MADIWANI BIHARAMULO WAPITISHA BAJETI YA BILIONI 54.9

……..

BIHARAMULO 

BARAZA la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera limepitisha mapendekezo ya mpango na bajeti ya mwaka 2026/27 kiasi cha shilingi 54,978,707,300 kwa lengo la kuchochea maendeleo na ustawi wa wananchi wake.

Akiwasilisha bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Innocent Mkandara, Mweka hazina wa halmashauri ya Biharamulo, Said Lue, amesema mapendekezo hayo yamezingatia hali halisi ya mahitaji ya jamii katika kuchochea maendeleo na kuinua uchumi wa wananchi.

Fedha hizo zinatarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo fedha kutoka serikali kuu na wafadhili kiasi cha Tsh. 49,575,310,100 pamoja na mapato ya ndani kiasi cha Tsh. 5,403,397,200.

Katika bajeti hiyo, mambo mbalimbali yanakusudiwa kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuboreshwa na kuimarishwa utoaji wa huduma za kijamii, kiuchumi na kiutawala ili kuhakikisha wananchi wa wilaya hiyo wanakuwa na maisha bora.

Kadhalika itasaidia kuimarisha huduma za afya ikiwemo ukamirishaji wa majengo ya kutolea huduma, vitendea kazi na uhakika wa dawa za binadamu na wanyama.

Hata hivyo, suala la maambukizi ya virus vya ukimwi(VVU) limepewa kipaumbele kwa kuweka mikakati ya kushusha kutoka aslimia 0.7 hadi kufikia 0.5 kwa kuhakikisha upimaji unafanyika katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Lue amesema bajeti hiyo pia imeweka mazingira rafiki na wezeshi kwa uwekezaji wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na kuimarisha huduma za ugani, uratibu, ufuatiliaji, tathimini na kuongeza tija kwenye uzalishaji wa sekta hiyo.

Vile vile bajeti hiyo imeangazia suala zima la mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu.

Kutokana na hali hiyo, Madiwani hao wakiongozwa na mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Apornary Mugarula, wamejadili na kupitisha kwa kauli moja makadirio ya makusanyo na matumizi ya kiasi cha Bilioni 54.9 huku wakisisitiza nidhamu katika matumizi ya fedha hizo.