Iran yajibu mapigo, yashambulia mataifa yenye mali za Marekani

Serikali ya Iran, jana Jumamosi, Februari 28, 2026, ilithibitisha mashambulizi yake dhidi ya maeneo kadhaa waliyoyalenga, kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, yakiwemo Bahrain, Kuwait, Qatar na Falme za Kiarabu (UAE), ambako kuna kambi za kijeshi zenye rasilimali za Marekani.

Al Jazeera imeripoti kwamba Jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) lilidai kuwa malengo yote ya kijeshi ya Israel na Marekani katika Mashariki ya Kati yameshambuliwa “kwa mapigo makali ya makombora ya Iran.”

“Operesheni hii itaendelea bila kusita hadi adui atakaposhindwa kikamilifu,” lilisema jeshi hilo. Aidha, liliongeza kuwa mali zote za Marekani katika eneo hilo zinachukuliwa kuwa shabaha halali kwa jeshi la Iran.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hamid Ghanbari, ameiambia Al Jazeera kuwa Iran ina haki ya kujilinda na inasikitika kwa hasara yoyote ya kibinadamu iliyosababishwa na ongezeko la sasa la mashambulizi ya kijeshi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema katika barua aliyotuma kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) na Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres kuwa Iran “itaendelea kutumia haki yake ya kujilinda kwa uthabiti na bila kusita hadi uchokozi utakapokoma kikamilifu na bila shaka yoyote.”

Mtu mmoja ameuawa mjini Abu Dhabi, mji mkuu wa Falme za Kiarabu (UAE), baada ya makombora kadhaa yaliyorushwa kutoka Iran kuzuiliwa angani, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya nchi hiyo, ambalo halikutoa maelezo zaidi.

Wakati huohuo, moto ulizuka karibu na hoteli moja katika kivutio cha Palm Islands jijini Dubai, huku moshi mzito ukionekana kwa mbali na milipuko kadhaa kusikika siku nzima.
Ofisi ya habari ya Dubai baadaye ilithibitisha kutokea kwa “tukio” katika jengo lililopo eneo la Palm Jumeirah lililosababisha moto na watu wanne kujeruhiwa.