Kaloleni jijini Arusha, Pendo Mushi, anasema uume mdogo, ambao Kiingereza hujulikana kwa jina la ‘micropenis’ ni hali ya nadra kiafya kwa wanaume.

Anaeleza kuwa hali hiyo husababishwa na matatizo ya homoni au ukuaji wa kimaumbile wakati wa ukuaji wa mtoto akiwa tumboni au katika kipindi cha kubalehe.

“Micropenis ni hali halisi ya kitabibu, lakini ni nadra sana. Wanaume wengi wanaodhani wana uume mdogo wako ndani ya viwango vya kawaida kabisa,” anasema Dk Mushi.

Kwa mujibu wa daktari huyo, vipimo maalum vya kitabibu hutumika kubaini hali hiyo. Kipimo kinachojulikana kama stretched penile length (SPL) hutumika kupima urefu wa uume kwa utaratibu wa kitaalamu.

Anasema kazi nyingi za kitafiti zinaonesha wastani wa uume uliosimama kwa mwanaume mzima ni kati ya sentimita 12 hadi 14.

“Hivyo, kuwa chini ya takribani sentimita saba hadi tisa kunaweza kuangukia kwenye vigezo vya kitabibu vya micropenis,” anasema.

Mwaka 2015, utafiti uliofanywa na watafiti wa Uingereza ukiongozwa na Dk David Veale wa King’s College London uliowahusisha wanaume zaidi ya 15,000, ulibaini wastani wa uume uliosimama ni sentimita 13.12.

Utafiti huo ulihitimisha kuwa wanaume wengi wanaohofia kuwa na uume mdogo wako ndani ya kiwango cha kawaida.

Kazi nyingine za kitafiti zilizofanyika Bulgaria na Ghana, pia zimeonesha kuwa micropenis ni hali nadra na hutambuliwa kwa vipimo vya kitabibu pekee.

Aidha, mapitio ya utafiti wa mwaka 2023 katika jarida la Journal of Clinical Research in Pediatric Endocrinology, yanaonesha kuwa hali hiyo mara nyingi husababishwa na upungufu wa homoni ya testosterone wakati wa ukuaji wa mtoto tumboni.

Dk Mushi anasema si kila mwanaume anayehisi ana uume mdogo ana tatizo Hilo.

Anataja sababu nyingine zinazoweza kufanya uume kuonekana mdogo kuwa ni pamoja na kitambi au mafuta mengi sehemu ya siri, hali inayoweza kuufanya uume uzame na kuonekana mfupi.

Mzunguko hafifu wa damu, unaoweza kuathiri uimara wa kusimama na upungufu wa homoni ya testosterone, unaopunguza nguvu ya uume kusimama.

“Hizi ni hali tofauti na micropenis. Wengi wanaojihisi kuwa na tatizo wana viwango vya kawaida kabisa,” anasema.

Dk Mushi anatoa tahadhari dhidi ya matumizi ya dawa au bidhaa zisizo na ushahidi wa kisayansi zinazodai kuongeza ukubwa wa uume.

“Baadhi ya dawa au vifaa vya kuvuta uume vinaweza kuharibu mishipa ya fahamu na kusababisha madhara ya kudumu,” anaonya.

Anasisitiza kuwa wanaume wenye wasiwasi wanapaswa kumuona daktari kwa ushauri wa kitaalamu, badala ya kuamini taarifa zisizo sahihi kutoka mitandaoni.

Kwa mujibu wa daktari huyo, uume mdogo ni hali halisi ya kitabibu, lakini ni hutokea kwa nadra. Wanaume wengi wanaoishi na hofu ya kuwa na uume mdogo hawana tatizo la kiafya, bali wanahitaji elimu sahihi ili kuondoa wasiwasi usio wa lazima.

Mkazi wa Mahina jijini Mwanza, Yahaya Israel, anasema hofu ya kuwa na uume mdogo imekuwa ikiwasumbua wanaume wengi kimya kimya.

“Wengi wanaishi na hofu wakidhani ni tatizo la kimaumbile. Wengine huanza kutafuta dawa za kuongeza uume bila kujua kuwa wako katika hali ya kawaida,” anasema.

Anadai hofu hiyo huongezeka kutokana na mijadala mitandaoni na kauli za kubeza kutoka kwa baadhi ya wanawake.

Kwa mtazamo wake, wataalamu wa afya wanapaswa kutoa elimu zaidi kwa umma ili kuondoa dhana potofu.

“Ni suala ambalo limeanza kuwa la kisaikolojia zaidi kuliko la kiafya,” anasema.

Kwa upande wake, Kalekwa Omari anasema kuridhika katika uhusiano hakutegemei ukubwa wa uume pekee.

“Kuridhika si ukubwa tu. Mawasiliano na uelewano vina nafasi kubwa zaidi,” anasema.

Hata hivyo, anakiri kuwa kejeli au maneno ya dhihaka yanaweza kuwaumiza wanaume na kuathiri afya yao ya kisaikolojia.