Fountain Gate yalamba dili | Mwanaspoti

TIMU ya Fountain Gate imeingia makubaliano ya miaka miwili yenye lengo la kuhakikisha kwamba wachezaji na benchi la ufundi wanakuwa katika mazingira bora ya kiutendaji wanapokuwa katika majukumu yao uwanjani.

Dili jipya la timu hiyo ukiondoa yale ya udhamini wa jumla katika Ligi Kuu Bara yanayotolewa na wadhamini wa michuano hiyo, limetoka katika maji ya Nano Filter ya jijini humo.

Akizungumza wakati wa halfa ya utiaji saini wa mkataba huo, rais wa klabu hiyo, Japhet Makau amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya timu hiyo na umefanyika baada ya utafiti wa kina ili kupata mshirika sahihi mwenye uwezo wa utaalamu katika uzalishaji wa bidhaa hiyo.

Makau alisisitiza kuwa makubaliano hayo hayatawanufaisha wachezaji wa timu hiyo ya Ligi Kuu Bara pekee, bali pia yatazigusa timu zote za vijana, ambapo mitambo ya maji itawekwa katika akademi ya Fountain Gate ili kuhakikisha afya na mazingira bora kwa wachezaji chipukizi.

Mkurugenzi wa Nano Filter, Ruth Lukwaro, amesema kupitia ushirikiano huo utasaidia kuzifanya wachezaji kujikita katika kupambania neno ya klabu na kuendeleza vipaji walivyo navyo.

“Kupitia Fountain Gate tumefurahi kupata nafasi ya kufanya kazi na klabu kubwa,” amesema Lukwaro.

Profesa Askwari Hilonga, mwenyekiti wa taasisi hiyo amesema wataendelea kuimarisha ushirikiano wa kimichezo na kijamii.