WAKATI hali ya taharuki ikiendelea kuripotiwa katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati kufuatia mshambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran, imeripotiwa wachezaji watatu wa Kitanzania wanaokipiga katika ukanda huo wako salama.
Wachezaji hao ni mshambuliaji Simon Msuva anayekipiga Al Talaba ya Ligi Kuu Iraq, Clara Luvanga (Al Nassr, Saudia) na Morice Sichone (Gulf FC, UAE).
Taarifa ilizozipata Mwanaspoti ni kwamba, eneo alilopo Msuva ni salama na wanaendelea kama kawaida kucheza mechi mbalimbali kwani hadi sasa hakuna ripoti ya kushambuliwa.
Ndugu wa Msuva, James Msuva anayekipiga Coastal Union ya Tanga, amesemawamekuwa wakizungumza mara kwa mara na nyota huyo na amewakikishia kazini kwake kuna usalama.
“Ni kweli amesemakule hali iko shwari, wanasikia milipuko kwa mbali, lakini wapo salama kabisa, maisha yanaendelea na ligi haijasimama,” amesemana kuongeza.
“Klabu imewahakikishia usalama, wanachokifanya sasa ni kuzingatia mpira na kufuata maelekezo ya mamlaka, ila tunachoshukuru kaniambia hali ni shwari kabisa.”
Wakati Msuva hali ikiwa shwari, kwa upande wa mshambuliaji mwingine wa Kitanzania, Morice Sichone huko bado hakujakaa sawa kwani wameendelea kukaa ndani kwa ajili ya usalama zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Sichone alisema: “Hata huku Dubai hali si shwari kabisa, hali mbaya sana tangu juzi saa tano kuna mabomu tu, yaani tunayasikia nje huko, jana kidogo yalipigwa matatu hali ilipopungua tukaenda kucheza mechi ya ligi.
“Ingawa bado tupo ndani tu na tumezuiliwa kutoka nje bila sababu ya msingi kwa ajili ya usalama zaidi lakini wenyeji wanaendelea na shughuli zao.”
Saudi Arabia anapocheza Clara, mapema jana mashambulizi yaliripotiwa, moto mkubwa katika kiwanda cha kusafisha mafuta ulionekana kabla ya kudhibitiwa kwenye eneo la Riyadh iliyopo kambi ya timu hiyo na Ras Tanura kwenye kituo kikubwa cha mafuta.
Mmoja wa mchezaji huyo, Amosi Mlandali aliliambia gazeti hili kuwa: “Clara aliondoka jana kujiunga na timu ya taifa iliyoweka maskani yake Dubai wanapojiandaa na mashindano ya WAFCON, nahisi kama yalitokea basi alikuwa tayari ameondoka.”