Dodoma. Serikali imefungua milango kwa Sekta binafsi kutoa huduma ya maji ili kuleta ushindani na mamlaka za maji nchini.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Februari 27, 2026 kwamba huu si wakati wa kuogopa ushindani wa sekta binafsi, ilimradi Wizara ihakikishe ubora wa huduma itakayotolewa na watu hao.
Waziri Aweso amesema hayo wakati akifungua, Mkutano Mkuu wa kwanza wa mwaka wa Wakala wa Maji na Usafi wa mazingira Vijijini (Ruwasa) na vyombo vya Utoaji huduma ya maji ngazi ya Jamii (CBWSO’s), ambao umehudhuriwa na wajumbe 931.
“Tunahitaji kuwahudumia Watanzania, tusiogope ushindani, mbona wenzetu Wizara ya Elimu wameruhusu ushindani na Wizara ya Afya pia mbali na kujenga mahospitali lakini wapo kwenye ushindani, sisi tusimamie ubora mambo mengine yaendelee,” amesema Aweso.
Waziri amewaagiza watumishi kufanya kazi zenye matokeo huku akisisitiza kuwa ni aibu wananchi kukosa maji kwa kisingizio cha kuisha kwa umeme wakati wahusika walikuwa na taarifa tangu mwanzo kwamba kuna kuisha kwa luku.
Kwa mujibu wa Aweso, upatikanaji wa maji maeneo ya vijijini ulifikia wastani wa asilimia 85.2 mwishoni mwa Desemba 2025 kutoka asilimia 79.9 mwaka 2024, akisema lengo limetimia.
Ameeleza kuwa hivi sasa viongozi wa Wizara wanapata usingizi hata inapokuwa katika kipindi cha bajeti, wakati zamani walikesha wakihofia hoja za wabunge.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amekemea tabia ya watumishi wa maji kutunisha misuli kwa wananchi wakati wanajua ni haki yao kuhudumiwa.
“Acheni ubabe kwa wateja na muache ubambikiaji wa bili za maji kwa wananchi, hudumieni watu kwa kutumia mifumo inavyotakiwa kwa sasa,” amesema Waziri.
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa tabia ya kubambikiza bili za maji imekuwa ikilalamikiwa na wabunge lakini kuna baadhi ya maeneo inaendekezwa bila kujali haki ya wananchi ni kupata huduma bora.
Amewaagiza wataalamu kuzingatia utaalamu na kuzuia maji kuvuja akibainisha kuwa kwenye baadhi ya maeneo mabomba huchukua hadi miezi miwili bila kuzibwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Ruwasa, Ruth Koya amesema wako kwenye mikakati wa kuhakikisha maji yanapatikana nchi nzima, hasa kwenye maeneo ya vijijini.