Dar es Salaam. Kama uliwahi kusikia kuhusu neno mapito magumu katika utumishi wa kisiasa, basi mbunge wa sasa wa Ukonga, Bakari Shingo ni miongoni mwa mifano sahihi ya watu waliopita katika njia hiyo hadi kushika wadhifa alionao.
Shingo aliyeianza siasa miaka 33 iliyopita akiwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anasema aliwahi kujikuta katika ugomvi mara kadhaa na viongozi wa wilaya na mkoa hadi kuweka mahabusu kwa sababu za kisiasa.
Mwanasiasa huyo anayewawakilisha wakazi wa Ukonga kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, hatua yake ya kuwa kiongozi wa Mtaa wa Gongo la Mboto anayetokana na upinzani ilimpa kashfa lukuki, majina mabaya na hata kuharibu biashara zake.
Shingo anasema hayo wakati wa mahojiano maalumu, yaliyofanyika hivi karibuni katika ofisi za Mwananchi, Tabata Relini, jijini Dar es Salaam.
Katika simulizi yake, anasema aliwahi kuingia kwenye mgogoro na baadhi ya viongozi uliosababisha awekwe ndani akituhumiwa kwa kughushi nyaraka za Serikali, wakati huo akiwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Gongo la Mboto kwa tiketi ya Chadema.
Tukio kama hilo, anasema lilimtokea tena wakati sio kiongozi wa kisiasa bali mwanachama wa kawaida wa ACT- Wazalendo, huku akiendelea na biashara zake.
Hata hivyo, anasema safari yake ya kisiasa ilianza mwaka 1993 alipokikataa hadharani Chama cha Mapinduzi (CCM) akiwa kijana, licha ya chama hicho kuwa madarakani.
Anasema alijiunga na Chadema, kwa sababu hakukubaliana na mfumo uliokuwa ukitumika na CCM wakati huo, kukabiliana na maadui watatu ujinga, maradhi na umaskini.
Akiwa Mwenyekiti wa kwanza wa Serikali ya Mtaa wa Gongo la Mboto kwa tiketi ya Chadema, anasema alifanya mambo makubwa anayojivunia hadi leo, likiwamo ujenzi wa ofisi ya Serikali ya mtaa.
“Mwaka 1994 kulikuwa na mpango wa ofisi za Serikali za mitaa kuwa nyumbani kwa mwenyekiti husika, maana yake vikao vyote vingefanyika nyumbani kwake,” anasema.
Anasema kuwa wakati huo alikuwa pekee kutoka upinzani huku wajumbe wengine wote wakiwa CCM.
Shingo anasema kuwa alipambana kutafuta ofisi ya kupanga, lakini hata ilipopatikana, halmashauri ilikataa kuilipia kwa madai ya kukosa fedha za kulipia pango.
“Nilianza kuwatafuta wadau. Kwa kweli nilikuwa nao wengi, niliowafahamu kupitia kazi yangu ya ufundi wa kusuka nyaya majumbani. Nilikuwa na marafiki watumishi wa umma na wafanyabiashara. Niliwashawishi, na mmoja wao alitoa eneo ambalo hadi leo hati yake inasoma jina langu,” anasema.
Katika mchakato huo, alisema baadhi ya wanachama wa CCM walimtenga na kumuachia jukumu la kupokea kiwanja hicho afanye peke yake kwa kushirikiana na wananchi, na alifanikiwa kulitekeleza.
“Hali hiyo haikunikatisha tamaa. Niliendelea kujenga hoja katika vikao vya halmashauri, na ikaonekana kuwa katika dunia ya leo haiwezekani ofisi ya Serikali ya mtaa kuwa nyumbani kwa mwenyekiti,” anasema.
Gongo la Mboto ulikuwa mtaa wa kwanza kumiliki ofisi yake rasmi ya Serikali ya mtaa mwaka 1996. Mageuzi hayo aliyatekeleza akiwa mwanachama wa Chadema.
Hata hivyo, hakudumu ndani ya Chadema. Baada ya kuingia katika mgogoro na uongozi wa chama hicho alipokuwa akishika wadhifa wa Katibu Mwenezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, alivuliwa uanachama.
“Tulipingana na viongozi wa wakati ule, na mimi ni miongoni mwa makada tuliotimuliwa. Tuliitwa majina mbalimbali, ikiwamo vibaraka wa CCM, lakini ndivyo siasa zilivyo,” anasema.
Anasema baada ya kuachana na Chadema, alikaa kando bila kujiunga na chama chochote, ingawa aliendelea kufanya siasa za chini kwa chini.
Baadaye alihisi ana jambo la kuzungumza lakini akakosa jukwaa, ndipo alipojiunga na Chama cha Wananchi (CUF).
Akiwa CUF, anasema aligombea tena uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Gongo la Mboto kupitia chama hicho na akashinda.
Anasema alifanikiwa kuweka rekodi nyingine kwa kusambaza maji katika mtaa huo kwa kushirikiana na marafiki zake.
“Nilifanikiwa kusambaza maji Gongo la Mboto, na hadi nilipoondoka, zaidi ya asilimia 80 ya miundombinu ya maji ilikuwa imewekwa chini ya ardhi. Hadi leo, karibu kila nyumba ina miundombinu hiyo,” anasema.
Shingo anasema ingawa alianza siasa katika nafasi ndogo, isichukuliwe kama kigezo cha kumpima kisiasa.
“Turufu hiyo naamini ilinisaidia. Kata ya Gongo la Mboto imezalisha wakazi wengi zaidi wanaohamia maeneo mengine; ndiyo inaongoza kwa watu wanaosambaa kwenda kuanzisha makazi sehemu mbalimbali,” anasema.
Anasema aliungwa mkono na jamii, hakuwa na shaka kuhusu idadi ya kura za ubunge.
Anasema anajivunia kutangazwa kwake mshindi wa ubunge na anatembea kifua mbele, akisisitiza kuwa alistahili ushindi huo kutokana na maandalizi aliyoyafanya.
Shingo anasema tangu aingie madarakani amefanikiwa kuwapeleka vijana wengi shuleni.
Hata hivyo, anasema ameanza kupata upinzani kutoka kwa baadhi ya washindani wake, wanaodai kuwa anawachonganisha na wananchi.
Anasema madai hayo si kweli, kwa kuwa anachofanya ni kurudisha fadhila kwa waliomsaidia.
“Wananchi wamenisaidia, wapo waliochangia fedha na muda. Nisingeweza kubeba gharama zote peke yangu. Nirudishaje wema wao? Nasema kweli, sina shida ya fedha ya kula, lakini kitendo cha kunipa cheo hiki kimeniongezea fursa za kiuchumi. Nilichokifanya ni kuwagawia na nitaendelea kufanya hivyo,” anasema.