Mapinduzi ya Kahawa Mbinga Yawanufaisha Wakulima, Wawapongeza Wadau huku Wakiahidi Uzalishaji zaidi.

 Wakulima wa zao la kahawa wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma wameonyesha matumaini makubwa na jitihada pamoja na mikakati ya uboreshaji wa kilimo cha zao hilo wilayani humo huku wakiwashukuru wadau mbalimbali likiwemo serikali na shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) kwa jitihada zake hususani kwenye utoaji wa mafunzo ya mbinu bora za kilimo cha zao hilo.

Jitihida za shirika hilo zimewafikia wakulima wadogo wapatao 2,000 kupitia vikundi 65 na vyama vya Ushirika wa Msingi (AMCOS) 10 ambapo wamepatiwa mafunzo ya mbinu bora za kilimo cha kahawa, usimamizi wa vitalu vya miche bora ya kisasa na kuimarishwa kwa mifumo ya ushirika ili waweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea.

Wakizungumza wakati wa ziara ya maofisa wa HRNS wilayani humo, viongozi wa vikundi na AMCOS hizo zilizonufaika na jitihada za shirika hilo walisema matokeo ya jitihada za shirika hilo lililoanza mradi huo miaka mitatu iliyopita, yameanza kuonekana hususani kwenye ongezeko la bei ya zao hili kutoka wastani wa sh 7,000 hadi kufikia zaidi ya Sh 11,000 kwa kilo katika msimu uliopita.

Ongezeko hilo linalotafsiriwa moja kwa moja kuwa ni matokeo ya ubora wa kahawa inayozalishwa na ongezeko la uelewa wa wakulima hao kuhusu bei stahiki za zao hilo.

“Mabadiliko haya yanatafsiriwa moja kwa moja kuwa nafuu kwa wakulima na matumaini mapya kwa vijana wanaotazama kilimo kama ajira yenye heshima,” alisema Bw. Steven Milinga, Mwenyekiti wa Kikundi cha Ngwindi Group chenye wanachama 29 wenye uwiano unaokaribiana wa jinsia.

Kwa mujibu wa Bw. Milinga, mafunzo ya kilimo cha kisasa na ujasiriamali waliyopata kupitia HRNS yamewawezesha kuzalisha miche 30,000 kati ya lengo la miche 150,000. Aidha, kikundi hicho kimefanikiwa kukopa Sh milioni 70 kutoka Halmashauri ya Wilaya, fedha zinazowezesha ujenzi wa nyumba ya kulala wageni katika Kata ya Mpapa, Mbinga Vijijini – hatua inayoashiria kupanuka kwa wigo wa uwekezaji wa wakulima hao.

“Tumepata hamasa kubwa. Tuna ndoto kubwa licha ya changamoto zilizopo, ikiwemo uhitaji wa neti za vivuli kulinda miche, viliba vya kutosha (tube za kuoteshea miche) na kuboresha mfumo wa maji kutoka milimani ili kurahisisha upatikanaji wa maji vitaluni,” aliongeza.

Kwa upande wake, Bi. Grace Ndunguru, Mwenyekiti wa AMCOS ya Kigoti katika kata hiyo, alisema mradi huo umeleta mageuzi ya dhahiri katika uzalishaji na usimamizi. “Tulianza kwa kujifunza kuanzisha vitalu vya miche kutumia mbegu bora tulizopewa kutoka Taasisi ya Utafiti wa zao la Kahawa nchini (TaCRI). Leo tunauza miche kwa wanachama na watu binafsi. Mapato hayo yametuwezesha kujenga ofisi ya kisasa ya AMCOS yetu. Huu ni uthibitisho kuwa tukipata maarifa na umoja, tunaweza,” alisema kwa furaha.

Naye Bw. January Komba, mwanachama na Bwana Shamba wa Kikundi cha Namwang’ina, Kata ya Kitanda, alisema msaada wa mbegu bora, pampu ya maji na viliba vya miche umepunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa miche wakati wa upandikizaji. “Tofauti kati ya zamani na sasa ni kubwa. Tunaona mashamba yenye afya na tija zaidi,” alisisitiza.

Akizungumzia hatua hiyo, Mtaalamu wa Kilimo wa HRNS, Bw. Isack Lungu, alisema kabla ya kuanza kwa mradi huo wakulima walikabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa miche bora, uelewa mdogo wa mbinu za kisasa za kilimo na mitaji haba.

“Walikuwa wanajitahidi, lakini bila zana sahihi na maarifa ya kisasa. Sasa wamejengewa uwezo wa kuanzisha na kusimamia vitalu, kutumia pembejeo kwa usahihi, kupulizia dawa kwa wakati na kuweka mbolea kwa mpangilio unaoongeza tija. Tunaona mashamba yenye afya, mavuno bora na ari mpya ya uzalishaji,” alisema.

Mbali na mafunzo, baadhi ya AMCOS zimepatiwa neti za vivuli (shed nets), viliba vya kuoteshea miche na mbegu bora. Hatua hiyo imeongeza uzalishaji wa miche yenye ubora na inayostahimili magonjwa ya kahawa, ikiweka msingi imara wa uzalishaji endelevu kwa miaka ijayo.

Kwa mujibu wa Bw. Benson Wanyuike, Mhamasishaji (Producer Organiser Trainer) wa HRNS, mafanikio hayo yametokana pia na kuimarika kwa ushirika na uelewa wa masoko. “Tumewekeza katika elimu ya uongozi, uwazi na usimamizi wa vyama. Wakulima sasa wanaelewa haki na wajibu wao, wanashiriki kikamilifu kwenye minada na wanafuatilia bei kwa uelewa mkubwa zaidi. Hata hivyo maboresho hayo kwenye mfumo wa ushirika yanawahakikishia wakulima kunufaika pale soko linapokuwa zuri zaidi,’’ alisema.

Mapinduzi haya hayakuishia shambani pekee. Vikundi 65 vilivyofikiwa vimeanzisha miradi mingine ya kiuchumi ikiwemo ufugaji wa nyuki, samaki, uzalishaji wa maparachichi, pamoja na ujenzi wa nyumba za kulala wageni na ofisi za AMCOS. Mkakati huo wa vyanzo mbadala vya mapato umepunguza utegemezi wa zao moja na kuimarisha ustahimilivu wa kaya kiuchumi.

Aidha, katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, HRNS imesambaza zaidi ya miti 200,000 ya kivuli na matunda kwa wakulima wa Mbinga. Miti hiyo inachangia kuongeza kivuli mashambani, kuboresha afya ya udongo na kufyonza hewa ya ukaa.

“Tunajenga mashamba yanayostahimili joto kali na mvua zisizotabirika. Huu ni uwekezaji kwa kizazi kijacho,” aliongeza Bw. Lungu.

Zaidi, wataalamu hao wa HRNS walitoa wito kwa Serikali na wadau wengine kuendelea kuhamasisha wakulima kujiunga na vikundi na vyama vya ushirika ili kuongeza tija, uwazi na nguvu ya pamoja katika kilimo na biashara ya kahawa.

“Uzoefu wa Mbinga unaonesha wazi kuwa uwekezaji katika elimu ya kilimo, kuimarisha ushirika na mikakati himilivu kwa tabianchi unaweza kugeuza changamoto kuwa fursa. Leo, kahawa ya Mbinga si zao la biashara tu – ni alama ya mageuzi, umoja na matumaini mapya kwa maelfu ya familia za wakulima, na injini mpya ya kuchochea uchumi wa vijijini.’’ Alihitimisha Bw Lungu.

Wakulima wa zao la kahawa wa kikundi cha Mangwagala kilichopo kata ya Kitanda, wilayani Mbinga mjini wakihudumia kitalu cha miche ya zao walipotembelewa na maofisa wa Shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) la nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki. Kikundi hicho ni moja ya vikundi 65 vyenye jumla ya wakulima 2000 walionufaika na program ya mafunzo na uwezeshwaji kutoka shirika hilo inayolenga kuwajengea uwezo wakulima hao kuhusu mbinu bora za kilimo cha kahawa, usimamizi wa vitalu vya miche bora ya kisasa na kuimarishwa kwa mifumo ya ushirika ili waweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea.

Wakulima wa zao la kahawa wa AMCOS ya Kigoti iliyopo Kata ya Mpapa, Mbinga Vijijini wakionesha mbegu bora za zao hilo walizootesha kwenye kitalu chao walipotembelewa na maofisa wa Shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) la nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki. AMCOS hiyo ni moja ya AMCOS 10 na vikundi 65 vyenye jumla ya wakulima 2000 walionufaika na program ya mafunzo na uwezeshwaji kutoka shirika hilo inayolenga kuwajengea uwezo wakulima hao kuhusu mbinu bora za kilimo cha kahawa, usimamizi wa vitalu vya miche bora ya kisasa na kuimarishwa kwa mifumo ya ushirika ili waweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea. Kushoto Mtaalamu wa Mawasiliano wa Kanda kutoka HRNS Bw Muddy Kimweri.


Wakulima wa zao la kahawa wa kikundi cha Ngwindi kilichopo Kata ya Mpapa, Mbinga Vijijini wakionesha mbegu bora za zao hilo walizootesha kwenye kitalu chao walipotembelewa na maofisa wa Shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) la nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki. Kikundi hicho ni moja ya vikundi 65 vyenye jumla ya wakulima 2000 walionufaika na program ya mafunzo na uwezeshwaji kutoka shirika hilo inayolenga kuwajengea uwezo wakulima hao kuhusu mbinu bora za kilimo cha kahawa, usimamizi wa vitalu vya miche bora ya kisasa na kuimarishwa kwa mifumo ya ushirika ili waweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea. Pamoja nao yupo Mtaalamu wa Mawasiliano wa Kanda kutoka HRNS Bw Muddy Kimweri (wa tatu kushoto)

Wakulima wa zao la kahawa wa kikundi cha Uhai Uzena kilichopo Wilayani Mbinga wakionesha mbegu bora za zao hilo walizootesha kwenye kitalu chao walipotembelewa na maofisa pamoja na wataalamu wa kilimo kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) la nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki. Kikundi hicho ni moja ya vikundi 65 vyenye jumla ya wakulima 2000 walionufaika na program ya mafunzo na uwezeshwaji kutoka shirika hilo inayolenga kuwajengea uwezo wakulima hao kuhusu mbinu bora za kilimo cha kahawa, usimamizi wa vitalu vya miche bora ya kisasa na kuimarishwa kwa mifumo ya ushirika ili waweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea. Pamoja nao yupo Mtaalamu wa Mawasiliano wa Kanda kutoka HRNS Bw Muddy Kimweri (kushoto)

Wakulima wa zao la kahawa wa kikundi cha Namwang’ina kilichopo kata ya Kitanda, wilayani Mbinga mjini wakihudumia kitalu cha miche ya zao walipotembelewa na maofisa na wataalam wa kilimo kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) la nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki. Kikundi hicho ni moja ya vikundi 65 vyenye jumla ya wakulima 2000 walionufaika na program ya mafunzo na uwezeshwaji kutoka shirika hilo inayolenga kuwajengea uwezo wakulima hao kuhusu mbinu bora za kilimo cha kahawa, usimamizi wa vitalu vya miche bora ya kisasa na kuimarishwa kwa mifumo ya ushirika ili waweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea.

Wakulima wa zao la kahawa wa kikundi cha Amkeni Kitelea kilichopo wilayani Mbinga wakimsikiliza kwa umakini Mtaalamu wa Mawasiliano wa Kanda kutoka Shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) la nchini Ujerumani Bw Muddy Kimweri wakati maofisa wa na wataalam wa kilimo kutoka shirika hilo walipowatembelea wakulima hao mwishoni mwa wiki. Kikundi hicho ni moja ya vikundi 65 vyenye jumla ya wakulima 2000 walionufaika na program ya mafunzo na uwezeshwaji kutoka shirika hilo inayolenga kuwajengea uwezo wakulima hao kuhusu mbinu bora za kilimo cha kahawa, usimamizi wa vitalu vya miche bora ya kisasa na kuimarishwa kwa mifumo ya ushirika ili waweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea.

Wakulima wa zao la kahawa wa AMCOS ya Kigoti iliyopo Kata ya Mpapa, Mbinga Vijijini wakionesha maendeleo ya ujenzi wa ofisi za AMCOS hiyo walipotembelewa na maofisa wa Shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) la nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki. AMCOS hiyo ni moja ya AMCOS 10 na vikundi 65 vyenye jumla ya wakulima 2000 walionufaika na program ya mafunzo na uwezeshwaji kutoka shirika hilo inayolenga kuwajengea uwezo wakulima hao kuhusu mbinu bora za kilimo cha kahawa, usimamizi wa vitalu vya miche bora ya kisasa na kuimarishwa kwa mifumo ya ushirika ili waweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea. Pamoja nao yupo Mtaalamu wa Mawasiliano wa Kanda kutoka HRNS Bw Muddy Kimweri (wa tatu kushoto)

Mwenyekiti wa Kikundi cha wakulima cha Vumilia kilichopo Kata ya Mpapa, Mbinga Vijijini Bw Reginald Ndunguru (wa pili kushoto) akionesha maendeleo ya mradi wa bwawa la Samaki unaotekelezwa na kikundi hicho walipotembelewa na maofisa wa Shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) la nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki. Kikundi hicho moja ya vikundi 65 vyenye jumla ya wakulima 2000 walionufaika na program ya mafunzo na uwezeshwaji kutoka shirika hilo inayolenga kuwajengea uwezo wakulima hao kuhusu mbinu bora za kilimo cha kahawa, usimamizi wa vitalu vya miche bora ya kisasa na kuimarishwa kwa mifumo ya ushirika ili waweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea.

Wanachama wa kikundi cha wakulima cha Agriculture Arusha kilichopo wilayani Mbinga wakionesha maendeleo ya mradi wa ufugaji nyuki unaotekelezwa na kikundi hicho walipotembelewa na maofisa wa Shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) la nchini Ujerumani mwishoni mwa wiki. Kikundi hicho moja ya vikundi 65 vyenye jumla ya wakulima 2000 walionufaika na program ya mafunzo na uwezeshwaji kutoka shirika hilo inayolenga kuwajengea uwezo wakulima hao kuhusu mbinu bora za kilimo cha kahawa, usimamizi wa vitalu vya miche bora ya kisasa na kuimarishwa kwa mifumo ya ushirika ili waweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea.

Muonekano wa kitalu cha kukuzia miche ya kahawa kinachomilikiwa na AMCOS ya Kigoti iliyopo Kata ya Mpapa, Mbinga Vijijini. AMCOS hiyo ni moja ya AMCOS 10 na vikundi 65 vyenye jumla ya wakulima 2000 walionufaika na program ya mafunzo na uwezeshwaji kutoka shirika lisilo la kiserikali la Hanns R. Neumann Stiftung (HRNS) la nchini Ujerumani Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wakulima hao kuhusu mbinu bora za kilimo cha kahawa, usimamizi wa vitalu vya miche bora ya kisasa na kuimarishwa kwa mifumo ya ushirika ili waweze kujiendesha kwa ufanisi na kujitegemea