Kardinali Pengo alivyoagwa Dar | Mwananchi

Dar es Salaam. Nyuso zenye huzuni zimetamalaki katika Kanisa Kuu Katoliki la Mtakatifu Yosefu jijini Dar es Salaam, ambapo mamia ya waombolezaji wamejitokeza katika misa takatifu ya kumwombea na kumuaga hayati Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Kardinali Pengo (82) alifariki dunia Februari 19, 2026 akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), mazishi yake yanatarajiwa kufanyika kesho Jumamosi Februari 28, 2026 ndani ya kanisa la Kituo cha Hija Pugu, ambako alichagua.

Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba ni miongoni viongozi na waombolezaji waliojitokeza katika misa hiyo iliyoongozwa na mwashamu Wolfgang Pisa, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na askofu wa Jimbo la Lindi.



Wananchi wakiaga mwili wa Kardinali Pengo kanisani

Wengine waliohudhuria ni mawaziri, watendaji wa Serikali, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa vyama vya siasa.

Mbali na maasko wa Kanisa Katoliki Tanzania na viongozi wa madhehebu mengine nchini, pia walikuwepo maaskofu kutoka mashirika ya kikanda ya kanisa hilo kutoka kote Afrika.

Pia, viongozi wa Kanisa Katoliki wa nchi jirani wamehudhuria misa hiyo akiwemo Askofu Fridolin Ambongo Besungu ambaye ni Kadinali Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Askofu Antoine Kambanda ambaye ni Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Kigali nchini Rwanda.

Wengine ni Charles Kasonde ambaye ni Askofu wa Jimbo la Solwezi (Zambia), Martin Anwel Mtumbuka ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Karonga nchini Malawi.

Pia, Charles Mahuza Yava ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Moroni katika Visiwa vya Comoro, yaani Roman Catholic Diocese of Moroni.

Walikuwepo makatibu wa mabaraza la maaskofu katika maeneo mbalimbali ambao ni Padri Raphael Sindeni, Padri Anthony Makunde mabaye ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki na Kati na Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Angelo Accattino.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ni miongoni mwa viongozi mbalimbali wanaoshiriki misa ya kumwombea marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo katika Kanisa Kuu la Mt. Joseph jijini Dar es Salaam.



Pia, walikuwepo viongozi wa vyama vya siasa, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche, Katibu John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa na Luhaga Mpina wa ACT-Wazalendo.

Katika mahubiri yake kwenye misa hiyo, Askofu Wolfgang Pisa, Rais wa TEC alimzungumzia Kardinali Pengo akionyesha kwa namna mbalimbali alivyokuwa zawadi kutoka kwa Mungu.

Alisema alipewa upadirisho akiwa na umri wa miaka 27 tu huko Sumbawanga. Mwaka 1977 alianza kufundisha Seminari Kuu Kipalapala mkoani Tabora ambako alikaa mwaka mmoja.

“Wengine wanaendaga pale inservice mpaka miaka tano bado wanafanyiwa ‘inservice’, mpaka akae sawa ‘inservice’ ndio aende shule. Mwaka mmoja yeye amekaa baadaye anapelekwa Segerea (Dar es Salaam) kuanzisha seminari kuu, hakuhitaji ‘mentorship na alifanya hiyo kazi kwa miaka mitano.

Mwaka 1983 akiwa na miaka 39 tu aliteuliwa kuwa Askofu wa Nachingwea mkoani Lindi.

“Cha ajabu anateuliwa askofu ndio anafika tayari ana mawazo ya kulihamisha jimbo kutoka Nachingwea kulipeleka Tunduru-Masasi. Ni akili ya wachache ya uthubutu, kwanza kule Wakristo ni wachache, Nachingwea anakoacha Wakristo ni wengi.

“Kiti chake kipo mpaka leo pale Nachingwea ambacho amekikalia, mara moja moja mimi nakikalia. Sasa kipo kwenye himaya yangu, kwa hiyo sihitaji ruhusa ya mtu yeyote.”

Sasa mwaka 1984, miaka mitatu tena, baada ya kukaa pale Masasi. Akaja Dar es Salaam kama askofu mwandamizi na miaka minane baadaye, yaani mwaka 1998 akawa kardinali.

“Alijinasua na mambo ya Ulimwengu alitoa mali zake zote, vitu vyake vyote, hakuwa na mali ya binafsi, hakuwa hata na akaunti binafsi benki, hakuwa nayo. Watawa wengine hapo utawatoa macho ukiwaambia wasiwe na akaunti. Hakuwa nayo, yeye hakuwa nayo, Mwadhama, Askofu Mkuu hakuwa na akaunti benki.

“Simu wengine wanasema alikuwa nayo, mimi sikuwahi kumuona na sikuwahi kumpigia, mimi nilimpata kupitia wasaidizi. Alikuwa anashangaa mapadri wanaingia ofisini pale wanamwaga simu tatu mezani, wakati Mzee hana hata simu moja na Mzee anawaonea huruma hivi wanazibebaje, wanazitumiaje.”

Mapema akisoma wasifu wa marehemu, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Henry Mchamungu amesema kabla ya umauti, kwa muda mrefu askofu Pengo alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya mgongo na moyo kwa muda mrefu.

Waumini wakitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo leo Ijumaa Februari 27, 2026 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Josefu Jimbo Kuu la Dar es Salaam.



“Alitibiwa hapa nchini na nje ya nchi ikiwemo Ujerumani, India na Marekani. Matatizo ya kiafya ya mara ya mwisho yaliongezeka na kugundulika zaidi kuanzia Novemba 2025. Alianza matibabu hapa nchini na kisha kwenda nchini India 27 Desemba 2025.
“Alifariki kwa maradhi ya moyo muda mfupi baada ya kurudi kutoka India alikokuwa akipata matibabu. Tunatoa shukrani za dhati kwa wote waliokuwa naye katika kipindi cha mahangaiko yake ya maradhi wakiwemo madaktari na wauguzi waliomhudumia,” amesema askofu Mchamungu na kuongeza

“Pia tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kushughulikia upatikanaji wa Air Ambulance, iliyomsafirisha kutoka India hadi Dar es Salaam,” amesema.

Askofu Mchamungu amesema kanisa Katoliki nchini Tanzania litamkumbuka Kardinali Pengo kwa mambo kadhaa ikiwemo moyo wa ibada na sala kwa ekaristi takatifu, hasa alipenda kushinda na Yesu mara nyingi na mapenzi yake kwa mama Bikira Maria kwani alipenda mno kusali rozali takatifu.


Kwa mujibu wa Askofu Mchamungu, Kardinali Pengo aliishi kile alichokihubiri. Unyenyekevu wake haukuwa wa maneno, bali wa matendo. Alijitoa kwa Kanisa kwa moyo wote na hakuwa mtu wa kujilimbikizia mali.

“Aliishi maisha ya kifukara. Hakupenda kabisa kujikusanyia mali. Baada ya kustaafu, zawadi alizopewa alizitoa mara moja kwa miradi ya Kanisa. Huo ulikuwa moyo wake wa sadaka,”

“Mbali na unyenyekevu, marehemu alijulikana kwa nidhamu binafsi ya hali ya juu hasa katika sala, kuheshimu muda na kufanya kazi kwa bidii. Alikuwa mchungaji aliyethamini upadri wake na kuuheshimu kwa vitendo, akionyesha mfano wa maisha ya utumishi.

Waombolezaji wakiwa kwenyeibada ya kuaga mwili wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo leo Ijumaa Februari 27, 2026 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Josefu Jimbo Kuu la Dar es Salaam.



Askofu Mchamungu amesema Kardinali Pengo alijiepusha na upendeleo wa aina yoyote na aliwahudumia watu wote bila kujali asili, hadhi au tofauti zao. Katika kipindi chote cha utumishi wake, alisimamia ukweli, haki, amani na maadili bila kuyumbishwa.

“Alikuwa na msimamo kwa mambo ya msingi. Hakusita kusimama upande wa ukweli hata pale ilipokuwa vigumu,” amesema.

Katika kuimarisha Kanisa, Kardinali Pengo alibuni na kusimamia mikakati mbalimbali ya kuliwezesha jimbo kujitegemea. Alianzisha parokia nyingi, taasisi na vyama vya kitume vilivyochangia kukuza imani na huduma kwa jamii.

Moja ya ubunifu wake uliotajwa ni utaratibu wa parokia kuchangia kusomesha maflateri kwa njia ya sadaka ya misa siku ya Kipaimara, hatua iliyosaidia kuimarisha malezi ya watumishi wa kanisa.

Luhaga Mpina akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo leo Ijumaa Februari 27, 2026 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Josefu Jimbo Kuu la Dar es Salaam.



Aidha, alianzisha mfumo wa kusaidia baadhi ya taasisi za jimbo kupitia vyama vya kitume, akiamini kuwa ushiriki wa waamini katika kuchangia maendeleo ya kanisa ni msingi wa ukuaji wake.

Upendo wake kwa watoto nao ulikuwa wa pekee akielezwa kusimama imara kuunga mkono utume wa Mtoto Mtakatifu, akiamini kuwa malezi ya kiroho kwa watoto ni uwekezaji wa kanisa la kesho.

Tangu alfajiri maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki na watu wa madhehebu mbalimbali walijitokeza kanisani hapo kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo wa kiroho aliyelitumikia taifa kwa miongo kadhaa.

Viongozi wa Katoliki wakitoa heshima za mwisho kwa mwili wa Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo leo Ijumaa Februari 27, 2026 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Josefu Jimbo Kuu la Dar es Salaam.



Foleni ndefu zilionekana kuankatikaia viunga vya kanisa hilo, huku baadhi wakishika rozari mikononi, wengine wakiwa na nyuso zilizojaa simanzi.

Mwili wa Kardinali Pengo uliwasili kanisani ukitokea katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo ulikohifadhiwa ambapo msafara wake ulipita barabara za Ali Hassan Mwinyi na Ohio kabla ya kufika kanisani hapo.

“Alikuwa sauti ya wanyonge na nguzo ya maadili katika jamii,” alisema mmoja wa mapadri wakati wa ibada hiyo, akisisitiza mchango wa Kardinali Pengo katika kuimarisha maadili na mshikamano wa kitaifa.

Baadhi ya waumini waliozungumza na Mwananchi walisema wameguswa na pengo kubwa lililoachwa na kifo cha kiongozi huyo wa kiroho.

“Tumempoteza baba, mshauri na mlezi. Alikuwa mtu wa watu, hakuchoka kusimamia ukweli,” amesema mmoja wa waumini aliyefika kutoka Mkoa wa Pwani.