Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa siku 30 kwa upande wa Jamhuri katika kesi ya wizi wa fedha inayomkabili, raia wa Bulgaria, Eduardl Mladenov (32) na Mtanzania Juma Ndambile(58), kuanza vikao vya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo.
Hatua hiyo inatokana na washtakiwa hao, wanaodaiwa kujihusisha na miamala ya fedha kwa kutoa fedha katika Benki ya CRDB na NBC, kumwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), wakiomba kufanya majadiliano ya kukiri makosa yao na kuimaliza kesi hiyo (Plea Bargaining).
Mladeno na Ndambile, wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa na kujihusisha na miamala ya kutoa fedha yenye thamani ya Sh364 milioni kutoka Benki ya CRDB na NBC.
Pia, wanadaiwa kukutwa na mali ya wizi ambayo ni mashine ya kuchanjia kadi kwa ajili ya kufanya malipo ya fedha kwa njia ya kielektroni (POS) yenye thamani ya Sh500,000 mali ya Selcom Tanzania.
Uamuzi wa kutoa siku hizo 30 kwa Jamhuri, umetolewa leo Februari 27, 2026 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Hakimu Mhini aliwaeleza washtakiwa pamoja na upande wa mashtaka kuwa, Mahakama hiyo inatoa nafasi kwa siku 30 kwa ajili ya pande zote kuanza majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo.
Awali, Wakili wa Serikali, Theresia Mtawa alidai kuwa kesi imeitwa kwa kutajwa, lakini washtakiwa wameandika barua ya kukiri mashtaka yao, hivyo wanaomba mwongozo wa Mahakama.
Kwa upande wake wakili wa washtakiwa, Steven Lucoo alidai Januari 19, 2026 wateja wake wote wawili walimuandika barua ya kufanya majadiliano na DPP ya kuimaliza kesi hiyo, lakini hawajapewa majibu.
Akijibu hoja hiyo, Mtawa alidai rekodi zinaonesha kuwa, upande wa utetezi waliambiwa wasubiri kwani barua hiyo ilikuwa inafanyiwa kazi.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, hakimu Mhini alitoa siku 30 kwa ajili ya pande zote mbili kuanza vikao vya majadiliano ya kuimaliza kesi na kisha watatoa taarifa kwa Mahakamani.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 5, 2026 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana.
Kwa mara ya kwanza, walifikishwa mahakamani hapo Desemba 12, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 29134 ya mwaka 2025 yenye mashtaka sita.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka la kuongoza genge la kupangwa.
Inadaiwa kati Januari mosi, 2025 hadi Novemba 11, 2025 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, washtakiwa waliongoza genge la uhalifu wa kupangwa.
Shtaka la pili ni kupatikana na mali ya wizi, linalomkabili Ndambile pekee yake, anadaiwa Oktoba 24, 2025 eneo la Mbweni, Wilaya ya Kinondoni mshtakiwa alikutwa na mashine ya kuchanja kadi kwa ajili ya kufanya miamala ya fedha (POS) yenye thamani ya Sh500,000 mali ya Selcom Tanzania.
Pia, wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu shtaka linayowakabili washtakiwa wote, kati ya Julai Mosi 2024 hadi Novemba 11, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walidanganya na kujipatia Sh116 milioni kutoka NBC.
Shtaka la nne ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, shtaka linalowakabili washtakiwa wote walijipatia Sh248 milioni kutoka CRDB PLC.
Ilidaiwa kuwa shtaka la tano na la sita ni utakatishaji fedha na linawakabili washtakiwa wote.
Alidai washtakiwa kwa pamoja walijihusisha na miamala ya moja kwa moja ya Sh116 milioni kutoka NBC na Sh248 milioni kutoka CRDB PLC, wakati wakijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.