Hanang‘. Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, amewasihi wasaidizi wa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kuiga namna anavyotatua changamoto na kero za wananchi kwa kusikiliza na kuzitatua.
Sumaye ameyasema hayo leo Jumapili Machi Mosi, 2026, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji mdogo wa Katesh, wilayani Hanang’ mkoani Manyara.
Amesema anavutiwa na namna Waziri Mkuu Mwigulu anavyowatumikia wananchi kwa kuwqsikiliza kero, malalamiko na changamoto zao na kisha kuzitatua.
“Naomba wasaidizi wako kuanzia mawaziri, manaibu, wakuu wa mikoa na wilaya waige mfano wako wa kusikiliza changamoto za wananchi wetu na kuzipatia ufumbuzi,” amesema Sumaye.
Amesema kila kiongozi akitimiza wajibu wake, wananchi watakuwa wanafurahia maisha yao na kufanya kazi zao za kujenga uchumi kuliko kukimbizana na migogoro.
“Miaka iliyopita tulikuwa tunatambua kuwa serikali ya mwananchi mwisho wake ni kwa mkuu wa wilaya au halmashauri, ili atu akiwa na shida anatatuliwa ila akienda mbali na hapo zaidi ni changamoto,” amesema Sumaye.
Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Spika, Daniel Sillo amesema;
“Waziri Mkuu Dk Mwigulu unatafsiri kwa vitendo usaidizi wako kwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwatumikia wananchi na kutatua kero zao,” amesema Sillo.
Mbunge wa Hanang’, Asia Halmashauri pamoja na kuipongeza serikali kwa kazi inazofanya, ameishukuru kwa kuwapatia fedha za miradi ya maendeleo. Amesema baadhi ya changamoto zinazolikabili jimbo hilo tayari zimeanza kutatuliwa.
Hata hivyo, amesema kero kubwa ya barabara bado haijapatiwa ufumbuzi.
Mbunge Halamga amesema barabara ya lami ya kipande cha kilometa 80 kutoka eneo la Dareda hadi kata ya Gehandu mpakani na mkoa wa Singida imeharibika.
Ametaja pia barabara ya lami kutoka Gehandu hadi hospitali ya rufaa ya Haydom na Nagwa hadi Kuondoa mkoani Dodoma zinapaswa kujengwa kwa kiwango cha lami.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Dk Mwigulu amesema hawana muda wa kulumbana na baadhi ya watu wanaotegemea kufugwa na baadhi ya mataifa ya nje kwa kisingizio cha kutafutwa na nchi yao.
“Mtu anafugwa yeye, mke wake na watoto kisa uvivu wa kufanya kazi anatunga vitu ili alipwe ila sisi tunaachana na hayo tukipambana na miradi ya maendeleo ya elimu, afya, maji na miundombinu,” amesema Dk Mwigulu.
Hata hivyo, amemuagiza Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya kuhakikisha barabara za lami zilizoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi wa CCM zinajengwa.
“Mkoa wa Manyara ni miongoni mwa mikoa ambayo haina lami zaidi ya barabara mbili kupitiwa na lami, hivyo barabara hizo zijengwe kwa kiwango cha lami, hiyo ya Gehandu isiwekwe viraka” amesema Waziri Mwigulu.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa eneo hilo wametoa kero zao ikiwemo bidhaa zao kukamatwa na askari mgambo na kutupwa jambo ambapo Dk Mwigulu amelikemea.