STRAIKA mpya wa Yanga, Laurindo Dilson Aurelio ‘Depu’ ameendelea kudhihirisha sio mtu wa mchezo mchezo kutokana na kasi yake ya ufungaji mabao Ligi Kuu Bara, akifunika mastaa kadhaa waliowahi kusajiliwa dirisha dogo na kutisha kwa kutupia mipira kambani.
Kwa msimu uliopita, nyota aliyetisha kwa walioingia dirisha dogo alikuwa ni Jonathan Sowah aliyekuwa Singida Black Stars aliyeipiku rekodi ya Jean Baleke aliyeichezea Simba iliyomsajili dirisha dogo la msimu wa 2023-2024 kwa kufunga mabao katika mechi mfululizo.
Sowah ambaye kwa sasa yupo Simba, alifunga mabao matatu katika mechi nne mfululizo na kuja kumalizia nusu msimu akitumika katika mechi 14 akimaliza na mabao 13, akimpiku Baleke aliyetumia nusu msimu kufunga mabao manane.
Hata hivyo, kile anachokifanya Depu kwa sasa ni wazi, straika huyo kama ataendelea na moto huo ataandika rekodi mpya kwa wachezaji walioingia dirisha dogo kwa misimu mitatu iliyopita, kwani hadi sasa tayari ana mabao matano na asisti moja kupitia mechi nne tu akiipiku ile ya Sowah.
Depu ambaye ni raia wa Angola aliyetua Yanga mwezi uliopita akitokea Radomiak Radom ya Poland, juzi alifunga bao lake la tano msimu huu katika Ligi Kuu wakati Yanga ikiwazamisha maafande wa JKT Tanzania kwa mabao 5-0 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge.
Straika huyo anayesifika kwa kufunga mabao ya vichwa kama alivyofanya juzi dhidi ya JKT, alianza kutupia katika mechi ya kwanza akiwa na uzi wa timu hiyo ilipovaana na Mashujaa Januari 19 akifunga bao la sita katika ushindi wa 6-0. Depu alifunga bao hilo katika dakika ya 89, pia aliasisti moja ya mabao mengine matano ya Yanga.
Depu aliendelea kudhihirisha kuwa hakubahatisha katika mechi ya kwanza kwa kufunga tena mabao mawili Januari 27, wakati Yanga ikiinyuka Dodoma Jiji 3-1, alianza kwa kuchomoa bao la utangulizi la wageni lililofungwa na Edgar William katika dakika ya 41 kwa kuweka mizani sawa sekunde chache kabla ya mapumziko kwa penalti kisha kuongeza la pili (dk61). Dube alifunga bao la tatu la Yanga katika dakika ya 67.
Mechi ya tatu kwa Depu akiwa na Yanga ilikuwa ni dhidi ya Namungo ikichezwa ugenini Feb 22 akifunga kwa pigo la penalti ya dakika ya 26 ya pambano hilo lililokuwa kali kabla ya juzi kukamilisha idadi ya mabao matano kupitia mechi nne tu alipoizamisha JKT Tanzania dakika ya 60.
Kwa upande wa Sowah licha ya kuanza na bao katika mechi ya kwanza akiwa na uzi wa timu hiyo, lakini alishindwa kufunga mechi iliyofuata japo aliendelea kufunga katika mechi mbili mfululizo zilizofuata kukamilisha nne akiwa na mabao matatu.
Sowah alianza katika pambano Feb 07, 2025 lililoisha kwa sare ya 2-2 dhidi ya Kagera Sugar akifunga bao la kwanza la Singida katika dakika ya 7, kisha Kagera kuchomoa kupitia kwa Saleh Kambenga (dk21) na Halifa Nolo kuongeza la pili la wageni (dk59). Marouf Tchakei aliiokoa Singida isife kwa kusawazisha bao kwa penalti katika dakika ya 62.
Hata hivyo, mechi iliyofuata iliyopigwa Feb 10, 2025 kwenye Uwanja wa KMC, Sowah alishindwa kuiokoa Singida isife mbele ya KMC iliyoibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Oscar Paul (dk34 na 40), lakini akazinduka mechi ya tatu dhidi ya JKT Tanzania iliyopigwa Feb 13, 2025 alipofunga bao pekee na la ushindi katika dakika ya 51.
Mechi ya nne kwa Sowah ilikuwa ni dhidi ya Yanga, ambapo Singida ililala 2-1, huku yeye akifunga bao la kufutia machozi katika dakika za mwisho za majeruhi, baada ya wenyeji Yanga kutangulia kwa mabao ya Clement Mzize dk 14 na Prince Dube dk ya 44 katika mechi hiyo iliyopigwa Feb 17, 2025.
Licha ya kuifunika rekodi ya Sowah, Depu pia ameisaidia Yanga kupata pointi nyingi kulinganisha na nyota huyo Mghana aliyepo Simba kwa sasa.
Katika mechi zote nne ambazo Depu alifunga, Yanga iliibuka na ushindi na kuvuna jumla ya pointi 12, tofauti na Sowah mabao yake yalivuna pointi nne tu, akiipa ushindi mmoja na sare moja, huku mechi mbili nyingine Singida ikipoteza mbele ya wapinzani na zote kwenye Uwanja wa KMC.
Kwa sasa Depu ana kibarua kupitia pambano la watani wa jadi, Kariakoo Derby itakayopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar ili kuendeleza rekodi ya kutupia mechi mfululizo, iwapo atapangwa na kucheza pambano hilo la kwanza la Simba na Yanga katika ligi.