JMAT YAIMARISHA AMANI MWANZA, YAPANDA MITI ZAHANATI YA POLISI

::::::::::::::

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh. Alhaji Mussa Salum, amewasili mkoani Mwanza leo Februari 26, 2026, na kufanya ziara katika Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.

Akiwa ofisini hapo, amepokelewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, SACP Gideon Msuya, kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa, akiongozana na maafisa mbalimbali wa Jeshi la Polisi.

Ziara hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Siku ya Maridhiano, inayotarajiwa kuadhimishwa kitaifa mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu.

Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, SACP Gideon Msuya alimkaribisha Mwenyekiti wa JMAT pamoja na wajumbe wa jumuiya hiyo alioongozana nao, huku akipongeza mchango wao katika kuunga mkono kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi ya kulinda raia na mali zao, pamoja na kuimarisha amani kupitia utoaji wa elimu kwa jamii katika majukwaa mbalimbali, hususan kupitia dhana ya Polisi Jamii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JMAT, Sheikh. Alhaji Mussa Salum, amesema kuwa Siku ya Maridhiano ni wazo lililoasisiwa na mlezi wa taasisi hiyo, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, likiwa na lengo la kuwakutanisha wadau wa amani nchini ili kujenga mshikamano na kudumisha amani ya taifa.

Ameongeza kuwa kupitia maadhimisho hayo, wadau wa amani kutoka mikoa yote nchini hukutana na kuungana katika kuimarisha ushirikiano, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Vilevile, Sheikh. Alhaji Salum amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuendelea kuwa imara katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kudumishwa.

“Mimi naamini kuwa Jeshi la Polisi ni mdau mkubwa wa amani chini ya uongozi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillus Wambura, ambaye ni kiongozi anayethamini na kupenda amani,” alisema.

Aidha, amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi limeendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa Jumuiya ya Maridhiano na Amani wakati wote, hususan katika nyanja ya ushirikishwaji wa jamii, hali ambayo imeongeza urafiki na ushirikiano kati ya wananchi na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani nchini.

Ziara hiyo pia iliambatana na zoezi la upandaji wa miti ya kivuli na matunda katika eneo la Zahanati ya Polisi Mabatini, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa mazingira na kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii.