MHE BALOZI OMAR AIPONGEZA KAMPUNI YA PUMA ENERGY KWA KUCHANGIA MAENDELO YA KIUCHUMI NCHINI

 

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa pili kulia), Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma Mohammed Abdallah (wa pili kushoto) Mkuu wa Masuala ya Sheria na Mahusiano ya Puma Energy Tanzania, Bw. Emmanuel Bakilana (wa kwanza kushoto) na Mkuu wa Masuala ya Fedha wa Puma Energy Tanzania, Bw. Gibson Mgina (kulia), wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao chao kilichofanyika katika Ofisi Ndogo ya Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,WF, Dar es Salaam)

………………

Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (MB), amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma Mohamed Abdallah katika Ofisi Ndogo ya Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo fupi ya kujitambulisha,, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma Mohamed Abdallah, alitoa taarifa ya utendaji kazi ya Kampuni yake ambapo aliishukuru Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla kwa ushirikiano wanaopatiwa unaoiwezesha Kampuni hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa.

Alisema kuwa pamoja na utekelezaji wa majukumu mengine, Puma Energy Tanzania, imezindua Kituo Mama cha Gesi Asilia (CNG) kilichojengwa katika eneo la Tegeta, mkabala na IPTL, Jijini Dar es Salaam, ambacho ni kikubwa zaidi barani Afrika,

Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amempongeza Mkurugenzi Mkuu na Kampuni ya Puma Energy Tanzania, kwa matokeo yanayotokana na utendaji mzuri wa Kampuni hususani kwa ulipaji kodi na utoaji gawio kwa Serikali, ambapo mafanikio hayo yanachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi nchini.

Aliahidi kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kutoa ushirikiano kwa Puma Energy katika kusaidia kuleta mazingira endelevu ya kibiashara nchini.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkuu wa Masuala ya Sheria na Mahusiano ya Puma Energy Tanzania, Bw. Emmanuel Bakilana na Mkuu wa Masuala ya Fedha ya Puma Energy Tanzania, Bw. Gibson Mgina.

Puma Energy Tanzania ni Kampuni inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Mwekezaji (Puma Investments), inayojihusisha na utoaji huduma ya ununuzi na uuzaji wa mafuta ya usafiri wa anga, ardhini pamoja  na nishati safi ya kupikia (LPG), gesi iliyoshindiliwa (CNG) pamoja na huduma za ziada.