Arusha. Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wilaya ya Arusha, Dominic Mollel, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi, huku jitihada za kumpata mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Morris Makoi, zikitarajiwa kutua kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Februari 24, 2026, mbele ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, mfanyabiashara Josephine Shirima alidai mbunge huyo na Mollel walimdhulumu mali zake zilizokuwa dukani.
Waziri Mkuu aliwagiza Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, kuhakikisha wahusika waliochukua mali hizo za Josephine wanazirudisha, kisha ashughulikie masuala mengine yaliyokuwa yamesalia.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Machi mosi, 2026, Mkude amesema bado wanaendelea kumshikilia Mollel, huku dalali aliyedaiwa kuchukua mali hizo akidaiwa kutoroka na kutopatikana.
Mkude amesema kwa sasa amechukua hatua kumuomba Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, kupitia kwa Waziri Mkuu, aombe kibali kwa Spika wa Bunge ili aruhusu mbunge huyo kutoa ushirikiano katika suala hilo.
“Nimewasiliana na OCD, amenipa taarifa ya suala hilo. Bado anaendelea kufuatilia. Yule dalali hapatikani tena, ni kama ametoroka, hakutoa ushirikiano na hakazima simu kabisa.
“Mbunge ni vigumu kushirikiana naye moja kwa moja mpaka apate ruhusa kwa Spika wa Bunge. Nimechukua hatua ya kumuomba Mkuu wa Mkoa kupitia kwa Waziri Mkuu ili aombe Spika aruhusu au kumpa nafasi mbunge huyo ya kuja kutoa ushirikiano kwenye jambo hili,” amesema Mkude na kuongeza;
“Kimsingi tunataka mali za mfanyabiashara zirejeshwe kwani ni zaidi ya miaka minne, lakini kama hazipo pia ni jibu na tutachukua hatua nyingine. Dalali alikubali kuja kuonesha mali zilipo na alidai alikuwa njiani, ila sijui nitumie lugha gani, aliogopa au alidanganya kwa sababu alisema anakuja ila hakuwahi kufika,” ameongeza Mkude.
Awali, Februari 25, 2026, Mkude alieleza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia Mollel, huku mbunge huyo akitoa ushirikiano wa kumtafuta dalali aliyedaiwa kuchukua mali za Josephine, aliyekuwa mfanyabiashara wa dukani moja ya stendi ndogo Arusha.
Amesema wamewasiliana na mbunge huyo, ambaye yuko nje ya mkoa wa Arusha, na kuwa amewapa ushirikiano mkubwa wa kumtafuta dalali wa mahakama aliyedaiwa kuchukua mali hizo za mfanyabiashara dukani kwake.
“Bado mali hazijarudishwa, lakini tumewasiliana na mbunge, anakaa nje ya mkoa huu, lakini ametupa ushirikiano mkubwa wa kumtafuta dalali wa Mahakama aliyetumika kwenda kuchukua mali hizi,” amesema Mkude.
“Dalali sasa hivi yuko njiani, anatokea Moshi, ataingia mchana huu. Akiingia, ataenda kuonesha mali ambazo zinasemekana ziko dukani, yule mama Josephine atavitambua kama ni hivyo na viko katika hali gani,” Mkude amesema.
Baada ya hatua hiyo, kesi ya msingi itaendelea dhidi yao, kwani walichukua mali hizo bila kufuata taratibu za kisheria.
“Mollel anashikiliwa mpaka mali hizo zipatikane. Tumetoa muda mpaka mchana huu viwe vimepatikana, vifaa vitakabidhiwa Josephine mbele ya watu na viongozi wa Serikali ili ahakiki kama ndiyo hivyo. Hii haijasimamisha hoja kuisha. lazima kesi ya msingi itakuwepo kwa wote, Mollel na Mbunge,” amesema Mkude.