Dar es Salaam. Kama wewe sio mwenyeji wa Mkoa wa Dar es Salaam na unataka kununua ardhi, magari au kuchukua mkopo wa fedha, chukua tahadhari, kwani Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametaja maeneo hayo kuongoza kwa matukio ya utapeli.
Chalamila amesema waathirika wakubwa wa migogoro hiyo ya ardhi mkoani humo ni wajane, warithi wa mirathi na watoto.
Kwa upande wa magari, Chalamila amesema wapo watu huagiza magari kupitia kwa wauzaji walio na maduka ya magari, kisha hulipa fedha kabisa, lakini huishia kutapeliwa na kuzungushwa kwa kauli kwamba magari hayo yapo ila hayajawasili bandarini.
Kuhusu mikopo, Chalamila amesema wamebaini kuna watu husainishwa mikataba ya kukopeshwa na, wakati huohuo, husainishwa mkataba wa kuuziwa nyumba au mali zake siku inayofuata.
Kufuatia changamoto hizo, Chalamila ametoa wiki moja kuanzia leo, Jumatatu, Machi 2, hadi Machi 7, 2026, kwa wananchi wote waliodhulumiwa na wenye nyaraka za kuthibitisha madai hayo, kuwasilisha ofisini kwake.
Amesema baada ya tarehe hiyo kupita, ataanza ziara ya kufuatilia ukweli wa mambo yote yanayolalamikiwa.
Mkuu huyo wa mkoa amesema hayo leo, Jumatatu, Machi 2, 2026, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ziara aliyoifanya hivi karibuni mkoani humo, amebaini changamoto hizo na akiahidi Machi 9, 2026, atafanya ziara nyingine katika Wilaya ya Ilala.
Chalamila amesema wamebaini kuwepo kwa kiwango kikubwa cha utapeli wa ardhi unaowaathiri wananchi, huku changamoto hiyo ikichangiwa mara nyingine na baadhi ya watumishi wa umma wanaoshirikiana na matapeli.
Amesema baada ya kukamilisha ziara yake ya kusikiliza na kutatua kero, watu kadhaa waliokuwa wamedhulumu ardhi kwa hiari yao wameanza kuirejesha, na hadi sasa jumla ya maeneo 19 ya ardhi yamerejeshwa kwa wahusika halali.
“Tuna maeneo 19 ambayo yamerejeshwa, na wale wote waliokuwa wamepora ardhi hiyo tumekubaliana kuwasamehe kwa kuwa wameirejesha kwa wahusika. Kundi kubwa lililoathirika ni wajane, wafiwa na watoto waliopoteza wazazi wao,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Akizungumzia maeneo yanayofanyiwa biashara ya uuzaji wa magari maarufu ‘showroom’, amesema wamebaini pia kuwapo kwa utapeli mkubwa, ambapo wananchi hulipia magari lakini baadaye hudhulumiwa kwa kuelezwa kuwa bado yapo bandarini.
“Ukifuatilia, unagundua kuwa ama hayapo bandarini au kama yapo, hayajalipiwa. Huu ni utapeli mkubwa unaowaumiza wananchi,” amesema.
Amesema wananchi kutoka mikoa mbalimbali wamemtafuta wakilalamikia watu wanaojinasibu kuwa wafanyabiashara wa magari, lakini baada ya kupokea fedha zao huwatapeli.
Ametoa mfano wa baadhi ya wananchi waliodhulumiwa hadi Sh100 milioni wakitaka kuagiza magari, akieleza kuwa hilo ni tatizo linalowaumiza zaidi wananchi wa kipato cha chini.
Kuhusu mikopo, amesema wamebaini uwepo wa mikataba yenye utata, ambapo mtu husainishwa mkataba mmoja na, wakati huohuo, husainishwa mkataba mwingine wa kuuza ardhi yake.
“Mtu anakopeshwa na kuwekewa masharti kwamba ifikapo kesho saa tisa, ardhi yake, nyumba au dhamana yoyote aliyoweka inauzwa. Hapa tumegundua kuna unyang’anyi pia mkubwa,” amesema.
Atoa wiki moja kwa wanaodaiwa kupora ardhi
Chalamila amesema wana orodha ya watu waliothibitishwa kujihusisha na uporaji wa ardhi katika Mkoa wa Dar es Salaam.
“Tuna orodha ambayo tumedhibitisha kuwa ni wanyang’anyi wakubwa wa ardhi katika mkoa wa Dar es Salaam. Nawapa wiki moja kurejesha hati za ardhi walizokalia ambazo si zao. Tumefanya uchunguzi wa kina na wa kutosha,” amesema.
Ameongeza kuwa tayari wameanza mchakato wa awali wa kuhakiki nyaraka mbalimbali, na kwamba atatoa taarifa kuhusu matukio yoyote ya unyang’anyi wa ardhi yatakayoendelea kujitokeza ndani ya mkoa huo.
Ametaja maeneo yenye changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi kuwa ni Ilala, Kigamboni na Kinondoni, akisisitiza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amemtuma kuhakikisha kero zinazowakabili wananchi zinapatiwa ufumbuzi.
Chalamila amesema kuanzia Machi 2, 2026, atakuwa ofisini kwake akiwakaribisha wananchi wote waliodhulumiwa ardhi kufika na kuwasilisha nyaraka zao kwa ajili ya uhakiki, zoezi litakalodumu kwa wiki moja.
“Machi 9, 2026, nitaanza ziara ya mguu kwa mguu kufuatilia maeneo ambayo wananchi watakuwa wamenithibitishia kuwa wameporwa,” amesema.
Ameongeza kuwa katika ziara hiyo ataanzia eneo la Salasala, kwa lengo la kushughulikia suala la mtu anayeonekana kuwa na ushawishi kijamii, lakini kisheria hana uzito huo.
“Katika awamu hii, kwa kuwa haki imekuwa ikitajwa sana na Watanzania, sisi kama viongozi tumejipima. Tukisimamia haki ipasavyo, matokeo yake yanakuwa mazuri,” amesema.
Wito wa mageuzi ya kimfumo
Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Magabilo Masambu, amesema changamoto zinazoikumba sekta ya ardhi katika Jiji la Dar es Salaam haziwezi kumalizika kwa operesheni za kushtukiza pekee, bali zinahitaji mabadiliko ya kimfumo yatakayorejesha nidhamu, uwazi na uaminifu katika usimamizi wa rasilimali hiyo.
Amesema maeneo mengi yameendelea kujengwa kabla ya kupimwa rasmi, hali inayosababisha migogoro ya mipaka, uuzaji wa viwanja zaidi ya mara moja na ucheleweshaji wa utoaji wa hati.
“Suluhisho la kwanza ni kupanga mji kabla haujakua. Serikali inapaswa kupima na kutenga mapema maeneo ya makazi, biashara na huduma za jamii ili kuondoa mianya ya ujenzi holela,” amesema.