Rais Samia apanga pangua mabalozi, yumo mrithi wa Polepole

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uhamisho na kuwapangia vituo vya kazi mabalozi huku baadhi wakirejeshwa nchini akiwemo Balozi Mobhare Matinyi aliyekuwa Sweden.

Katika mabadiliko hayo, Luteni Jenerali Mathew Mkingule aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia amepelekwa Cuba kwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Humphrey Polepole ambaye Julai 13, 2025 alitangaza kujiuzulu.

Taarifa ya mabadiliko hayo imetolewa leo Jumatatu, Machi 2, 2026 na Bakari Machumu, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu akimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Luteni Jenerali Mkingule anapangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba ikiwa ni siku 301 tangu Polepole alipovuliwa hadhi ya ubalozi Agosti 5, 2025 na Rais Samia ikiwa ni siku chache tangu alipotangaza kujiuzulu.

Rais Samia alichukua hatua hiyo zikiwa zimepita wiki chache tangu Polepole kudai kumwandikia barua kumweleza kuhusu uamuzi wake wa kujiuzulu, huku katika barua hiyo aliyoiweka kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, akilalamikia baadhi ya mambo.

Katika barua hiyo ya Julai 13, 2025 aliyoiweka kwenye ukurasa wake wa Instagram, Polepole alieleza kufikia uamuzi huo kwa sababu ya kile alichoeleza ni kusikitishwa na mwelekeo wa uongozi usiojielekeza katika kusimamia haki, amani na kuheshimu watu.

Polepole siyo mtu wa kwanza kuvuliwa ubalozi, wapo mabalozi wengine waliowahi kuvulia hadhi hiyo na marais waliopita.

Polepole amewahi kuhudumu nafasi ya mbunge wa kuteuliwa, mkuu wa wilaya na katibu wa itikadi, uenezi na mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Pia, aliwahi kuwa mjumbe wa kamati ya mabadiliko ya Katiba.

Mbali na mrithi wa Polepole, Rais Samia amemteua Balozi Togolani Mavura kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, New York, akiwa amehamishwa kutoka kituo chake cha awali cha Korea Kusini.

Balozi Cyprian Luhemeja amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia akichukua nafasi ya Luteni Jenerali Mkingule aliyehamishiwa nchini Cuba.

Balozi Salim Othman Hamad amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Comoro akichukua nafasi ya Balozi Saidi Yakubu.

Balozi Maulidah Bwanakheri Hassan amepangiwa kuiwakilisha Tanzania nchini Oman akichukua nafasi ya Balozi Fatma Mohammed Rajab.

Pia, Balozi Suleiman Suleiman amepangiwa kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini China, akichukua nafasi ya Balozi Khamis Mussa Omar.

Balozi Omar kwa sasa ni Waziri wa Fedha wa Tanzania.

Balozi Swahiba Mndeme amepangiwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden akichukua nafasi ya Mobhare Matinyi.

Matinyi anarejeshwa nchini kutoka kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, akiwa amehudumu kwa siku 342 pekee tangu alipoteuliwa Machi 25 mwaka 2025.

Kabla ya kuwa Balozi, Matinyi aliwahi kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali ambapo Desemba 8, 2024 aliteuliwa kuwa balozi lakini hakupangiwa kituo cha kazi.

Taarifa hiyo imeeleza, Balozi Musa Haji Ali amepangiwa kuwa Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa New York akichukua nafasi ya Hoyce Temu.