Kuuawa kwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei katika mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel, kumeiweka Iran njia panda wakati uongozi wa juu wa nchi hiyo ukianza mchakato wa kumtafuta mrithi wake.
Viongozi kadhaa waandamizi waliokuwa karibu na Khamenei pia wameripotiwa kuuawa katika shambulizi hilo, akiwemo mshauri wake mkuu wa usalama, Ali Shamkhani, pamoja na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC), Mohammad Pakpour.
Kuuawa kwa Khamenei, aliyeingia madarakani mwaka 1989, kumeuacha uongozi wa juu wa Iran ukijiandaa kwa uhamisho wa madaraka katika wakati ambao Marekani, dola yenye jeshi lenye nguvu zaidi duniani, imeahidi kuvunja muundo wa utawala ulioanzishwa kufuatia Mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979.
Nani atakuwa Kiongozi Mkuu ajaye wa Iran? Na atachaguliwaje?
Kwa mujibu wa mfumo wa kikatiba wa Iran, mchakato wa kumchagua Kiongozi Mkuu unafanywa na chombo kinachoitwa Assembly of Experts — baraza la wanazuoni wa Kiislamu lililochaguliwa kwa kura na wananchi.
Kiongozi mkuu wa Iran huchaguliwa na Baraza la Wataalamu, ambalo linaundwa na wajumbe 88 ambao ni viongozi wa kidini waliochaguliwa na umma na wajumbe hao huchaguliwa kila baada ya miaka minane.”
Wagombea wanaowania ujumbe wa baraza hilo lazima kwanza wachunguzwe na kupitishwa na Guardian Council, chombo chenye mamlaka makubwa ya usimamizi ambacho baadhi ya wajumbe wake huteuliwa na kiongozi mkuu mwenyewe.
Iwapo nafasi ya kiongozi mkuu itakuwa wazi kutokana na kifo au kujiuzulu baraza la wataalamu hukutana kumchagua mrithi. Wingi wa kura (asilimia 50 na zaidi) unatosha kumteua kiongozi mkuu mpya.
Kwa mujibu wa Katiba ya Iran, mgombea lazima awe mwanazuoni mwandamizi wa sheria za Kiislamu (fiqhi) katika madhehebu ya Shia, mwenye uelewa wa kina wa fiqhi ya Kiislamu, pamoja na sifa za busara ya kisiasa, ujasiri, na uwezo wa kiuongozi na kiutawala.
Kifungu cha 111 cha katiba ya Iran kinaaelekeza kwamba baraza la muda litashughulikia majukumu hadi kiongozi mkuu mpya atakapochaguliwa.
Baraza hilo litajumuisha Rais Masoud Pezeshkian, Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu, Gholam-Hossein Mohseni-Ejei, na kiongozi wa dini kutoka Baraza la Walezi (Guardian Council), kulingana na vyombo vya habari vya Iran.
Ayatollah Alireza Arafi kutoka Baraza la Walezi, mwenye umri wa miaka 67, ameteuliwa Jumapili kuwa mjumbe wa baraza la muda la watu watatu.
Watatawala wa nchi hiyo hadi bunge litakapochagua kiongozi mkuu mpya.
Kiongozi wa usalama wa Iran na mtu wa karibu na marehemu Khamenei, Ali Larijani, amesema, leo Jumapili Machi mosi, 2026 kuwa mchakato wa mpito umeanza.
Luciano Zaccara, profesa mshirika wa utafiti kuhusu siasa za Ghuba katika Chuo Kikuu cha Qatar, ameliambia Al Jazeera kwamba mfumo wa kisiasa wa Iran umejiandaa kwa hali ya sasa, ukijua kuwa mauaji ya Khamenei yalikuwa na uwezekano halisi.
“Trump anataka kupata
dili bora zaidi inavyowezekana, lakini njia anayoitumia kupata dili hilo ni kuharibu au kuangamiza kadri anavyoweza,” Zaccara amesema. “Hii ndiyo njia ya kuweka masharti, si kufanya mazungumzo yoyote. Trump anataka utawala kujisalimisha, si mabadiliko.”
Ili kuepuka pengo la madaraka, marehemu Khamenei aliweka mbadala kwa kila ofisa aliyefutwa katika miezi michache iliyopita, na kuhakikisha kuwepo kwa muundo fulani, Zaccara ameliambia Al Jazeera.
“Miundo inabaki, mstari wa madaraka na mstari wa amri unabaki palepale,” amesema.
Mtoto wa pili wa Khamenei, Mojtaba Khamenei ni miongoni mwa wagombea wakuu wanaotajwa kumrithi baba yake kama kiongozi mkuu ajaye.
Anajulikana kuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa watendaji wa serikali na Jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislam (IRGC), chombo chenye nguvu zaidi cha kijeshi nchini humo.
Hata hivyo, ukoo wa Khamenei pia ni miongoni mwa vikwazo vikubwa anavyokumbana navyo. Inaripotiwa kuwa hapo awali alipingana na urithishwaji wa uongozi kutoka kwa baba kwenda kwa mwana. Mtindo huo haukubaliki sana nchini Iran, hasa baada ya utawala wa kifalme ulioungwa mkono na Marekani wa Mohammad Reza Pahlavi kupinduliwa mwaka 1979.
Arafi, mwenye umri wa miaka 67, ni mwanazuoni wa dini mwenye ushawishi mkubwa ndani ya taasisi za kidini za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, lakini si mwanasiasa anayekubalika kwa upana.
Anahudumu kama naibu mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu (Assembly of Experts), chombo kinachosimamia mchakato wa kumchagua kiongozi mkuu, na pia amewahi kuwa mjumbe wa Guardian Council, baraza linalochuja wagombea wa uchaguzi na kupitia sheria zinazopitishwa na bunge.
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran viliripoti Jumapili kuwa Arafi ameteuliwa kuwa mwanasheria mjumbe wa Baraza la Uongozi la Iran, chombo chenye jukumu la kutekeleza majukumu ya kiongozi mkuu hadi Baraza la Wataalamu litakapomchagua kiongozi mpya.
Pia, ni kiongozi wa swala ya Ijumaa katika mji wa Qom, kitovu kikuu cha kidini nchini Iran na anaongoza mfumo wa vyuo vya kidini nchini humo, akisimamia elimu ya makleri kote nchini.
Mohammad Mehdi Mirbagheri
Mirbagheri ni mwanazuoni wa dini mwenye msimamo mkali wa kihafidhina ndani ya taasisi za utawala na ni mjumbe wa Assembly of Experts.
Anajulikana kwa mtazamo wake mkali unaoyakosoa mataifa ya Magharibi, na kwa sasa anaongoza Chuo cha Sayansi za Kiislamu katika mji wa kaskazini wa Qom.
Gholam-Hossein Mohseni-Ejei
Mohseni-Ejei ni mwanazuoni mwandamizi wa dini nchini Iran na kwa sasa anaongoza mhimili wa mahakama wa Jamhuri ya Kiislamu. Aliteuliwa kushika wadhifa huo Julai 2021 na marehemu Khamenei.
Aliwahi kuwa waziri wa ujasusi kuanzia mwaka 2005 hadi 2009, na baadaye akahudumu kama mwendesha mashtaka mkuu na naibu mkuu wa mahakama. Anachukuliwa kuwa mmoja wa watu wenye msimamo mkali anayelingana na mrengo wa kihafidhina wa utawala.
Khomeini, mwenye umri wa miaka 54, ni miongoni mwa majina yanayotajwa sana katika mijadala ya urithi wa uongozi kwa nafasi ya kiongozi mkuu ajaye.
Yeye ni mjukuu wa Ruhollah Khomeini, mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na pia ni msimamizi wa kaburi la babu yake lililoko mjini Tehran.
Ingawa hajawahi kushika wadhifa wa umma, Khomeini anachukuliwa kama kiongozi mwenye mwelekeo wa mageuzi anayejulikana kwa misimamo ya wastani katika masuala ya kijamii na sera za umma. Alijaribu kugombea uanachama wa Assembly of Experts mwaka 2016, lakini baraza la uchunguzi wa wagombea lilimwondoa katika mchakato huo.