Arusha. Mbuni amechaguliwa kuwa ndege wa Mwaka 2026, baada ya kuibuka mshindi katika kura za kitaifa zilizoshirikisha wapenzi wa ndege nchini na kimataifa, akimrithi ‘kwezi maridadi’ (Superb Starling), aliyeshikilia taji hilo kwa mwaka 2025.
Ndege huyo mkubwa zaidi duniani, ametwaa heshima hiyo baada ya kuwashinda washindani wake wanne maarufu wa uwanda wa nyasi katika kampeni ya kitaifa iliyoanza Septemba, 2025.
Mpango huo wa mashindano umeratibiwa na taasisi ya uhifadhi ya Nature Tanzania kwa kushirikiana na BirdLife International.
Ikumbukwe kwamba matokeo hayo yamekuja katika kipindi hiki cha kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanyamapori duniani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 3.
Shindano la mwaka 2026 lilijumuisha aina nne za ndege wanaopatikana katika nyanda za malisho ambao ni Mbuni, Kanga Shingo -Nyekundu, Tandawala Kori na Ndege homa wa Ardhini (Southern Ground Hornbill).
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo leo Jumapili Machi Mosi, 2026 katika Shule ya Msingi Manyara Ranch, Kata ya Makuyuni wilayani Monduli, Ofisa Mawasiliano wa Nature Tanzania, Gaudensia Mariki amesema Mbuni alipata kura 303 sawa na asilimia 38.9 ya kura zote zilizopigwa. Kati ya hizo, kura 186 zilipigwa mtandaoni na 117 zilikuwa za karatasi.
“Mpinzani wake wa karibu, Kori Bustard anayejulikana kama ‘Balozi wa Nyanda za Wazi,’ alipata kura 217 (209 mtandaoni na nane za karatasi), sawa na asilimia 30.1,” amesema Mariki.
Kanga wa shingo Nyekundu ‘Red-necked Spurfowl’ ameshika nafasi ya tatu kwa kupata kura 117 (60 mtandaoni na 57 za karatasi), huku ndege Homa wa Ardhini ‘Southern Ground Hornbil’ akishika nafasi ya nne kwa kujishindia kura 136 (132 mtandaoni na nne za karatasi).
“Upigaji kura ulifanyika kwa njia ya mtandao na kwa njia ya kawaida, ukihusisha Watanzania wa ndani na nje ya nchi pamoja na watalii na wapenzi wa ndege duniani kote” amesema na kuongeza;
“Kwa ushindi huu, ndege mshindi anakuwa balozi wa kitaifa katika kampeni inayoendelea ya kulinda nyanda za malisho chini ya kaulimbiu “nyanda za malisho si jalala,” amesema Mariki.
Amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhamasisha ulinzi wa ndege na kuhifadhi makazi yao na kuwalinda dhidi ya Toshio la kutoweka.
Kaimu Ofisa Utalii wa Wilaya ya Monduli, Jonas Nyange amesema ushindi wa ndege Mbuni ni jambo la kujivunia kwa eneo hilo na wameahidi kumlinda rasmi dhidi ya ujangili.
“Licha ya kuwa haruki, ni ndege mwenye hadhi kubwa, anayetaga mayai makubwa zaidi duniani na huvutia wageni wengi wa kimataifa wanaokuja kumwona na kumchunguza, hivyo tutamlinda maana umaarufu wake sasa imeongezeka,” amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Esilalei, Leeko Tayai ametoa wito kwa serikali kumtambua rasmi Mbuni kama ndege wa taifa ili kuimarisha juhudi za uhifadhi.
Ameongeza kuwa jamii tayari imechukua hatua za kulinda ndege huyo mkubwa.
Mwanafunzi wa Darasa la Saba kutoka Shule ya Msingi Ziwa Manyara, Zawadi Shinini amesema anafurahia kuona wanafunzi wakihusishwa katika kampeni hiyo.
“Watoto ndio kizazi cha baadaye, tukihusishwa mapema katika masuala ya mazingira, tutakuwa walinzi bora wa urithi wetu wa asili,” amesema mwanafunzi huyo.