BOT yahamasisha kampeni ya malipo kidijitali

Kigoma. Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeongeza kasi ya kampeni ya kuhamasisha matumizi ya mifumo ya malipo ya kidijitali badala ya fedha taslimu, ikieleza kuwa hatua hiyo itaimarisha usalama na kupunguza hasara inayotokana na uchakavu wa noti na sarafu.

Akizungumza leo Jumamosi, Februari 28, 2026 katika mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari kutoka mikoa ya Katavi, Tabora, Kagera na Kigoma, Meneja Msaidizi Uchumi na Takwimu wa BoT, Shamy Chamicha  amesema bado kuna changamoto ya wananchi kutunza vibaya fedha, hali inayosababisha noti nyingi kuharibika na kutoka kwenye mzunguko mapema.

Amesema fedha zinapochakaa au kuharibika na kushindwa kukidhi viwango vya kimataifa, hulazimika kurejeshwa BoT na kuteketezwa, jambo linaloigharimu Serikali fedha nyingi kwa ajili ya kuchapisha noti mpya au kuziondoa rasmi kwenye matumizi.

“Serikali inaingia gharama kubwa kutengeneza au kuteketeza fedha zinazotoka kwenye mzunguko kutokana na uchakavu au kuchanika. Ni muhimu wananchi wakazitunza vizuri au watumie zaidi mifumo ya kidijitali ili kupunguza gharama hizo,” amesema Chamicha.

Meneja Msaidizi wa Idara ya Mawasiliano BoT, Noves Moses amewataka wananchi wanaokusudia kukopa fedha kuhakikisha taasisi wanazotumia zimesajiliwa rasmi ili kuepuka usumbufu na vitendo vya udhalilishaji.

Ameonya pia tabia ya baadhi ya wakopaji wanaochukua mikopo kupitia programu za simu kisha kuvunja laini wakidhani wataepuka kulipa madeni.

“Kuvunja laini hakufuti deni. Taarifa zako zinahifadhiwa na deni linaendelea kukua. Mwisho wa siku utalilipa, tena likiwa limeongezeka zaidi,” amesema Moses.

Mchambuzi kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha ya BoT, Ephraim Madembwe amewashauri wananchi kutumia mifumo rasmi kuwekeza kwenye dhamana za Serikali, akieleza kuwa ni njia salama yenye faida.

Amefafanua kuwa, dhamana hizo zinazojumuisha muda mfupi na mrefu ni nyenzo zinazotumiwa na Serikali kukopa kutoka sokoni, hivyo mwananchi anayewekeza anakuwa ameikopesha Serikali na kunufaika na riba huku akiunga mkono miradi ya maendeleo.

“Tunawahamasisha wananchi kuchangamkia fursa hizi kwa kuwa ni uwekezaji salama unaowanufaisha wao binafsi na Taifa kwa jumla,” amesema Madembwe.