Unguja. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (DCEA), kwa kushirikiana na Kikosi Kazi cha Kupambana na Uhalifu Mkubwa wa Kupangwa (ZTOCTF), imebaini mbinu mpya za usambazaji wa dawa za kulevya kwa kutumia bidhaa za kawaida.
Katika operesheni maalumu iliyofanywa na kikosi hicho, wamekamata pipi, chokoleti, korosho na shisha zenye majina ya ELF Bar na Freshy, ambazo ndani yake zilikuwa na viambata vya dawa za kulevya aina ya bangi, cocaine na LSD, zikiwa na uzito wa kilo 7.448.
Kukamatwa kwa dawa hizo kunathibitisha kuwa wahalifu wanabadilisha mbinu, wakitumia bidhaa za kawaida za chakula na burudani kusambaza dawa za kulevya, huku walengwa wakiwa ni watoto chini ya miaka 18 na vijana.
Bidhaa hizo ziliuzwa katika maduka ya Popeyes UK Treatz na Shop N’GO katika mikoa ya Kusini Unguja na Magharibi, maeneo ya Paje, Jambiani, Mbweni na Shangani, pamoja na ghala lililopo eneo la Mpendae.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Jumatatu, Machi 2, 2026, Kamishna wa Mamlaka hiyo, Kanali Burhani Zuberi Nassor, amesema operesheni hiyo ilifanyika Januari 25 na 29, 2026.
“Katika operesheni hiyo, tulifanikiwa kukamata pipi, chokoleti, korosho na shisha zenye majina ya ELF Bar na Freshy, ambazo ndani yake zikiwa na viambata vya dawa za kulevya aina ya bangi, cocaine na LSD, zikiwa na uzito wa kilo 7.448, zikiwa zinauzwa katika maduka hayo kama bidhaa halali,” amesema Nassor.
Kwa mujibu wa Kanali Zuberi, uchunguzi wa awali umebaini bidhaa hizo zimetengenezwa katika vifungashio vya kibiashara vyenye muonekano wa kuvutia na ladha zinazowavutia watumiaji, wakiwemo watoto na vijana, bila kutambua hatari iliyomo ndani yake.
“Ladha hizo ni grape ice, mango ice, bubble gum, watermelon ice, strawberry ice, peace ice, strawberry kiwi na nyingine nyingi,” amesema.
Uchunguzi uliofanywa unaonesha dawa hizo za kulevya zinaingizwa nchini na raia wa Romania, Alexandru Rozescu (25), mkazi wa Mbweni, kupitia “Zebra Retail Investment,” na kisha kusambazwa ndani ya nchi na nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Zambia na Malawi.
Amesema tayari mtuhumiwa Alexandru amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Watuhumiwa wengine waliofikishwa mahakamani kwa kukutwa na bidhaa hizo ni Nahid Bandar Imtiz (33) na Farhad Mustafa Gulam (33), wote raia wa Tanzania wenye asili ya India.
Aidha, watuhumiwa wengine waliohusika kusaidia kuingiza, kusambaza au kunufaika na biashara hiyo haramu watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapo kamilika.
Vyombo vya usafiri vilivyokamatwa kuhusiana na uhalifu huo ni magari matatu aina ya Toyota Town ICE, Toyota Harrier na Toyota Alphard, pamoja na pikipiki sita aina ya TVS.
Kwa mujibu wa wataalamu, dawa hizo zisipodhibitiwa zitasababisha changamoto za afya ya akili, kupoteza fahamu, vifo vya ghafla, mshtuko wa moyo, saratani ya mapafu, kupoteza uwezo wa kunusa, mabadiliko ya ghafla ya tabia, na kuongezeka kwa uhalifu nchini.
Pia, itasababisha madhara makubwa kwa kuongezeka kwa waraibu wapya, hasa watoto chini ya miaka 18 na vijana.
“Tunatoa wito kwa wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla kuwa makini na bidhaa tunazonunulia watoto na zile zinazoonunuliwa na vijana, hususani bidhaa mpya au zenye vifungashio visivyozoeleka,” amesema.
Baadhi ya wananchi wamesema hawana uelewa wa kutosha juu ya namna ya kubaini bidhaa salama na zisizo salama.
Khadija Ali Salum, mkazi wa Magomeni, ameomba mamlaka kutoa elimu ili kuwapa wananchi uelewa wa kubaini bidhaa hizo na kuwaepusha watoto kupata madhara.
“Kama hali ni hii, basi hakuna aliye salama, maana wananchi hatuna uelewa kuhusu masuala haya. Tunaomba elimu kubwa itolewe, na hatua kali zichukuliwe kwa wanaofanya uhalifu huu maana wanataka kutuharibia watoto,” amesema Hamad Haji, mkazi wa Kilimani Unguja.