Richardson Ng’ondya atangaza vita mpya Geita Gold

KIUNGO mshambuliaji wa Geita Gold, Richardson Ng’ondya amesema kufanya vizuri kwa washindani wao wakubwa msimu huu, ni jambo linalowaongezea morali ya kupambana zaidi, ili kwa pamoja wafikie malengo ya kuirejesha tena timu hiyo Ligi Kuu.

Nyota huyo, amesemaubora wa benchi la ufundi na wachezaji wa kikosi hicho unawapa motisha ya kuipambania timu hiyo ili irejee tena Ligi Kuu, baada ya kushuka msimu wa 2023-2024, licha ya kasi na ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani wao.

“Mechi hizi za raundi ya pili huwa ni ngumu sana kwa sababu unakutana na timu zenye malengo mbalimbali, sisi wachezaji tumejipanga ipasavyo, licha ya Ligi kwa sasa haitabiriki hususani unapocheza viwanja vya ugenini,” amesemaNg’ondya.

Nyota huyo aliyecheza Azam FC chini ya miaka 20, African Sports, Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na Mbeya City, amejiunga na Geita Gold msimu huu, baada ya kuachana na Kagera Sugar, huku akiwa tayari ameifungia mabao matatu.

Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, kutoka Ligi Kuu hadi Ligi ya Championship, kabla ya mechi ya jana dhidi ya Gunners, inashika nafasi ya pili na pointi 46, sawa na za vinara, Kagera Sugar, ila zikitofautiana kwa mabao ya kufunga.