Arusha. Mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Ijumaa Februari 27, 2026 imesababisha kifo cha mwanafunzi mmoja na wawili kuokolewa wakati wakielekea shuleni kupitia kwenye korongo lililokuwa likipitisha maji kutoka maeneo ya miinuko.
Mwanafunzi huyo, Daniel Joseph (11) wa darasa la nne katika Shule Msingi Terrat iliyopo Kata ya Muriet jijini Arusha, mwili wake umehifadhiwa kwenye Kituo cha Afya Muriet.
Baba mzazi wa marehemu, Joseph Masawe ameleza kusikitishwa na kifo cha ghafla na mazingira yaliyosababisha kifo cha mtoto wake.
“Ni tukio la huzuni kwa familia yangu, mtoto ameamka vizuri kwa ajili ya kwenda shule lakini safari yake ya masomo imekuwa mauti,” amesema Masawe.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mashariki kulipotokea tukio hilo, Emmanuel Sanare amewataka wananchi kuchukua tahadhari kabla ya kuwaruhusu watoto wao kwenda shule.
“Nitoe wito kwa wazazi katika kipindi hiki cha msimu wa mvua kujiridhisha kabla ya kuwaruhusu watoto kwenda shule na kuwashauri kutumia barabara,” amesema Sanare.
Amesema jiografia ya Mtaa wa Mashariki ipo na makorongo makubwa ambayo ameshatolea taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha ambaye ameahidi kujenga vivuko kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo kuhusu tukio hilo zinaendelea.