Chuo cha Aga Khan chatoa mafunzo ya malezi bora kwa watoto

Arusha. Katika kuimarisha malezi na makuzi bora kwa watoto, Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) kimeendesha programu maalumu za kuwajengea uwezo wadau mbalimbali, wakiwamo wawakilishi wa asasi za kiraia zinazojihusisha na maendeleo ya awali ya mtoto.

Mradi huo wa mafunzo kuhusu sayansi ya malezi na makuzi ya maendeleo ya awali ya watoto umefanyika leo, Jumamosi, Februari 28, 2026, jijini Arusha.

Mafunzo hayo yanatekelezwa na AKU kupitia Taasisi ya Maendeleo ya Binadamu pamoja na Taasisi ya Maendeleo ya Elimu Afrika Mashariki ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (IED, EA).

Mhadhiri wa AKU, Profesa Fortidas Bakuza amesema mafunzo hayo ya wiki moja yamehusisha mashirika ya kitaifa na kimataifa, wakufunzi na wahadhiri kutoka kwenye vyuo vinavyotoa mafunzo ya elimu ya malezi na makuzi ya awali ya watoto.


“Lengo la kuwajengea uwezo ni kuwawezesha kutoa huduma ya malezi na makuzi ya watoto wadogo kwa kuzingatia ufahamu na utalaamu,” amesema Profesa Bakuza.

Profesa Bakuza amefafanua kuwa malezi na makuzi ya awali ya watoto yanahitaji ufahamu sahihi, si kitu kinachoweza kufanywa na kila mtu atakayejisikia.

Mhadhiri huyo, amesisitiza dhumuni la Chuo Kikuu cha Aga Khan kuja na mafunzo hayo ni kuhakikisha watu wanakuwa na utalaamu unaofaa.

“Kwa mfano tunaanza na sayansi ya ukuaji wa ubongo, tukitambua ubongo wa mtoto unakuaje katika siku 1,000 za kwanza za makuzi yake. Siku 1,000 tunazozizungumzia zinaanzia tangu mimba inapotungwa hadi miaka mitatu ya kuzaliwa mtoto.

“Kuna vitu vingi ambavyo wazazi wanapaswa kuvifahamu, mama, baba na jamii inayomzunguka kuanzia chakula cha mama anachokula, mazingira anayojihusisha nayo ya kihisia, lishe na maono yake,” amesema.


Profesa Bakuza amesema ikitokea mama anapata changamoto yoyote katika ujauzito wake, haishii kumwathiri yeye pekee bali hadi ukuaji wa mtoto aliyepo tumboni.

“Anapojifungua na endapo hajapata mazingira sahihi inakwenda kumuathiri hata mtoto katika ukuaji wake. Hivyo vyote wanapata nafasi ya kujifunza, kwa sababu tunaamini ni wazazi na walezi wa watoto wao,” ameeleza.

Mtalaamu Mbobezi wa masuala ya malezi na makuzi bora kwa watoto wadogo kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Binadamu, Everlyne Okeyo amesema mafunzo hayo yameshirikisha pia watu wanaotoka katika NGO’s pamoja na walezi wanaoshughulikia masuala ya watoto chini ya miaka minane.

“Mafunzo haya ya siku sita yanazingatia sana tafiti zilizofanyika kuhusu watoto wanavyokua, hasa ukuaji wa ubongo na mambo gani yanachangia ubongo kuwa hali ya usawa.

“Pia, yana zingatia kabla ya mtoto hajazaliwa hadi kufikisha miaka minane na mazingira yake yanachangiajie anavyokua, matokeo yake ya baadaye ya afya, elimu na tabia yake ya baadaye.” amesema Okeyo.

Mbali na hilo, Okeyo amesema mafunzo hayo yanahamasisha jamii kuwekeza zaidi katika masuala ya watoto kwenye siku za awali za mtoto.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo, Fatina Mndeme amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao hasa kwa eneo analolifanyika kazi linahusisha watoto wachanga hadi miaka miwili.