Watuhumiwa wa uchochezi watoweka baada ya dhamana, wasakwa

Iringa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limefafanua madai yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kupotea kwa watuhumiwa wanne wanaodaiwa kushikiliwa na jeshi hilo, likisisitiza kuwa, hakuna aliyepotea mikononi mwa polisi, bali baadhi yao wanatafutwa kwa kuvunja masharti ya dhamana na tuhuma za mauaji.

Akizungumza na waandishi wa habari Februari 26, 2026 ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amesema watuhumiwa hao ni Ibrahim Myovella (33), Asajile Anthony (33), Anthony Mwasika (29) na Ally Kalolo (26).

Kuhusu tuhuma za uchochezi kabla ya uchaguzi 2025, jeshi hilo limesema watuhumiwa hao walihusishwa na tuhuma za kuhamasisha maandamano na kuchapisha maudhui ya uchochezi dhidi ya Serikali kupitia mitandao ya kijamii, wakidaiwa kulenga kuvuruga uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Inadaiwa, walikuwa wakihusishwa na kundi la vijana waliotambulika kwa jina la ‘Watoto wa mbwa’ waliodaiwa kuwa na malengo ya kuharibu miundombinu ya Serikali ikiwamo kuhatarisha usalama wa vyanzo vya maji mkoani humo.

Inaelezwa kuwa, katika hatua ya awali, Asajile Anthony, mkulima mkazi wa Ihemi, alikamatwa Oktoba 24, 2025 kwa tuhuma za kuchapisha maudhui ya uchochezi kupitia akaunti ya Facebook iliyotajwa kwa jina la ‘Mnyakyusa mpinga utekaji.’

Kamanda Bukumbi  amesema mtuhumiwa huyo alishikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Iringa na baadaye kupewa dhamana Desemba 30, 2025 kwa masharti ya kuripoti kila baada ya siku tano.

Hata hivyo, amesema aliripoti hadi Januari 15, 2026 nkisha kutoripoti tena, hatua inayodaiwa kuwa ni

Kamanda Bukumbi amesema kwa upande wa Myovella, alikuwa anatafutwa kwa tuhuma za uchochezi kupitia makundi ya WhatsApp, likiwamo kundi la M4C Ruaha, alilodaiwa kuliongoza.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, Februari 10, 2026, Myovella alikamatwa pamoja na Anthony Mwasika na Ally Kalolo kwa tuhuma za kumshambulia mkazi wa Ipogoro aitwaye Benito Avinash na kuwa watatu hao walidaiwa kupewa dhamana ya Polisi Februari 17, 2026 na kutakiwa kuripoti tena Februari 18, 2026.

Kamanda Bukumbi amesema watuhumiwa hao hawakuripoti baada ya kubaini kuwa mtu waliyedaiwa kumjeruhi alifariki dunia, hivyo kuanza kutafutwa kwa tuhuma za mauaji na hatua za kisheria dhidi ya wadhamini wao zinaendelea.

Vilevile, Kamanda Bukumbi amesema upelelezi wa shauri hilo unaendelea na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

“Tunatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa watuhumiwa hawa azifikishe katika kituo chochote cha polisi,” amesema Kamanda Bukumbi.