Rais Mwinyi ahimiza amani na mshikamano nchini

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amewataka Watanzania kudumisha amani, utulivu na mshikamano katika taifa, kwani bila amani hakuna mafanikio yanayoweza kufikiwa.

Rais Mwinyi amesema hayo leo Machi mosi, 2026, katika mashindano ya kimataifa ya Quran yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Al-Hikma, yakikutanisha washiriki 26 kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya Afrika.

“Niitake jamii kudumisha maadili, umoja na mshikamano, na kushikana kupambana na mmomonyoko wa maadili kwa kutumia Quran. Kwa kufanya hivyo, watakuwa wameitendea haki kitabu kitakatifu cha Quran.

“Pia muendelee kutenda mambo mema ikiwa ni kusoma Quran, mdumishe amani, utulivu na mshikamano katika taifa kwani bila amani hatuwezi kufikia mafanikio yeyote,” amesema Rais Mwinyi, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye tukio hilo.

Dk Mwinyi, Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, amesema mashindano hayo yamekuwa kitambulisho chema cha taifa kwa kuvutia washiriki kutoka mataifa mbalimbali.

Ili mashindano hayo yaendelee kufanyika kila mwaka, Rais ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuiunga mkono taasisi hiyo ili raia mbalimbali waanze kunufaika nayo na kuendeleza vijana wazalendo kwa taifa.

“Nitoe wito kwa kila Mwislamu kufahamu kuwa ushindi sio kupata zawadi bali ni kuishi katika mafundisho ya Mtume,” amesema.

Awali, Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa, amesema taasisi ya Al-Hikma imeendelea kuiheshimisha taifa kwa kuendelea kujaza watu kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo ni heshima kwa Tanzania na Waislamu kwa ujumla.

 “Tuna jumla ya washiriki 26 kutoka mabara mbalimbali, niendelee kuipongeza taasisi hii kwa uratibu mzuri; hakika uratibu wenu ni mzuri na una mvuto,” amesema.

Kwa upande wake, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubar Zubeir, amelitaja tukio hilo la mashindano ya Quran kama moja ya matukio yanayoipa sifa Tanzania nje ya nchi, akidokeza miongoni mwa sifa hizo ni kutokana na tukio hilo.

Sheikh Abubakar amewataka Waislamu kutumia tukio hilo kama fursa ya kumuomba Mungu kuendelea kuwapatia baraka na kudumisha amani na utulivu uliopo hapa nchini.

“Tumuombe sana Mungu atupe heri za Ramadhani katika nchi yetu,” amesema.

Mshindi wa mashindano hayo, aliyeshirikisha washiriki 26, ni kijana wa miaka 13 raia wa Uganda, aliyepatiwa Sh30 milioni kwa uwezo wake wa kuhifadhi juzuu 30, na pia alichaguliwa kuwa mshiriki mdogo zaidi.

Aliyeshika nafasi ya pili ni mshiriki kutoka Canada aliyepatiwa Sh20 milioni, nafasi ya tatu raia wa Sweden Sh12.5 milioni, mshindi wa nne kutoka Afrika Sh10 milioni, na mshindi wa tano kutoka New Zealand Sh7.5 milioni.

Taasisi ya Al-Hikma pia ilitangaza kuwalipia mahari vijana 130 ambao hawajaoa, sharti likiwa mwanamke mwenye uhitaji wa kuolewa awepo na mwenza kuchukua fomu kuanza mchakato.

Mratibu wa Taasisi amesema, “Mwaka huu tuna mpango wa kuwaozesha vijana 130.

“Mwaka jana tuliozesha vijana 370. Sharti lingine, mwanaume awe na kibarua cha kumuingia kipato, kuongeza mke bila kufuata masharti haya haitakuwa na sifa ya kulipiwa mahari.

Tukio la kipekee lilitokea nusu saa baada ya kuanza mashindano pale jukwaa kuu walilokaa majaji likivunjika kutokana na mvua kubwa, na kusababisha tukio kusimama kwa saa moja.

Mashindano yaliyoanza saa 1:00 asubuhi Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku mvua ikiendelea kunyesha saa 1:26 jukwaa lilivunjika, na mshiriki wa kwanza, Muhamed Mustapha, aliyefungua dimba kuonesha ujuzi wake wa kuhifadhi juzuu, kukatisha zoezi hilo kwa saa moja.

Mbali na jukwaa kuu, hata wananchi waliokuwa majukwaani walilazimika kuhama kutokana na mvua, iliyokuwa ikiaathiri maeneo walipo, kuanzia saa 1:26 hadi 2:30 asubuhi, ambapo mashindano yaliendelea kwa waratibu kubadili jukwaa.