Mgogoro wa wakulima, wafugaji unavyopasua kichwa Serikali

Dar es Salaam. Uso wake ukiwa umeonyesha kukata tamaa baada ya kusubiri nafasi ya kueleza kero yake mbele ya Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, hatimaye Ngodi Jengo, mkazi wa Kijiji cha Lesweti anapata fursa ya kuzungumza.

Jengo analalamikia kuondolewa na uongozi wa kijiji kwenye shamba analodai kulirithi kutoka kwa baba yake, kwa madai kuwa eneo hilo linahitajika kwa ajili ya malisho ya wanyama.

“Shamba hili lilikuwa ekari 60 na baba yangu alianza kulimiliki mwaka 1986, yeye alifariki na tuliendelea kulihudumia hadi mwaka 2015 tukanyang’anywa na kijiji, nilifuatilia sikupata chochote hadi sasa.”

“Haikutosha, nikakodi shamba lingine, ilinigharimu Sh4.5 milioni, mazao yalipokaribia kuvunwa wafugaji wakaingiza ng’ombe. Sikupata hata kilo moja ya mahindi,” anasimulia Jengo.

Kwa upande mwingine, mkazi wa Kijiji cha Lotepesi kilichopo Kata ya Sunya, Mussa Loshilo yeye ana simulizi tofauti.

Amesema wafugaji wamejikuta wakionekana wahalifu kila panapotokea tatizo la ardhi, amedai baada ya mifugo kuingia kwenye mashamba ya wakulima, mwenyekiti wao alikamatwa, ng’ombe wakaswagwa umbali wa kilomita 39 na baadhi wakapotea.

“Tangu hapo tumekuwa tukiishi kama digidigi, wafugaji wamekuwa wakikamatwa na kudaiwa fedha ili waachiwe.”

Simulizi hizi mbili zinaakisi namna migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji inavyozidi kupasua kichwa wilayani Kiteto mkoani Manyara, huku kila upande ukijiona mwathirika.

Migogoro hii inaibua maswali mengi kuhusu upangaji wa matumizi ya ardhi, uwajibikaji wa viongozi wa ngazi za chini na nafasi ya vyombo vya dola katika kusimamia haki bila upendeleo.

Akitoa ufafanuzi wa kilichotokea kwenye kilio kilichowasilishwa na Loshilo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Remidius Mwema anasema tukio la kukamatwa kwa mwenyekiti huyo lilitokea Januari 1, 2026 baada ya kubainika kuwa kulikuwa na uchochezi wa makusudi.

Amesema Januari 17 na 18 kulifanyika mikutano ya kuhamasisha wafugaji kupeleka mifugo kwenye mashamba ya wakulima, jambo lililochochea vurugu.

“Siku ya tukio tulipita katika eneo hilo nikiwa na kamati ya ulinzi na usalama, nikakuta nyumba tano zimechomwa moto. Mimi mkuu wa wilaya nilishuhudia kwa macho yangu tukio hilo linaongozwa na mwenyekiti wa kijiji na wa kitongoji, nikaelekeza wakamatwe mara moja pamoja na vijana 16,” amesema.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa wilaya, baadhi ya watuhumiwa walikutwa na silaha za jadi wakishambulia wakulima.

Pia, alidai kulikuwa na viashiria vya rushwa, akisema baadhi yao walijaribu kumshawishi kwa hongo.

“Niliwaweka ndani na kuwaambia mimi sihongeki. Pia, nilimwelekeza kamanda wa Takukuru afuatilie tuhuma za rushwa dhidi ya baadhi ya viongozi wanaopindisha haki,” ameeleza.

Wakati hali ikiwa hivyo wilayani Kiteto, msimamo wa Serikali umekuwa kusisitiza matumizi bora ya ardhi na kutovumilia uvunjaji wa sheria kwa makusudi.

Akizungumza Februari 27,2026 akiwa wilayani Kiteto, Waziri Mkuu Dk Nchemba amesema Serikali haitaruhusu vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani, vikiwamo vya kuchochea uhasama kati ya wakulima na wafugaji.

Amesema Serikali haitaruhusu uvunjaji wa sheria kwa makusudi, akionya kuwa kushindwa kusimamia sheria ni sawa na kuruhusu wananchi kuchukua sheria mkononi hali ambayo inaweza kulifikisha Taifa pabaya.

“Mimi sipingi mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa sababu ndiyo mwelekeo wa Serikali, lazima twende kwenye matumizi bora ya ardhi. Lakini kitu kimoja tunachopaswa kukifahamu wote, nchi hii hakuna namna tunaweza kutenga shughuli za kilimo na ufugaji,” alisema.

Amesema hakuna faida ya wakulima na wafugaji kufikia hatua ya kuonana maadui kwa sababu hata wakipigana ardhi haitaongezeka.

“Hata mchukiane ardhi haiongezeki, mtauana bure. Kinachotakiwa ni kuyamaliza haya mambo kindugu ili maisha yaendelee,” amesisitiza

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kumekuwa na mabadiliko ya kitabia katika jamii ambapo baadhi ya watu wameanza kufanya ubabe na unyama kuwa kama sifa, hali inayochochea migogoro.

Alikumbusha kuwa zamani, mfugaji alipoingiza mifugo kwenye shamba la mkulima kwa bahati mbaya, alikwenda kuomba radhi na suala hilo kumalizwa kindugu, lakini sasa kumekuwepo na kasumba ya kuingiza mifugo kwa makusudi na kufanya ubabe.

“Hili halikubaliki na Serikali haitaruhusu twende na uelekeo huo, kwa sababu kwenye mambo yanayohatarisha amani ya nchi hatuna mzaha kabisa,” amesema.

Amewataka wafugaji kutumia vikao vyao kujikosoa na kuwaonya wale wanaovunja sheria kwa makusudi kwa kuwa kuanza kuvunja sheria rejareja kunaweza kusababisha wananchi kuchukua sheria mkononi, jambo ambalo Serikali haitaliruhusu.

“Viongozi wala msimung’unye maneno kwenye hili, kuweni wakali kwa hawa wanaovunja sheria. Mambo yanayoweza kuvunja utaifa na undugu wetu tusimung’unye maneno,” ameeleza.

Aidha, amewataka wafugaji wanaohitaji malisho kwa ajili ya mifugo yao kukodi au kumiliki mashamba halali kwa ajili ya kulisha mifugo badala ya kupeleka ng’ombe katika mashamba ya watu wengine.