Kliniki ya ardhi kutatua changamoto za ardhi kwa wanawake

Dodoma. Serikali imeanzisha kliniki maalumu ya ardhi kwa lengo la kuwasaidia wanawake kutatua changamoto za umiliki wa ardhi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika Machi 8 mwaka huu.

Akizungumza leo Jumatatu Machi 2, 2026 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Anthony Sanga amesema kliniki hiyo imeanza rasmi leo na inalenga kuwahudumia wananchi, hususan wanawake ili kupata suluhisho la kero  mbalimbali zinazohusiana na umiliki na matumizi ya ardhi.

Amesema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wanawake wanapata haki ya kumiliki ardhi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi.

“Lengo letu ni kuongeza kiwango cha umiliki wa ardhi kwa wanawake kutoka asilimia 28 ya sasa, ili kuwapa fursa kubwa zaidi ya kushiriki katika maendeleo na kujitegemea kiuchumi,” amesema Sanga.

Amesema wanawake wengi hukumbana na changamoto mbalimbali, hususan katika masuala ya mirathi na umiliki wa ardhi, hali inayosababisha baadhi yao kunyimwa haki zao za kisheria.

Kutokana na hali hiyo, amesema wizara kupitia kampeni ya Samia Ardhi Kliniki, imejipanga kutoa huduma za ushauri wa kisheria, utatuzi wa migogoro ya ardhi pamoja na utoaji wa hati miliki kwa wananchi wanaokidhi vigezo.

Kwa upande wake, Mthamini Mkuu wa Serikali katika wizara hiyo, Eveline Mgasha amesema kliniki hiyo inaendeshwa kwa kushirikiana na ofisi za ardhi za mikoa yote nchini ili kuwafikia wanawake wengi zaidi na kurahisisha upatikanaji wa huduma.

Amesema tayari zaidi ya wananchi 160 wamejitokeza kuwasilisha changamoto zao jijini Dodoma, huku maombi 15 ya hati miliki yakipokelewa. Kati ya maombi hayo, hati 10 tayari zimetolewa.

“Zoezi hili linaendelea hadi Machi 7, mwaka huu. Linalenga kuwahudumia wanawake wenye changamoto za ardhi pamoja na kutoa elimu kuhusu sheria za ardhi, uthamini wa mali kwa ajili ya fidia, upimaji wa viwanja na upangaji wa miji,” amesema Mgasha.

Amewahimiza wanawake wa Mkoa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizo zinazotolewa na wataalamu wa wizara, akisisitiza kuwa upatikanaji wa hati miliki ni msingi wa usalama wa kiuchumi na kijamii kwa mwanamke.

Baadhi ya wanawake wakazi wa Dodoma wameipongeza Serikali kwa kuanzisha huduma hiyo, wakisema imewapa fursa ya kupata haki zao na kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili kwa muda mrefu.

Mkazi wa Miuji, Getrude Laurent amesema hatua hiyo itawasaidia wanawake wengi waliokuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu sheria na taratibu za umiliki wa ardhi.

“Wanawake wengi tulikosa taarifa sahihi au tulikuwa na hofu ya kufuatilia haki zetu. Kupitia kliniki hii tumepata elimu na msaada wa moja kwa moja kutoka kwa wataalamu,” amesema.

Naye mkazi mwingine wa Dodoma, Zena Hamisi, amesema huduma hiyo imeleta matumaini mapya kwa wanawake waliokuwa wananyimwa haki ya kumiliki ardhi katika familia zao.

“Tunaishukuru Serikali kwa kusogeza huduma karibu nasi. Mwanamke anapomiliki ardhi anakuwa na uhakika wa usalama wa maisha yake na wa familia yake,” amesema.