Korti yaruhusu mapitio shauri la kufutwa kazi ofisa wa Nida

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, imempa ushindi wa aliyekuwa Ofisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Njiti Manyumba dhidi ya mwajiri wake baada ya mabishano makali ya kisheria.

Uamuzi huo umetolewa Februari 27, 2026 na Jaji Elizabeth Mkwizu wakati akitoa uamuzi kuhusiana na maombi ya Manyumba kuongezewa muda kufungua maombi ya kupatiwa kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya Mahakama nje ya muda.

Katika uamuzi wake, Jaji Mkwizu amekubaliana na hoja moja tu, kati ya nyingi kwamba, kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria anaoona unahitaji Mahakama kuupitia, hivyo imempa siku 14 kufungua maombi yake ya kupatiwa kibali hicho.

Manyumba alifungua maombi hayo ya kuongezewa muda namba 28086 ya 2025 dhidi ya Katibu Mkuu Kiongozi kama mujibu maombi wa kwanza, Nida mjibu maombi wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mjibu maombi wa tatu.

Kwa mujibu wa hati ya kiapo aliyowasilisha Mahakama Kuu, Manyumba alieleza kuwa, aliajiriwa na Nida Septemba 10, 2015 kama Ofisa Usajili Daraja la II na ajira yake ikathibitishwa na mjibu maombi wa pili, Septemba 30, 2016.

Hata hivyo, anadai kuwa Desemba 14,2022, alipewa notisi na mwajiri ikidai amefanya makosa matatu kati ya Desemba 2021 na Oktoba 2022, na akapewa siku 14 kujibu tuhuma hizo, ambazo hata hivyo katika uamuzi huo hazikuwekwa wazi.

Desemba 28, 2022 alijibu na kukanusha mashitaka yote lakini mjibu maombi wa pili alikataa majibu yake na kuunda Kamati ya Nidhamu ya watu wanne akiwamo Ofisa Rasilimali Watu (HR) wa Nida, Edna Wanna.

Katika usikilizwaji, mwajiri hakuita shahidi yeyote na kwamba yeye (Manyumba), alishiriki kikao cha kamati hiyo ya nidhamu bila uwakilishi, akasaini mwenendo wa shauri pasipo kukagua na alishitakiwa kwa makosa yasiyo na mashiko.

Machi 10, 2023, mleta maombi ambaye ni Manyumba alipokea barua ya kuachishwa kazi kuanzia Januari 31, 2023 pasipo kupewa nafasi ya kujitetea.

Aliomba apatiwe ripoti ya uchunguzi na barua za uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Nidhamu, lakini hakupewa na kuishiwa kupewa tu mwenendo, akakata rufaa Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), rufaa yake ikatupwa Februari 20, 2024.

Kwa mujibu wa mleta maombi, rufaa yake hiyo ilitupwa pasipo PSC kuzingatia sababu alizoziwasilisha, lakini halikadhalika rufaa yake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nayo ilitupwa bila kufanyia kazi sababu zake za rufaa.

Katika kipindi hicho, anadai aliumwa na kupatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Februari 15, 2025 na pia akakabiliwa na matatizo ya kifedha yaliyomfanya ashindwe kufungua maombi ya kibali cha Mahakama.

Baada ya kupata nafuu, alirejea kuandaa rasimu ya maombi ya kupatiwa kibali cha Mahakama ili aweze kufungua maombi ya mapitio ya Mahakama (judicial review), lakini hakukamilisha kutokana na uchaguzi mkuu na kuzimwa kwa mtandao.

Katika maombi hayo, anadai kufutwa kwake kazi kulikiuka Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya Tanzania kutokana na kutopewa nafasi ya kujitetea na pia hakuitwa mbele ya Mamlaka ya Nidhamu na alinyimwa ripoti ya uchunguzi.

Pia, alidai kitendo cha HR, Edna Wanna kuwasilisha mashitaka kulikiuka kanuni ya kutokuwa na upendeleo, kwa kuwa mwendesha mashitaka na hapo hapo Jaji.

Mbali na madai hayo, alidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria katika mchakato mzima wa uamuzi na kueleza Rais alikataa rufaa yake kwa kuegemea mwenendo wa mashitaka ambao haukuzingatia kikamilifu sababu za rufaa.

Mjibu maombi 1, 2 na 3 walipinga maombi hayo ya kuongezewa muda, wakieleza kuwa, kulikuwa hakuna ukiukwaji wowote wa sheria katika uamuzi unaolalamikiwa kiasi cha kuhitaji Mahakama kufanya mapitio ya kimahakama ya uamuzi huo.

Walieleza kuwa, mleta maombi alikuwa ameshindwa kujenga hoja kwa nini alichelewa kufungua maombi hayo kwa siku 82 kuanzia Agosti 15, 2025 hadi Novemba 7, 2025 na kwamba sababu alizotoa hazitoshi kuishawishi Mahakama.

Waliegemea msimamo uliotolewa, shauri namba 12 la 2018 kati ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dhidi ya African Cargo Handling Ltd, Mahakama ilisema matatizo ya kifedha au binafsi hayahalalishi kuchelewa kufungua shauri.

Kuhusu ugonjwa, wajibu maombi walijenga hoja kuwa barua ya JKCI ambayo ni kielelezo “K” hakioneshi kama alishindwa kabisa kutafuta nafuu ya kisheria na kwamba matibabu pekee hayawezi kutoa udhuru wa kuchelewa kufungua shauri.

Mbali na hoja hiyo, walijibu hoja ya ukiukwaji wa sheria na kueleza kuwa mleta maombi huyo alipewa haki ya kusikilizwa kwa kujulishwa mashitaka yake, akayajibu na akafika mbele ya kamati ya uchunguzi na kusaini mahudhurio.

Wajibu maombi hao walikanusha madai kuwa, mleta maombi aliadhibiwa bila kusikilizwa na kueleza kuwa alipewa nyaraka zote alizoziomba ikiwamo ripoti ya uchunguzi na kwamba alikuwa na nyaraka zote muhimu za kufungua rufaa.

Katika uamuzi wake ambao umewekwa katika tovuti ya Mahakama Februari 28, 2026, Jaji Mkwizu alisema ni jambo lililo wazi kuwa maombi ya kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya Mahakama yanapaswa kufunguliwa ndani ya miezi sita.

Hata hivyo, alisema katika shauri hilo, mleta maombi hakuzingatia takwa hilo la kisheria na kuegemea katika sababu za ugonjwa na kwamba kuzimwa kwa intaneti Oktoba 29 hadi Novemba 3, 2025 kulimfanya ashindwe kuandaa nyaraka.

Jaji Mkwizu alisema baada ya kupitia nyaraka za maombi hayo, ushahidi wa ugonjwa uliopo hautoi picha ya namna ulivyomfanya ashindwe kufungua maombi hayo kati ya Februari 2025 na Oktoba 2025 na haielezi kwanini alichukua muda mrefu wa kuwasiliana na mawakili wake ili waweze kufungua maombi hayo mahakamani.

“Mleta maombi ametaja suala la ugumu wa kifedha kama moja ya sababu zilizochangia kuchelewa kufungua maombi. Lakini, sheria zetu ziko wazi kuwa matatizo ya kiuchumi au kukosa fedha sio sababu ya kuongezewa muda,” alisema Jaji Mkwizu.

“Kuna hoja nyingine hapa. Kwamba baada ya kupokea barua ya JKCI alitafuta ushauri lakini kiapo chake kipo kimya na hakitaji ni kina nani alioomba ushauri kwao na aina ya ushauri aliokuwa anautafuta kabla ya kufungua shauri.”

Kuhusu hoja ya ukiukwaji wa sheria, Jaji alisema hata kama hakuna maelezo ya kutosha ya kwanini mleta maombi alichelewa kufungua maombi, lakini pale kunapokuwepo na ukiukwaji wa sheria, kunaruhusu muda huo kuongezwa.

“Sheria inatambua kuwa pale mleta maombi anaibua maswali juu ya mamlaka au ukiukwaji wa taratibu, Mahakama inapaswa kuzingatia madai hayo kwa minajili ya kutenda haki. Lakini sio kila ukiukwaji unaruhusu kuongezwa kwa muda,”alisema Jaji Mkwizu.

“Ukiukwaji unaolalamikiwa ni lazima uwe wazi, unajitosheleza na unajionesha kwenye kumbukumbu, ambao hauhitaji uchunguzi mrefu kupata ushahidi. Mahakama ni lazima ijiridhishe kuwa huo ukiukwaji sio uvumi,” alisisitiza.

Katika maombi yaliyokuwa mbele yake, Jaji Mkwizu alisema katika aya ya 13 ya kiapo cha mleta maombi, anadai uamuzi unaolalamikiwa ulijaa ukiukwaji wa taratibu ikiwamo kunyimwa usawa katika hatua zote za usikilizwaji wa shauri lake.

Lakini, Jaji akasema pili, mleta maombi analalamika kuwa mjibu maombi wa pili (Nida) aligeuka kuwa mshitaki na hapo hapo mtoa uamuzi, kunyimwa haki ya kuwauliza mashahidi maswali ya dodoso na hakupatiwa nyaraka muhimu.

Jaji Mkwizu alisema ingawa tuhuma hizo zinaibua hoja za msingi, lakini sheria inataka katika kuongeza muda, ukiukwaji wa sheria unaotajwa lazima uonekane kwenye kumbukumbu wenyewe wala hauhitaji majibizano au ushahidi mrefu.

Kwa mujibu wa Jaji Mkwizu, kwa kutizama kumbukumbu za shauri hilo, barua ya kufutwa kazi ilitolewa Machi 10, 2023 ikionesha amefutwa kazi kuazia Januari 31, 2023 na kwamba hili linaonesha wazi wazi kulikuwa na ukiukwaji wa sheria.

Hivyo, Mahakama inaona maombi yake yana mashiko, hivyo inayakubali na inatoa muda wa siku 14 kuanzia tarehe ya kutolewa uamuzi huo kwa mleta maombi awe amewasilisha maombi ya kupewa kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya Mahakama.