Dereva wa bajaji adaiwa kujinyonga

Njombe. Dereva bajaji, Msafiri Sanga (40), amekutwa amefariki dunia kwa kile kilichoelezwa kuwa alijinyonga, huku chanzo kikitajwa ni wivu wa mapenzi.

Hata hivyo, leo Jumamosi Februari, 28 2026 alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga kwa njia ya simu ili kupata taarifa rasmi za tukio hilo, simu yake haikupokewa.

Mwili wa Sanga ulikutwa asubuhi ya Februari 26, 2026 ukining’inia kwenye nyumba ambayo ujenzi wake haujakamilika, siku mbili baada ya kutoweka nyumbani kufuatia ugomvi na mkewe.

Akizungumza na Mwananchi jana Februari 27, 2026, ndugu wa marehemu, Paulo Luvanda alisema usiku wa kuamkia Februari 24, walipigiwa simu na mama mkwe wa marehemu akieleza kuwa mke wa Sanga amempigia akidai mumewe ametoka nyumbani katika mazingira yasiyoeleweka.

“Saa tisa usiku tulipigiwa simu kuwa ametoweka nyumbani baada ya kutokea kutokuelewana kati yake na mkewe. Tulianza kumtafuta hadi tulipomkuta akiwa amejinyonga,” amesema Luvanda.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwembetogwa, George Mlelwa amesema amesikitishwa na tukio hilo akibainisha kuwa marehemu alikuwa nguvu kazi muhimu katika jamii.

“Uamuzi kama huu si sahihi. Vijana wanapaswa kutafuta ushauri wanapokumbwa na changamoto badala ya kuchukua hatua za kujiua,” amesema Mlelwa.

Diwani wa Mwembetogwa, Robart Shejamabu, amewataka vijana kuepuka kujitenga wanapopitia matatizo, akisema kufanya hivyo kunachochea uamuzi yasiyofaa.

“Kujifungia ndani au kubeba tatizo peke yako ni kujiweka gizani. Hakuna jipya chini ya jua, changamoto zipo na zinaweza kutatuliwa kwa ushirikiano,” amesema Shejamabu.

Katibu wa Madereva Bajaji Makambako, Pascal Shauri amesema matukio ya kujinyonga yanaongezeka Njombe, kuna haja ya Serikali na wataalamu wa saikolojia kuingilia kati kwa kutoa elimu kwa jamii.

“Wengi wanatajwa kujiua kwa wivu wa mapenzi, wengine wanahusisha na imani potofu. Lakini ukweli ni kwamba tunahitaji elimu ya afya ya akili ili kupunguza vifo hivi,” amesema Shauri.

Baadhi ya wananchi akiwamo Ester Wikes, wamewataka vijana kumrudia Mungu na kutafuta msaada wanapokumbwa na changamoto za maisha.