SERIKALI, WADAU WA MAENDELEO WAKUTANA KUHAKIKI MPANGO WA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI

* Huku Nchi za Afrika zikitakiwa kufanya biashara za pamoja, Wananchi waitwa kutoa maoni…

Na Leandra Gabriel, MMG

KATIKA Kuhakikisha biashara, uwekezaji na uchumi wa Nchi unakua Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wadau mbalimbali wa Maendeleo wameendelea kujadili, kutoa maoni na mapendekezo yatakayowezesha kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji pamoja na kuiandaa jamii kuona wadau wa maendeleo ni wadau wakubwa katika kuyafikia maendeleo hayo.

Akizungumza leo katika ukumbi wa Johari Rotana Jijini Dar es Salaam Katika mkutano wa Uhakiki wa Mpango wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema, kuelekea utekelezaji wa Dira 2050 Serikali imekamilisha maandalizi ya rasimu ya mkakati wa pili wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ‘ MKUMBI’ na hatua inayofuata ni kuwarudishia wadau waliotoa maoni waone namna gani maoni yao yamezingatiwa.

“Katika kuhakiki maoni hayo yaliyotolewa na wadau mbalimbali leo tumekutana na Mabalozi wanaoziwakilisha Nchi mbalimbali hapa Nchini na wawakilishi wa mashirika ya Kimataifa ambao wapo hapa Dar es Salaam na Dodoma wamepitia nyaraka hizi na tutawafikia wadau wengi zaidi wakiwemo wakuu wa mikoa, makatibu Tawala na wakurugenzi wa Halmashauri kwa Kuwa masuala mengi yatatekelezwa katika ngazi ya Serikali za Mitaa.’’ Ameeleza.

Prof. Kitila amesema kuwa rasimu ya mpango huo hiyo imebainisha maeneo kumi na moja ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi pamoja na changamoto 59 zilizoibuliwa na wataalam ambazo zinakwaza biashara na uwekezaji na wamependekeza hatua za kimageuzi 246.

Ametaja maeneo kumi na moja ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi pamoja na mazingira ya kuanzisha biashara, maeneo ya kufanyia biashara, mitaji, mazingira ya kidijitali, ustadi, mafunzo na utafiti, masoko, miundombinu ya huduma, utatuzi wa migogoro, ulinzi wa Hakimiliki, kubadili mitazamo na uwajibikaji pamoja na usimamizi, ufuatiliaji na upimaji.

Aidha amehimiza Bara la Afrika kukuza ushirikiano katika biashara hususani katika masoko na biashara za pamoja na kuwa timu moja kupitia Jumuiya zao ikiwemo ya Afrika Mashariki na SADC na kutumia vizuri soko la pamoja ambalo biashara hufanyika kwa asilimia 16 pekee.

Kuhusiana na ushiriki wa wananchi katika kufanikisha Dira ya Maendeleo 2050 Waziri Kitila amesema baada ya kukamilishwa kwa rasimu wanaiweka hadharani ili wadau na wananchi waweze kutoa maoni yao kupitia tovuti ya Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji http://www.popi.go.tz ili kuboresha rasimu hiyo kabla ya haijaingizwa kwenye mchakato wa kufanya maamuzi ndani ya Serikali na kusisitiza kuwa kufikia mwezi wa nne itaingizwa rasmi katika mchakato wa kufanya maamuzi ndani ya Serikali na baadaye kuidhinishwa rasmi.

Awali Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Uwekezaji na Mipango Dkt. Fred Msemwa alieleza kuwa licha ya Tanzania kutajwa katika ukuaji wa uchumi kukamilika kwa mpango huo kutachochea zaidi ukuaji wa uchumi, ajira, uboreshwaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji pamoja na kuandaa Sera, Sheria na Mipango ya kuhakikisha sekta binafsi zinafanya kazi katika mazingira rafiki huku watanzania wakinufaika na uwekezaji huo na pato la Taifa kwa ujumla likiendelea kukua.

Mkutano huo umeikutanisha Serikali, Mabalozi wanaowakilisha Nchi mbalimbali zikiwemo Zambia, Ujerumani, Marekani, Vietnam, Comoro, mwakilishi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, Italia na Hispania ambao kupitia nyaraka zilizowasilishwa kwao walitoa maoni na wamekubali mapendekezo hayo kwa kueleza kuwa yatasaidia sana iwapo yatatekelezwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa, kuelekea utekelezaji wa Dira 2050 Serikali imekamilisha maandalizi ya rasimu ya mkakati  wa pili wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ´Mkumbí  na hatua inayofuata ni kuwarudishia wadau waliotoa maoni waone  namna gani maoni yao yamezingatiwa. Leo jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Uwekezaji na Mipango Dkt. Fred Msemwa akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa licha ya Tanzania kutajwa katika ukuaji wa uchumi kukamilika kwa mpango huo kutachochea zaidi ukuaji wa uchumi, ajira, uboreshwaji wa mazingira ya ufanyaji biashara. Leo jijini Dar es Salaam.

Prof. Faustine Kamuzora, Katibu wa Timu ya Kitaifa ya Kiufundi (NTT) akizungumza katika mkutano huo.