Viongozi wajitokeza maziko ya Kardinali Pengo, Pugu

Dar es Salaam. Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wa kitaifa wamejitokeza kushiriki mazishi ya Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, yanayofanyika katika Kituo cha Hija ya Bikira Maria, Pugu, jijini Dar es Salaam.

Ibada ya Misa Takatifu ya mazishi inaongozwa na viongozi wa Kanisa Katoliki, huku maelfu ya waumini na wananchi wakihudhuria kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo wa kiroho aliyelitumikia Taifa kwa miongo kadhaa.

Ibada hiyo inayofanyika leo Februari 28, 2026 inaongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Juda Thadeus Ruwa’ichi.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akisalimiana na viongozi wastaafu akiwamo Makamu wa Rais mstaafu, Dk Philip Mpango, mawaziri wakuu wastaafu, Kassim Majaliwa, Mizengo Pinda na Jaji Joseph Warioba.



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel Nchimbi, ameongoza waombolezaji katika hafla hiyo akimwakilisha Rais akiwa na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba.

Viongozi wengine walioudhuria ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, Makamu wa Rais mstaafu, Philip Mpango, pamoja na Waziri Mkuu mstaafu Joseph Sinde Warioba.

“Pamoja na kwamba maadhimisho haya yalikuwa ya jana lakini tunashkuru Mungu na leo mmejumuika nasi hapa tunashukuru sana,” amesema Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima.

“Napenda kumtambulisha Makamu wa Rais, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, naomba niwatambulishe wastaafu wafuatao Makamu Mstaafu wa Rais, Isdory Mpango.”

Hata hivyo alivyosimama Dk Mpango waumini wengi walipiga vigelegele. Akamtambulisha pia Waziri Mkuu mstaafu Jaji Sinde Warioba ambaye naye alishangiliwa na Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda naye akashangiliwa.

Pia, alimtambulisha Waziri Mkuu mstaafu, Majaliwa Kassim Majaliwa, ambaye naye alipokewa kwa nderembo na vifijo. Akatambulishawa Anna Makinda, Simbachawene ambao nao walishangiliwa.

Pamoja na viongozi hao, maziko hayo pia yamehudhuriwa na viongozi wengine mbalimbali wa kiserikali, mawaziri na wabunge mbalimbali.

Pamoja na viongozi hao, Ibada hiyo imehudhuriwa na ma Kardinali na Maaskofu mbalimbali kutoka nje ya nchi na akiwamo Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora.

Katika salamu zake za rambirambi, Balozi wa Vatican (Apostolic Nuncio) nchini Tanzania, Askofu Angelo Accattino amesema “Tumekusanyika hapa kuadhimisha mazishi ya Kardinali Pengo tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha yake, kanisa Tanzania limebarikiwa kuanza kama Kasisi, Askofu na Kardinali huyu, vipaji vyake vingi alivyopata mafunzo kutoka shule na vyuo mbalimbali vilimsaidia kupata ujuzi uliomsindikiza katika ujuzi wake wote.”

Amesema kuanzia mwaka 2007 hadi 2009 pamoja na kuwa miongoni mwa wahudumu wa idara mbalimbali za Vatican mchango wake kwa Kanisa Katoliki Tanzania umeonekana katika kukuza haki, umoja na uwajibikaji wa maadili, akilifanya kanisa kama dira hasa wakati wa changamoto za kijamii.

Viongozi mbalimbali kutoka nje ya nchi wamemwelezea Kardinali Pengo kama mtetezi wa haki, mwalimu wa maadili na mshauri wa viongozi wa Serikali katika nyakati mbalimbali za kihistoria.

Mazishi hayo yamehudhuriwa pia na maaskofu, mapadri, watawa, viongozi wa dini mbalimbali pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti ya nchi, wakionesha heshima na upendo kwa marehemu.

Kardinali Pengo anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kuliongoza Kanisa Katoliki Tanzania, kuhubiri amani na kuhimiza mshikamano wa kitaifa, mchango ambao umeacha alama isiyofutika katika historia ya Taifa.