Usikubali kupoteza mwelekeo, elekeza moyo kwa Yesu

Bwana Yesu asifiwe, karibu katika tafakari ya neno la Mungu. Ninaitwa Mwalimu Erasto Maliganya kutoka mkoani Mbeya. Somo la leo ni mwendelezo wa somo lililopita ambalo lilikuwa linasema; ‘Kwa neno lako nitazishusha nyavu’.

Katika injili ya Mathayo 9:20–22 tunaona habari ya mwanamke aliyekuwa anatokwa na damu kwa muda wa miaka kumi na miwili.

Hali yake haikuwa tu ya kimwili, bali pia ya kihisia na kijamii.

Kwa mujibu wa sheria za wakati ule, alikuwa ametengwa na jamii. Aliishi maisha ya maumivu, aibu na kukataliwa. Lakini siku moja aliposikia kwamba Yesu anapita, jambo fulani lilizaliwa ndani ya moyo wake.

Alisema moyoni mwake: “Nikigusa tu upindo wa vazi lake, nitapona.” Hii haikuwa kauli ya kawaida; ilikuwa ni kauli ya imani. Na alipochukua hatua ya kusogea na kugusa vazi la Yesu, mara moja damu ikakoma. Yesu akageuka na kumwambia, “Jipe moyo, binti; imani yako imekuponya.”

Safari ya muujiza wake ilianzia moyoni. Kabla hajamgusa Yesu kwa mkono, tayari alikuwa amemgusa kwa imani. Hii inatufundisha kwamba mwelekeo wa ndani huzaa matokeo ya nje.

Kulikuwa na umati mkubwa ukimsonga Yesu, lakini mwanamke huyu hakuruhusu msongamano kumzuia. Alikuwa na lengo moja tu, kumfikia Yesu. Hakujali watu watasema nini. Hakujali mazingira. Alijali muujiza wake. Penye nia pana njia.

Ukiweka shabaha yako kwa Kristo, hutazuiliwa na vikwazo vya nje. Wakati unahitaji mabadiliko katika maisha yako, macho yako lazima yawe kwa Yesu, si kwa kelele za watu. Usipoteze mwelekeo kwa sababu ya mazingira yanayokuzunguka.

2. Maumivu hayakumfanya apoteze mwelekeo

Miaka kumi na miwili ni muda mrefu sana. Miaka 12 ya mateso. Miaka 12 ya aibu. Miaka 12 ya kukata tamaa. Watu wengi wangeacha kuamini. Wengine wangezoea hali yao. Lakini mwanamke huyu hakuruhusu muda mrefu wa mapambano kuzalisha imani fupi.

Kuchelewa si kukataliwa. Mara nyingi Mungu hachelewi, bali huandaa wakati sahihi. Maumivu yanaweza kukufanya upoteze dira kama hutakuwa makini. Watu wengi wameacha ndoto zao, biashara zao na hata imani yao kwa sababu ya maumivu ya muda mrefu. Lakini mwanamke huyu hakutaka maumivu yauue muujiza wake.

Unapopita katika kipindi kigumu, muombe Mungu mwelekeo wako usiharibiwe na maumivu. Usiruhusu historia yako kuwa kizuizi cha kesho yako.

3. Sio wote waliogusa walipokea

Watu wengi walimsukuma Yesu siku ile. Wengi walimgusa kimwili, lakini hawakupokea chochote. Tofauti ya mwanamke huyu ilikuwa mguso wa imani. Alimgusa Yesu kuanzia moyoni.

Unaweza kuwa kanisani kila Jumapili. Unaweza kusikia Neno mara kwa mara. Unaweza kuwa karibu na waumini. Lakini kama moyo wako umetawanyika, unaweza kukosa wakati wako wa neema kutoka kwa Bwana.

Mguso wenye mwelekeo na imani humvutia Yesu. Ndiyo maana Yesu alisimama na kumtambua. Imani yake ilimtofautisha katikati ya umati wa watu wengi.

4. Vitu vinavyoweza kukufanya upoteze mwelekeo

Kwanza ni kukata tamaa. Watu wengi wamekata tamaa kwa sababu ya hali zao na hawataki tena kusikia kuhusu Mungu. Pili ni maneno ya watu. Kuna waliodhoofishwa na maneno mabaya na wakapoteza dira ya maisha yao. Tatu ni kuchelewa kwa majibu. Wengine wamechoka kusubiri na wakaamua kuacha njia. Nne ni maumivu ya zamani. Kumbukumbu za nyuma zinaweza kuharibu maono ya mbele kama hazijashughulikiwa vizuri.

Lakini wakati Mungu anataka kukutoa kwenye maumivu, hakikisha macho yako yanabaki kwa Kristo. Usiruhusu imani yako kuwa dhaifu. jiimarishe kwa maombi, Neno na subira.

Mwanamke huyu hakuruhusu umati, muda wala maumivu kumpotezea mwelekeo. Alijua anachotaka, akaamini, akachukua hatua, na akapokea muujiza wake.

Pia wewe leo, usipoteze mwelekeo. Elekeza moyo wako kwa Yesu. Shikilia imani yako hata kama umechelewa kwa miaka mingi. Kwa sababu mguso mmoja wa imani, ukiwa na mwelekeo sahihi, unaweza kubadilisha maisha yako milele.

Ndiyo maana katika injili ya Mathayo 9:22, Yesu anasema: “Jipe moyo, binti; imani yako imekuponya.” Maneno haya yanatukumbusha kuwa uponyaji, ushindi na mabadiliko huanzia moyoni. Imani iliyo na mwelekeo sahihi humfanya Mungu atusimamie katikati ya umati na kutenda muujiza binafsi katika maisha yetu.

Mwalimu Erasto Maliganya anapatikana Kanisa la AICT Forest Mbeya. Kwa maombi na ushauri 0755371354