Shadrack Nsajigwa apania Tanzania Prisons

KOCHA mpya wa maafande wa TZ Prisons, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ amesema malengo makubwa aliyonayo kwa timu hiyo ni kuhakikisha timu hiyo inajinasua na janga la kushuka daraja, licha ya ushindani mkubwa uliopo msimu huu katika mechi za Ligi Kuu Bara.

Nsajigwa aliyeachana na Transit Camp inayoshiriki Ligi ya Championship msimu huu, alitambulishwa rasmi kukiongoza kikosi hicho tangu Februari 27, 2026 baada ya aliyekuwa kocha mkuu wa maafande hao, Mkenya Zedekiah ‘Zico’ Otieno kuondoka.

Akizungumza na Mwanaspoti, Nsajigwa amesema ni heshima kubwa kupewa nafasi ya kukifundisha kikosi hicho, ingawa ili kwa pamoja wafikie malengo ya kukinusuru na janga la kushuka daraja, wanapaswa kuongeza mshikamano kikosini humo.

“Kwa nafasi tuliyopo sio nzuri sana kwa sababu tunahitaji kuongeza juhudi zaidi, jambo linalotupa matumaini makubwa ni kutopishana kwa pointi nyingi na washindani wetu, hivyo, tutapambana ili tutoke huku chini tulipo,” amesema Nsajigwa.

Katika miaka ya mwanzoni ya taaluma yake, Nsajigwa aliwahi kuichezea Prisons ya Mbeya, kisha kujiunga na Yanga aliyoitumikia kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2012 akiwa pia nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Taifa Stars.

Kwa msimu huu wa 2025-2026, Nsajigwa ameiacha Transit Camp inayoshiriki Ligi ya Championship ikishika nafasi ya nne na pointi 37, baada ya kucheza mechi 19, ikishinda 11, sare minne na kupoteza pia minne, ikifunga mabao 26 na kuruhusu 17.

Kwa upande wa Zedekiah aliyejiunga na Prisons Julai 24, 2025, kwa msimu wa 2025-2026, ameiongoza timu hiyo katika mechi 14, za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo ameshinda tatu, sare tatu na kupoteza minane, ikifunga mabao manane na kuruhusu 16.

Katika mechi hizo 14, Otieno ameiacha Prisons ikiwa nafasi ya 14 na pointi zake 12, huku Mkenya huyo akizifundisha pia, Gor Mahia, Sony Sugar, Posta Rangers na KCB FC zote za Kenya na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars.

Kibarua cha kwanza cha Nsajigwa, kitakuwa mechi ya Ligi Kuu nyumbani dhidi ya Azam FC, itakayopigwa Machi 5, huku kikosi hicho kikiwa na kumbukumbu mbaya ya kuchapwa mabao 4-0, mara ya mwisho zilipokutana, Machi 6, 2025.