Bakari Mahundu
February 28, 2026
0 Comments
Israel imeanzisha mfululizo wa mashambulizi ya makombora dhidi ya Iran mapema leo Jumamosi asubuhi, kufuatia wiki kadhaa za mvutano mkali uliokuwa ukiongezeka kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump, na Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ametangaza kuwa nchi hiyo ipo katika hali ya hatari (state of emergency), wakati moshi mzito ukionekana ukifuka kufuatia mlipuko uliotokea katikati ya Jiji la Tehran.
Vyombo vya habari vya Serikali ya Iran vimeripoti kusikika kwa milipuko katika mji mkuu huo.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilianzisha shambulio hilo la kushtukiza kabla ya kutoa onyo kwa raia wake kujiandaa kujikinga iwapo Iran itajibu mashambulizi hayo, huku ving’ora vya tahadhari vikisikika katika maeneo mbalimbali ya Israel.
Kupitia taarifa ya kitaifa ya tahadhari, Jeshi la Israel limesema: “Huu ni ujumbe wa tahadhari wa awali kwa ajili ya kuwaandaa wananchi dhidi ya uwezekano wa kurushwa makombora kuelekea Dola ya Israel.”
Aidha, anga la Israel limefungwa kwa safari za ndege za kiraia kufuatia shambulio hilo la asubuhi.
Mlipuko huo umetokea wakati mvutano ukiwa mkubwa kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.
Wiki hii, Trump alitoa onyo kali akidai kuwa Iran inatengeneza silaha zinazoweza kulenga Marekani katika siku za karibuni.
Akihutubia taifa katika hotuba yake ya State of the Union Jumanne, Trump alisema Tehran “inafanyia kazi makombora ambayo hivi karibuni yataweza kufika” Marekani.
Pia aliahidi kuzuia Iran, aliyoitaja kuwa “mfadhili namba moja wa ugaidi duniani,” isipate silaha za nyuklia.