Suala la gharama za usafiri wa anga nchini limechukua sura mpya baada ya Serikali kukiri kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu bei kubwa za tiketi ambazo zimekuwa zikionekana kama mzigo kwa Mtanzania wa kawaida.
Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amebainisha kuwa, licha ya uwekezaji mkubwa unaofanywa katika ujenzi wa viwanja vya ndege nchini, nia kuu ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona miundombinu hiyo inamnufaisha mwananchi wa hali ya chini.
Amesema Serikali inatambua kuwa usafiri wa anga haupaswi kuwa anasa ya watu wachache wenye uwezo mkubwa wa kifedha pekee, bali uwe ni huduma inayofikika na kila mmoja ili kuchochea biashara na maendeleo.
Katika hatua ya kwanza ya utatuzi, Msemaji wa Serikali amefafanua kuwa wataalamu kutoka wizara husika tayari wameanza kufanyia kazi uchambuzi wa kina wa tozo, kodi, na ada mbalimbali ambazo zinachangia kupanda kwa bei za tiketi.
Amesema Zoezi hili linalenga kuona ni maeneo gani yanaweza kupunguzwa bila kuathiri uendeshaji wa viwanja vya ndege na mashirika. Huu ni mchakato wa kimkakati unaolenga kuleta uwiano kati ya gharama za uendeshaji na uwezo wa kifedha wa abiria wa ndani.
Amesema akijibu swali katika mkutano wake na waandishi wa habari Februari 26, Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere kwamba wananchi wasubiri nini kitafanyika wakati wa bajeti Juni mwaka huu, ambapo bajeti mpya ya Serikali inatarajiwa kusomwa bungeni.
Msemaji amewahakikishia Watanzania kuwa wakati wa mchakato huo wa bajeti, kila kitu kitakuwa wazi na maamuzi yatakayochukuliwa yatalenga kutoa unafuu wa moja kwa moja kwa wasafiri. Hii itakuwa ni habari njema kwa wale wanaotegemea usafiri huo kwa shughuli za dharura na biashara za haraka.
Uwekezaji ambao Serikali imefanya, ikiwemo ununuzi wa ndege mpya 16 za ATCL na ukarabati wa viwanja vya mikoani kama Tabora, Kigoma, na Shinyanga, unalenga kutanua wigo wa huduma hizi. Hata hivyo, uwekezaji huo hautakuwa na tija kamili kama ndege zitakuwa zinaruka bila abiria wa kutosha kutokana na gharama kubwa za nauli.
Aidha, serikali imeeleza kuwa ongezeko la mashirika ya ndege ya kimataifa yaliyovutiwa kuanza safari nchini, kama vile Air France na Saudi Arabia, ni ishara ya kukua kwa soko. Ushindani huu unapaswa kwenda sambamba na mazingira wezesha ya kodi ndani ya nchi ili kutoa fursa kwa mashirika ya ndani pia kukua na kutoa huduma kwa bei nafuu. Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa sekta ya uchukuzi inachangia zaidi katika pato la taifa kwa kuwafanya watu wengi zaidi wasafiri kwa anga.
Wananchi sasa wanasubiri kwa hamu mwezi Juni ili kuona ni kwa kiasi gani nauli hizo zitashuka. Matarajio ni kwamba kupungua kwa tozo kutaongeza mzunguko wa fedha na kuchochea utalii wa ndani, ambao tayari umeshuhudia ongezeko la kufikia watalii milioni 3.6 mwaka 2025. Hii itakuwa ni hatua kubwa katika kuleta mapinduzi ya usafirishaji nchini Tanzania.