Arusha. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imejipanga kurejesha hekta milioni 5.2 za ardhi iliyoharibika ifikapo mwaka 2030, kama sehemu ya jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuboresha uhifadhi.
Lengo ni kurejesha uoto wa asili katika maeneo mbalimbali yaliyopoteza misitu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha biaonuwai na kuboresha maisha ya wananchi.
Hayo yamesemwa jana Ijumaa Februari 27, 2026 na Mwakilishi wa Kamishna wa TFS, Dk Fortunate Senya alipozungumza na wakulima na wazalishaji wa mazao ya misitu katika kongamano lililolenga urejeshaji na uhifadhi wa mazingira ikiwamo kilimo mseto, misitu, uzalishaji wa asali, mbegu na miche.
Amesema kuwa takwimu zinaonesha kila mwaka hekta 469,000 zinaharibiwa, hivyo watahakikisha ardhi iliyoharibiwa inarejeshwa katika uoto wake wa asili.
“Tumejipanga hadi ifikapo mwaka 2030 Tanzania itakuwa imerejesha ardhi iliyoharibiwa, hekta milioni 5.2.Tutashirikiana na wadau ikiwamo kutoa elimu kwa jamii,” amesema
Mwakilishi Msaidizi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Fao), nchini Tanzania, Charles Tulahi amesema wameamua kukutanisha wazalishaji wadogo wa mazao yatokanayo na misitu na wakulima wanaotoa mchango mkubwa wa uhakika wa chakula ambao watanufaika na mradi wa uhifadhi na urejeshaji wa misitu.
Amesema wameamua kuwakutanisha wazalishaji hao na taasisi za kifedha ili kuendeleza mifumo bunifu ya uwezeshaji kifedha kama sehemu ya kuimarisha shughuli za urejeshaji na uhifadhi wa mazingira.
“Licha ya umuhimu wa wakulima na wazalishaji hawa wadogo ambao wanakabiliwa na ukosefu wa mikopo,athari za mabadiliko ya tabia nchi ndiyo maana tunawakutanisha hapa ili kujadili namna ya kupambana na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi,” amesema.
Mmoja wa wavunaji wa asali kutoka Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita), wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro, Asha Hamisi ametaja changamoto kubwa wanayokutana nayo katika utekelezaji wa majukumu yao ni mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha kupata mavuno kidogo.
“Kiukweli tunatamani kusaidiwa kwenye mitaji na elimu, kwani mabadiliko ya tabia nchi yanachangia tupate mazao kidogo, hivyo kasi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi inapungua na wengine wanaharibu mazingira,” amesema
Maria Shinini kutoka kikundi cha Nameloc, wilayani Monduli ametaja moja ya changamoto zinazowakabili katika uzalishaji wa asali ni umbali wa kusafirisha malighafi kupeleka kwenye kiwanda cha kuchakatia mazao yao ya nyuki.
“Mitaji nayo ni changamoto, tuna mizinga 130 ila lengo letu ni kuwa na mizinga 300 ila tumekwama kwa sababu mtaji bado siyo mkubwa. Tunaamini kwa kupitia jukwaa hili wadau watatusaidia na tutatimiza lengo letu,”amesema.