MOI mguu sawa Afcon 2027

TAASISI ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), imesema iko tayari kwa ajili kutoa huduma kwa wanamichezo watakaopatwa na madhira kwenye mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Tanzania itakuwa mwenyeji katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2027 ikiungana na nchi za Kenya na Uganda ambapo maandalizi yanaendelea.

Mkurugenzi wa MOI, Dk Mpoki Ulisubisya amesema taasisi hiyo ina madaktari bingwa sita ambao wanatambuliwa na Shirikisho la Mpira wa miguu (TFF).

Dk Mpoki amesema utaalamu wa madaktari waliopo na wasaidizi unatosha kutoa huduma kwa wachezaji kama itatokea changamoto yoyote kwa mtu kupatwa na mvunjiko au shida nyingine itakayohitaji tiba bobezi.

“Tumejipanga vizuri kwa AFCON, madaktari wetu wanatambulika na Shirikisho la Mpia na mmojawapo alisafiri na timu yetu (Taifa Stars) kwenda Morocco kwenye AFCON (2025). Kwa hiyo tutakuwa Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar tukiwa tayari kutoa huduma. Hatuwezi kutia aibu kwa nchi yetu,” amesema Dk Mpoki.

Mbali na kuwa na madaktari, lakini mkurugenzi huyo amesifu uimara wa vifaa walivyo navyo ambavyo ni vya kisasa vinavyokubalika kwenye utoaji wa huduma kwa viwango vya kimataifa.

Kombe la Mataifa ya Afrika lilianzishwa 1957 na kwa mara mwisho lilifanyika mwishoni mwa mwaka jana nchini Morocco ambako mataifa 24 yalishiriki huku Tanzania ikiingia kwenye hatua ya 16 kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki 1980.