Dar/Dodoma. Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM kilichopangwa kufanyika Jumamosi, Februari 28, 2026, kimeahirishwa.
Taarifa za ndani ya chama hicho ambazo si rasmi zimebainisha kuwa kikao hicho kimesogezwa mbele hadi Machi 10, 2026, kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi.
Hata hivyo, taarifa zingine za zimedai kuwa awali mkutano huo ambao unaalezwa moja ya ajenda ni kufanya maboresho kwenye sekretarieti, ulipangwa kufanyika kwa njia ya mtandao, jambo ambalo baadhi ya wajumbe hawajaridhika nalo.
Hivyo, taarifa hizo zimedai kuwa baadhi ya wajumbe wamependekeza kikao hicho kifanyike kwa wajumbe kukutana ana kwa ana kwa kuwa wanakwenda kufanya maamuzi makubwa.
Uamuzi wa kufanya kikao cha NEC kwa njia ya mtandao ulilenga kupunguza gharama na kutekeleza maamuzi ya chama yanayoruhusu vikao kufanyika kwa njia ya mtandao kama sehemu ya mageuzi ya kiteknolojia katika utendaji wake wa chama.
Julai 26, 2025 CCM ilifanya Mkutano Mkuu Maalumu kwa njia ya mtandao kupitisha marekebisho madogo ya katiba ya chama.
Licha ya kwamba ajenda hazijaelezwa rasmi, mapema wiki hii gazeti hili lilidokezwa kwamba moja ya masuala yatakajadiliwa ni kufanya marekebisho kwenye safu za uongozi wa chama, ikiwemo sekretarieti ili kukidhi mahitaji ya sasa na maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama.
Sekretarieti ya CCM inaundwa Katibu Mkuu wa Chama ambaye ni mwenyekiti huku wajumbe wake ni Naibu katibu wakuu Zanzibar na Bara, Makatibu wakuu wa jumuiya, Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo na Katibu wa NEC Mambo ya Nje na Ushirikiano.
Sekretarieti ya CCM ngazi ya Taifa huteuliwa na Kamati Kuu na kuthibitishwa na NEC.
Katibu wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa Kenan Kihongosi hakupatikana kuzungumzia jambo hilo huku mmoja wa wasaidizi wake akieleza kuwa kiongozi huyo yupo kwenye majukumu ya chama.
Mmoja wa wajumbe wa NEC, ambaye hakupenda jina lake kutajwa, amesema alikuwa na taarifa za kikao cha NEC, lakini ghafla alipokea ujumbe wa kuahirishwa kwake na taarifa ikieleza kuwa watajulishwa tarehe nyingine baadaye.
Amesema kuwa taarifa ya kikao haikuwa imeweka wazi ajenda, kwa sababu sekretarieti haikuwa imechakata ajenda hizo. Ndiyo maana, hawakupewa taarifa kamili na hivyo hakuwa na tetesi zozote kuhusu ajenda hizo.
Chanzo kingine ndani ya NEC kimesema mkutano uliokuwa ufanyika Jumamosi Februari 28, umeahirishwa kwa sababu ya maziko ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na kuwa hutaishwa tena kdani ya muda usiozidi wiki moja.
Hata hivyo, mjumbe mwingine wa NEC, ambaye naye hakutaka kutajwa jina lake, naye amesema taarifa rasmi za kikao hicho hazikuwa zimetolewa, na hivyo ajenda zake pia hazikuwa wazi kwa umma.
Mjumbe huyo amebainisha kwamba, katika uzoefu wake wa miaka tisa ya ujumbe wa NEC, hajawahi kushuhudia ajenda za kikao hicho kuwa wazi kama watu wanavyotarajia.
“Mimi ni mjumbe huu mwaka wa tisa, hicho unachosema kuhusu ajenda zipi huwa haipo hivyo, kile kikao nyeti hakiwezi kuweka mambo hadharani hivyo, ingawa huwa tunakuwa na tetesi, lakini safari hii hatuna kabisa,” amesema.
Amesema vikao vya chama vinaweza kuwa wazi kama kuna mambo ya kawaida lakini usiri ndiyo msingi mkuu wa CCM na ndiyo nguzo inayowaongoza wakati wote.
Akizungumzia uwezekano wa mabadiliko ya Sekretarieti ya CCM Taifa, mjumbe huyo amesema hilo siyo tatizo na ikitokea haiwezi kuwa jambo jipya, hata kama muda wa uchaguzi umekaribia.
“Ukisema uchaguzi umekaribia kwa nini tubadili sekretarieti utakuwa unakosea, wale si wajumbe wa kuchaguliwa ambao lazima wamalize miaka mitano, anaweza kuteuliwa na akakaa miezi miwili akaondolewa kama hakidhi matakwa,” amesema.
Mjumbe wa Kamati ya siasa wa Wilaya Mstaafu, Joel Ilumbo amesema katika mwelekeo wa sasa na baada ya Uchaguzi Mkuu kupita, sekretarieti inaweza kubadilishwa bila kuleta madhara.
Ilumbo amesema kwa sasa inatakiwa nguvu mpya ya kuandaa chama kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2030 ambapo CCM itakuwa na mgombea mpya.
“Chama chetu kinajua mikakati yake na maono ya mbele, Mwenyekiti wetu anakwenda kufanya mazungumzo na upinzani ili kuleta Taifa pamoja, jambo hilo linaweza kuwapa nguvu wapinzani, sasa tunapaswa kuwa na damu mpya za kukimbia ili jamaa wasituzidi,” amesema Ilumbo.