Dar es Salaam. Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, ameipongeza Tanzania kwa kuunda tume ya kuchunguza matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Akizungumza katika kikao cha 61 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika Geneva, Uswisi, jana Februari 29, 2026, Turk amesema hatua hiyo ni chanya na muhimu katika kuimarisha uwajibikaji na kuhimiza maridhiano.
“Katika maendeleo yanayokaribishwa, Tanzania imeunda tume ya kitaifa kuchunguza ukiukwaji uliotokea wakati wa uchaguzi wa Oktoba,” amesema huku akitoa tathmini ya hali ya haki za binadamu katika maeneo mbalimbali duniani.
Katika hotuba yake, Turk ameeleza kuwa baadhi ya mataifa yanaendelea kuyapa vyombo vya dola sura ya kijeshi katika utekelezaji wa sheria. Akitolea mfano ukanda wa Sahel, amesema watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari wamekuwa wakilengwa, kukamatwa na kuwekwa kizuizini, huku vyombo huru vya habari vikifungiwa na vyama vya siasa kuvunjwa kwa madai ya kukabiliana na misimamo mikali ya vurugu.
Aidha, ameonesha wasiwasi wake kuhusu hali ya hatari ya miaka minne nchini El Salvador, akieleza kuwa matumizi ya kesi za pamoja kwa wingi yanazua maswali kuhusu misingi ya haki.
Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya uhalifu wa kupangwa yanapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia kanuni za haki na taratibu stahiki, akibainisha pia masikitiko yake juu ya taarifa za vifo vingi vya mahabusu.
Kuhusu Ecuador, Turk amesema anaridhishwa kwa kiasi na juhudi zinazofanywa, lakini akaeleza wasiwasi wake kuhusu mamia ya vifo magerezani vinavyotokana na vurugu na magonjwa.
Akizungumzia Marekani, amesema idara za uhamiaji na nyinginezo zimetuhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi wakati wa operesheni dhidi ya wahamiaji na waandamanaji wa amani, hali iliyopelekea baadhi ya watu kupigwa risasi na kuuawa.
Kwa upande wa Guinea, amebainisha kuwa uchaguzi uliofanyika Desemba mwaka jana uliashiria hatua ya kurejea katika utaratibu wa kikatiba, ingawa bado kuna changamoto za ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo kubanwa kwa nafasi ya kiraia, matukio ya utekaji na kuzimwa kwa mawasiliano ya kidijitali.
Hapa nchini, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza Novemba 2025 kuundwa kwa tume maalumu kuchunguza vifo na uharibifu uliotokana na maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Bunge la 13 mjini Dodoma, Rais Samia alitoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao kufuatia vurugu hizo, akisema matukio hayo yalimwathiri kwa kina.
Alieleza kuwa lengo la kuundwa kwa tume hiyo ni kubaini chanzo cha matatizo yaliyojitokeza, huku akisisitiza kuwa ripoti yake itaongoza mchakato wa mazungumzo na juhudi za kurejesha maelewano na amani nchini.
Rais pia aliwataka wananchi waliopoteza mali zao kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho taifa linapitia changamoto.
Tume hiyo imeendelea na majukumu yake, huku muda wa utekelezaji wa kazi zake ukiongezwa kwa siku 42 zaidi.