Mvua zaharibu barabara, RC Mtambi aomba fedha za dharura

Musoma. Serikali ya Mkoa wa Mara imeomba Sh16 bilioni kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kugharamia matengenezo makubwa ya dharura ya barabara zilizo chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) mkoani humo.

Ombi hilo limechochewa na uharibifu mkubwa wa barabara uliosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha, ambazo zimeelezwa kuwa hazikutarajiwa kwa kipindi hiki. Kutokana na hali hiyo, usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo umeathirika kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Mara kilichofanyika mjini Musoma leo, Jumatatu Machi 2, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema mvua hizo zimesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara, hivyo kuhitaji hatua za haraka.

Amesema juhudi za dharura zinapaswa kuchukuliwa mara moja ili kurejesha barabara hizo katika hali yake ya awali na kurahisisha huduma za usafiri kama ilivyokuwa kabla ya mvua hizo kunyesha.

“Serikali ya mkoa inaendelea kupaza sauti kuhusu changamoto ya barabara zetu. Mimi binafsi nimeandika barua kwa mawaziri husika nikiomba fedha za dharura kutokana na unyeti wa suala hili,” amesema Kanali Mtambi.

Ameongeza kuwa kiwango cha uharibifu ni kikubwa, na iwapo matengenezo hayatatekelezwa kwa wakati, kuna hatari ya barabara kuharibika zaidi na hatimaye kushindwa kupitika kabisa.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ameitaka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuweka alama za kingo za madaraja pamoja na viashiria vya tahadhari katika barabara zilizopo ndani ya hifadhi hiyo, ili kuimarisha usalama wa watumiaji, hasa kipindi cha mvua.

Amesema kwa sasa baadhi ya madaraja ndani ya hifadhi hiyo hayana alama wala kingo, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara hizo.

“Ni muhimu kuweka nguzo au reflectors (viakisi mwanga) kuonyesha kingo za madaraja kwa pande zote. Pia ziwekwe alama za tahadhari zinazoonyesha kuwa maji yakifikia kiwango fulani, watumiaji wasivuke daraja hilo kwa kuwa ni hatari. Hatua hizi zitasaidia kuimarisha usalama na hata kuboresha zaidi sekta ya utalii katika hifadhi yetu,” amesema.

Wakichangia hoja katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe wamesema hali ya barabara katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ni mbaya na inahitaji juhudi za haraka ili kupunguza adha wanazokumbana nazo wananchi.

Mbunge wa Tarime Mjini (CCM), Ester Matiko amesema barabara za mji wa Tarime, hususan zilizo chini ya Tarura, zinahitaji matengenezo ya haraka ili ziweze kupitika.

“Nilifanya ziara ya kata kwa kata na nilipofika Kata ya Nyandoto nilishindwa kuendelea kwa sababu barabara hazikupitika. Pia barabara ya Rebu imeharibika vibaya na imekuwa chanzo cha vifo na majeruhi. Tunaomba suala hili liangaliwe kwa umakini mkubwa kwa kuwa hali si nzuri,” amesema Matiko.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini, Matera Newland amesema hali ya barabara katika halmashauri yake ni mbaya, huku baadhi ya barabara zikiwa hazipitiki kabisa.

Ameomba ufuatiliaji wa karibu ufanyike ili kuhakikisha ombi la fedha za dharura linapatiwa ufumbuzi, akisisitiza kuwa wananchi wanahitaji hatua za haraka kurejesha hali ya kawaida ya miundombinu hiyo.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mara, Ezra Daniel, alisema ofisi yake imepanga kutumia zaidi ya Sh20.6 bilioni katika mwaka wa fedha 2026/27.

Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo, Sh17.3 bilioni zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara, huku Sh3.2 bilioni zikielekezwa kwenye utekelezaji wa miradi midogo ya maendeleo.

Kwa upande wake, Meneja wa Tarura Mkoa wa Mara, William Gyunah, amesema wameomba bajeti ya Sh47 bilioni  kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema bajeti hiyo imeombwa kupitia vyanzo mbalimbali, ikiwemo fedha za tozo, Mfuko Mkuu wa Jimbo, Mfuko wa Barabara na Mfuko wa Maendeleo, kwa lengo la kuboresha hali ya miundombinu ya barabara mkoani humo.