BONDIA NAMBA MOJA TANZANIA IBRAHIM CLASS AIANDIKIA BARUA WBC KUPINGA DHULUMA ALIYOFANYIWA THAILAND

::::::

 

Bondia namba moja kutoka Tanzania katika uzani wa ‘Super feather’, Ibrahim Class amepinga matokeo ya pambano lake alilocheza jana Februari 28 mwaka huu nchini Thailand.

Ibrahim Class alipigana na Mthailand Kritiphak Duangnut katika pambano la raundi 10 la kuwania mkanda wa WBC silver International ambapo majaji walitangaza matokeo ya sare.

Baada ya matokeo hayo Class ameonesha kusikitishwa na dhuluma aliyofanyiwa na majaji wawili raia wa Thailand ambao walionesha dhahiri dhamira ya kumbeba Mthailand mwenzao ambaye alipigwa raundi zote na Mtanzania huyo.

“Nimempiga jamaa raundi zote 

Mwisho wa siku wametoa sare

Tumeambiwa tuandike barua ya malalamiko WBC promota kasema tuandike itumwe kule WBC waliangalie pambano watende haki kwasababu majaji wawili wa hapa wametoa sare jaji mgeni ambaye ndio sio wa hapa kanipa nimeshinda sasa imekuaje wawili watoe sare wa hapahapa wamembeba ndugu yao alafu huyu mmoja ndio kanipa kwahiyo tunasikilizia majibu kwanza WBC,” amesema bondia huyo namba moja kutoka Tanzania.

Jaji namba moja Pongpan Rattanasutorn alimpa Ibrahim Class alama 95 na Duangnut alama 95

Jaji namba mbili Parin Hantabool pia alimpa Ibrahim Class alama 95 na Duangnut alama 95 lakini jaji namba tatu Joseph Gwilt alimpa Ibrahim Class alama 97 na Duangnut alama 93 na mwisho wa pambano matokeo yakatangazwa sare.

Hivyo basi uongozi wa bondia huyo Mtanzania upo kwenye mchakato wa kusubiri majibu ya WBC ambao wakishapokea barua hiyo watapitia pambano lote kisha na kutoa mrejesho wa matokeo.

Mungu akubariki Ibrahim Class katika hili uweze kufanikiwa na kuweza kupata haki yako.